Pages

KAPIPI TV

Tuesday, February 17, 2015

WAUGUZI WATUMIA TOCHI KUZALISHA WAJAWAZITO-KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma


KITUO  Cha Afya kilichopo Kijiji cha  Ilagala Kata ya Mwakizega Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma kinakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme na maji na kusababisha wauguzi kutumia  Tochi na vibatari ,katika utoaji wa huduma ya kujifungua kwa kina mama wajawazito.


Hali hiyo inachangiwa na sintofahamu ya uongozi wa wilaya husika kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kushindwa kutatua adha hiyo inayokikabili Kituo hicho kwa muda mrefu,ambapo ni hatari kwa wajawazito wanaohitaji huduma ya kujifungua.


Akifafanua hilo  Afisa Muuguzi wa kituo hicho Niite Kifutumo alisema kituo chake  kinakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi vikiwemo vya kufanyia usafi sanjari na kutokuwepo kwa nishati ya umeme na maji 
Kifutumo alisema kufutia hali hiyo wanalazimika kuwataka Wajawazito kuja na vifaa vya kujifungulia ikiwemo maji na tochi kama nyenzo zitakazosaidia kukamilisha huduma za kujifungua katika Kituo hicho.


“Muuguzi wa usiku anataabika sana hasa mama akichanika kushona ni shida kubwa ,wauguzi watatu tu,tunapeana zamu ya mmoja mmoja , usafi  ni shida ndio maana mnaona damu zimetapakaa muuguzi mmoja hawezi kufanya usafi na kutoa huduma kwa walengwa ipasavyo, anachoka sana ” alisema Kifutumo.


 Mratibu wa Afya ya Uzazi mama na mtoto Mkoa wa Kigoma  Bertha Ndalituki alipohojiwa adha hiyo alisema ni kweli kina mama Wajawazito hutumia vibatari na huenda na maji kwa ajili ya kufanya usafi baada ya kujifungua, amekiri kuipandisha hadhi ya kuwa kituo cha afya ni utashi uliotumika na uongozi husika,kwa kuwa haijakidhi kiwango cha kutoa huduma za uzalishaji zinazotolewa kwasasa.

Ndalituki alishauri wananchi kupitia vikao vya kijiji wajitolee kuongeza tija ya huduma bora ,huku wakisubiri Serikali kukamilisha maboresho ya kituo hicho,hususani mataa makubwa ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma ya uzazi hasa wanawake wajawazito wanaojifungua usiku.
 
Baadhi ya wagonjwa waliokutwa hapo Safi Sadick na Mwajuma Rashid kwa nyakati tofauti wakiri kujifungua kwa kibatari pamoja na lugha chafu wanazopewa na waguzi husika huchangia wanawake wajawazito kujifungua kwa wakunga wa jadi.
 
Akijibia  hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa hapa Leonard Subi alisema kituo kitakarabatiwa hivi karibuni kwa kuwekewa nishati ya umeme na maji na wananchi watasahau changamoto hizo .Wakati  huohuo Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Fidelis Kumbo alisema hana uhakika wa adha hizo kwa wajawazito  .

No comments: