Baadhi ya Wasaidizi wa kisheria wakipokea vyeti vya kuhitimu Mafunzo ya Sheria mbalimbali za nchi. |
Tabora
JUMLA ya vijana 23 wakiwemo wanawake 9 na wanaume 14
wamehitimu mafunzo maalumu ya ‘Wasaidizi wa Kisheria’ vijijini yaliyoendeshwa katika
wilaya ya Uyui mkoani Tabora na taasisi ya Jamii Salama Development Volunteers
(JSDV) yenye makao yake makuu mjini Tabora.
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa
na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kupitia Mfuko wa Huduma za Kisheria
(Legal Services Facility-LSF) yaliendeshwa kwa muda wa siku ishirini na tano
(25) chini ya usimamizi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law
Society).
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo
jana, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya
Magharibi Bw.Salvatory Kilasara alisema mafunzo waliyopata vijana hao ni msaada
mkubwa kwa jamii hasa kule vijijini ambako wananchi walio wengi hawana mtu wa
kuwapa mwongozo au msaada wa kisheria utakaowawezesha kupata haki zao kama
inavyostahili.
Ili wafanikiwe katika kazi hiyo ya utoaji msaada wa
kisheria kwa wananchi ikiwemo kusuluhisha migogoro ya wananchi hususani kule
vijijini, Kilasara aliwataka wahitimu hao kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa
weledi, kuweka mbele maslahi ya jamii na kuendelea kujifunza zaidi kwa
wanasheria wengine.
Aliwataka kuongeza mshikamano zaidi na taasisi ya
JSDV, halmashauri ya wilaya Uyui na jamii kwa ujumla, aidha aliasa vijana hao
kusaidia kuelimisha jamii juu ya utokomezaji vitendo vyote vya ukatili na
unyanyasaji kijinsia ikiwemo vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mwakilishi wa Tanganyika Law Society (TLS) Seleman
Pingoni alipongeza jitihada na utayari wa vijana hao kuitetea jamii
inayowazunguka, hivyo akawataka wasiwe watendaji wa ofisini tu bali wawatembelee
wananchi mbalimbali kule vijijini na kutoa mwongozo wa elimu ya sheria katika
jamii na sio kuwa mahakimu.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa JSDV Pascal Kilagula
alisema vijana hao sasa wameiva na wako tayari kuitumikia jamii na kama taasisi
wana matarajio makubwa juu yao, hivyo akawataka kuonyesha ufanisi wa hali ya
juu.
Aidha Kilagula alibainisha kuwa mkakati wa kuanzisha
kituo cha sheria katika kijiji cha Isikizya wilayani Uyui kwa ajili ya
kuwasaidia wananchi uko mbioni kuanza na kituo hicho kitaendeshwa na vijana hao
waliohitimu mafunzo ya msaada wa kisheria chini ya usimamizi wa TLS.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake
Bi.Theresia Kyejo alieleza kuwa wamepata elimu na uelewa wa kutosha
utakaowasaidia kutoa msaada wa kisheria kwa jamii na sasa wana ujasiri na ari
kubwa ya kuwatumikia wananchi hasa baada ya kufanikiwa kutatua na kusuluhisha
jumla ya migogoro 340 katika kata mbalimbali wilayani humo katika kipindi cha
mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment