Nilishtuka kidogo!
Mzee Mkinga alianza kwa kutufagilia Ndg. January Y. Makamba, mimi na vijana wengine lakini akasema muda bado. Wanawake aliwashukia moja kwa moja tu kuwa hawatoshi na Tanzania haiko tayari kwa Rais mwanamke, na kwamba CCM huwa kuna hila kama zile alizofanyiwa Mzee Sitta ili kufumba fumba Richmond.
Binafsi, niliona kama anatubagua kwa umri na jinsia zetu. Nikadhani si sahihi kufanya ubaguzi wa wazi namna hiyo. Kama unakubali kuwa sisi ni waadilifu na hauna shaka na uadilifu wetu, kinachofuata ni kutazama utayari wetu, uelewa wetu wa changamoto zinazolikabili taifa letu, maarifa yetu ya kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo, na uzalendo wetu.
Ukiona tunafaa basi unatuchagua. Kwani na sisi tukiamka tukasema wazee wote hawafai sababu uzoefu wao umepitwa na wakati, ni wa kizamani, na kwamba vijana wa sasa wasiwachague tutakuwa tumekosea?
Mzee Mkinga akaelezea kuhusu umuhimu wa uzoefu na kuponda sana kuwa wagombea wa aina yetu hatuna uzoefu wa kutosha, akilinganisha na uzoefu aliokuwa nao Rais Barack Obama wa Marekani kuwa alifanya kazi ya community organizing na useneta kwa muhula mmoja, na uzoefu mkubwa sana kumfanya kuwa Rais, mambo ambayo sisi hatuna. Ofcourse ni mtazamo wake, na ana haki nao, lakini nadhani ni wa juu juu sana.
Nitajizungumzia mimi binafsi na uzoefu - kwamba, wakati nasoma masomo yangu ya udaktari, nilifundishwa mambo mengi sana ya kwenye jamii - sociology, psychology, environmental health, psychiatry, community health, epidemiology, health policy and planning, menejimenti, uongozi, teamwork n.k. - hapa nilipata maarifa ya kutosha ya menejimenti na uongozi.
Baada ya shule nilifanya kazi kama mtafiti nikapata kuzunguka mikoa yote ya Tanzania, mijini na vijijini, nikifanya kazi na watu - nataka niulize, hivi katika hao wenye 'uzoefu' anaouzungumzia Ndg. Mkinga na wenzake wenye mawazo ya namna hiyo, wanao huu uzoefu kama wangu?
Baadaye nikasoma masomo ya uzamili kwenye afya ya jamii (MPH) na kwenye usimamizi wa biashara (MBA) - hapa nikijikita zaidi kwenye mambo ya utafiti, takwimu, usalama wa afya za watu, uongozi, oganaizesheni na menejimenti ya taasisi kwa upana wake - baada ya masomo haya nikaamua kujiajiri mwenyewe kwa kuanzisha kampuni ambayo tuliikuza na kufikia kuzalisha ajira zaidi ya 500 kwa mwaka (za moja kwa moja - direct), na zaidi ya 10,000 indirectly.
Nikiwa kiongozi mkuu mwendeshaji wa makampuni haya, na wenzangu, tuliweza, kwa mfano kufufua kilimo cha zao la pamba Nzega na kukuza uzalishaji kutoka kilo 20,000 mwaka wa kwanza wa mradi na kufikia leo hii (mwaka wa saba) takriban kilo milioni 9 za pamba. Mradi huu unagusa karibu watu laki 4.
Ni nani katika hao wenye 'uzoefu' anaowasema Mzee Mkinga, ana uzoefu wa namna hii?
Nimetoa mifano hiyo ili kuweka wazi hoja kwamba, kila mgombea katika sisi ana uzoefu wa aina yake, na uzoefu wa mtu mmoja, haufanani na uzoefu wa mwingine, na kwamba unapokuwa Rais haufanyi kazi peke yako na kwamba basi wewe unatakiwa uwe unajua kila kitu, na una uzoefu kwenye kila kitu...la hasha!
Kwenye uongozi huwa kuna kufanya kazi kwa timu, wewe ukitumia ujuzi na mamlaka yako kuwashawishi unaowaongoza wakubaliane na vision yako na Chama chako ili mwende pamoja kutekeleza mission yenu nyote hautokwama - nchi itaenda. tena kwa mimi 'upya' ni asset inayopaswa kukumbatiwa, maana tunataka mambo mapya.
Cha msingi tupimwe kama tuna uelewa wa namna ya kuongoza, changamoto za Taifa za leo na za kesho, na suluhu tunazopendekeza kwamba je zinaweza kufanya kazi, na kwamba je tuna weza kuwaunganisha watanzania pamoja tukakimbia kutekeleza vision yetu kama taifa?
Kuna wagombea hapa wamekaa serikalini zaidi ya miaka 30 lakini hawana cha kuonesha cha kutisha sana, zaidi wamekaa miaka yote hiyo wakifanya kazi kwa mazoea tu. Mtu hapimwi uwezo wake kwa kukaa kwenye uongozi miaka mingi sana bali kwa nini amefanya katika kipindi alichokaa humo.
Hata ukae miaka mingapi kwenye serikali ama kwenye chama, bado tu kuna vitu vingi sana hautovijua, lakini haimaanishi utashindwa kufanya maamuzi, maana ukiwa Rais unakuwa kiongozi tu wa taasisi yenye watu wengi, lakini utafanya kazi na wataalamu waliobobea kwenye maeneo yao - wewe unatakiwa uwe msikivu na mwenye utayari wa kupokea ushauri, kuuchambua na kuufanyia uamuzi sahihi.
Nasisitiza tena, kwamba, kazi tunayoomba ni mpya, na sote hatujawahi kuifanya, wenye uzoefu ni wanne, aliyetangulia mbele ya haki, wastaafu wawili (Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa) na aliyepo madarakani, na wote hawa hawagombei tena mwaka 2015. Na kwamba sisi sote tuna uzoefu kwenye mambo mbalimbali mengine tu, na uzoefu wa mmoja ni tofauti na wa mwingine.
Tupimwe kwa kushindanisha hoja za nani anakuja na ubunifu wa namna mpya ya kutatua changamoto zetu.
Kuna wagombea wengine wenye 'uzoefu' kweli na wanatumia gharama kubwa sana kuwakusanya watu wawasikilize lakini hawana wanachowaambia!
No comments:
Post a Comment