Pages

KAPIPI TV

Wednesday, April 22, 2015

WATU SITA MBARONI KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO

Vipande kumi na nane vya meno ya Tembo ambavyo Jeshi la   polisi mkoa wa Tabora ilivikamata mapema wiki hii huko wilayani    Sikonge.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora ACP Suzan Kaganda akiwaonesha baadhi ya waandishi wa habari vipande vya  meno ya Tembo ambavyo vilikamatwa na Jeshi hilo.
Hapa akionesha milipuko aina ya Superpower 90 ambayo   ilikamatwa wiki hii huko wilayani Nzega yenye uzito wa kilo 133

 
Na Allan Ntana, Tabora

JESHI la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kukamata watu 6 wakiwa na vipande 17 vya meno 8 ya tembo kutokana na operesheni maalumu inayoendeshwa na jeshi hilo mkoani hapa dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uharifu na waharifu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora ACP Suzan Kaganda amesema watuhumiwa hao walikamatwa mnamo tarehe 18 Aprili 2015 majira ya saa 1.00 za jioni katika barabara ya Sikonge –Tabora jirani na benki ya CRDB tawi la Sikonge.

Alitaja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Baraka Yohana (29) mkazi wa Mnanira, Kigoma, Rashid Chande (28) mkazi wa Kizanga-Sikonge, Keneth France kutoka Ofisi ya Mshauri wa Mgambo Manispaa ya Tabora, Ibrahimu John (25) mfanyabiashara Tabora, Peter Mollel (31) mfanyabiashara Tabora na Anthon Hamisi (42) mfanyabiashara Tabora.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 282 CXJ wakiwa na vipande hivyo 17 ambavyo ni sawa na meno 8 ya tembo.

Kamanda alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na mara baada ya kukamilisha taratibu za upelelezi watafikishwa mahakamani mara moja.

Kamanda aliongeza kuwa katika msako huo unaoendelea mnamo tarehe 13
Aprili 2015 majira ya saa 11.00 za jioni katika maeneo ya stendi ya mabasi wilayani Nzega mkoani Tabora pia walifanikiwa kukamata watu 3 waliokuwa na milipuko aina ya Power 90 ikiwa na uzito wa kilo 133 iliyokuwa ikisafirishwa kwa gari aina ya Toyota Saloon yenye namba T 347 BFH inayofanya shughuli za taxi mjini Nzega.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano zaidi na mara tu baada ya kukamilika upelelezi watafikishwa mahakamani.

No comments: