Pages

KAPIPI TV

Tuesday, February 17, 2015

BANGO SANGHO YAWEZESHA WANAFUNZI 150 SHULE YA MSINGI KIBUGUMO KUKETI

DSC_0003
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw akisalimiana na Daktari bingwa wa Afya ya jamii na familia, Dkt. Ali Mzige kwenye hafla fupi ya kukabidhi madawati 50 pamoja majengo mawili ya shule ya msingi Kibugumo yaliyokarabatiwa na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO. Katikati ni Mbunge wa Kigamboni Dk Faustine Ndungulile. (Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).

Na Mwandishi wetu
WANAFUNZI 150 waliokuwa katika dhiki ya elimu shule ya msingi Kibugumo kutokana na kulazimika kusoma wakiwa wameketi sakafuni wamekabidhiwa madawati yatakayowawezesha kusoma kwa raha.

Madawati hayo yamekabidhiwa jana na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO mbele ya shuhuda ya balozi wa India nchini, Debnath shaw.
Pamoja na madawati hayo taasisi hiyo ilikabidhiwa madarasa mawili yaliyokarabatiwa.

Akipokea msaada huo Kaimu Ofisa elimu wa Manispaa ya Temeke Angelina Nasazwa, alisema umekuja wakati muafaka hasa kwa kuangalia changamoto nyingi zilizopo katika shule hiyo, ikiwemo miundombinu ya madarasa na ofisi.
DSC_0026
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw (wa pili kulia) akiteta jambo na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (kulia) kwenye hafla fupi ya kukabidhi madawati 50 pamoja majengo mawili ya shule ya msingi Kibugumo yaliyokarabatiwa na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO.

Alisema kukabidhiwa kwa madawati na majengo hayo kunapunguza shida iliyopo na kufanya mazingira ya kusomea kwa wanafunzi wengi kuwa rafiki.

Aidha pamoja na kutoa shukrani kwa umoja wa Bango Sangho na pia kwa balozi mwenyewe kwa kusaidia shule hiyo, ofisa huyo alisema kwamba jumuiya hizo zimefanya vyema kuwakumbuka watoto hao ambao walikuwa na changamoto kubwa za kusoma wakiwa wameketi huku wakiwa hawajui kwamba kwa matatizo hayo wamekuwa wakikosa haki zao za msingi za elimu bora.

Hata hivyo pamoja na kupokea misaada hiyo aliwataka watu Bango Sangho kuendelea kutoa ushirikiano kwa shule hiyo ambayo inakabiliana na changamoto nyingi.

Naye Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustine Ndungulile aliwapongeza watu wa Bango Sangho kwa kuiona shule hiyo ya Kibugumo na kusema wananchi wa Kibugumo watauenzi msaada huo kwa kutunza madawati na madarasa hayo ambayo yamepatikana kutokana na kujinyima kwa wanachama wa Bango Sangho.
DSC_0036
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw akipokea zawadi ya maua kutoka kwa mmoja watoto wa shule ya msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Alisema mchango wa wanajumuiya ya Bango Sangho ni muhimu hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya sera ya elimu itakayoanza kutumika mwakani, ambayo inatarajia kuleta mapinduzi makubwa ya elimu nchini.

Mbunge huyo ameahidi kuendeleza ushirikiano na jumuiya hiyo huku akiahidi ushirikiano pia katika uendesha kliniki kwa wanafunzi wa shule ya Kibugumo.

Bango Sangho ni jumuiya ya wananchi wa India wanaoishi nchini Tanzania ambao hujishughulisha na masuala ya utamaduni na kidini na wakati mwingine hutoka na kusaidia jumuiya zingine hasa watoto.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Amit Nandy akimkaribisha mgeni rasmi balozi wa India kuzungumza machache, alisema pamoja na majukumu ya jumuiya hiyo katika masuala ya kidini na utamaduni,wamekuwa wakishirikiana na taasisi nyingine kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
DSC_0047
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kibugumo, Mzamilo Ally (kushoto) akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Balozi wa India nchini Tanzania, Mh. Debnath Shaw kuzungumza na wageni waalikwa.

Alisema walikabidhiwa jukumu la kusaidia shule hiyo miaka miwili iliyopita na kwamba wanashukuru wametimiza azma hiyo na sasa wanataka kufanya matibabu bure kwa wanafunzi kama kamati ya shule na serikali ya eneo hilo itakubali.

Awali Mwalimu Tatu Mhina akisoma risala ya kuukaribisha ugeni huo shuleni Kibugumo, alisema bado wana changamoto kubwa kubwa kutokana na shule hiyo kuwa na wanafunzi 1000 huku wengi wao wakiwa na tatizo la miundombinu, madarasa, ofisi za walimu na madawati.

Alisema pamoja na kwamba bado wana madarasa lakini madarasa yamechakaa na hivyo kuhitaji kuangaliwa.

Aidha baadae mwalimu huyo katika mahojiano alisema kwamba wanachangamoto ya chumba cha kompyuta na umeme na kwamba wanafundisha somo la tehema bila uhalisia.
DSC_0137
Mwalimu Tatu Mhina wa shule ya msingi Kibugumo akisoma risala iliyoandaliwa na walimu wa shule hiyo kwa mgeni rasmi Balozi wa India nchini (pichani meza kuu).

Pamoja na kuomba ushirikiano pia mwalimu Tatu alisema upo uwezekano wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 wakati wa kamepni za vijijini vya ujamaa, kupata umeme kwa kuwa nguzo zimepita karibu kinachotakiwa kwa wahusika kuliona hilo.

Naye balozi wa India nchini amesema amefurahishwa kushuhudia uhusiano mzuri uliopo kati ya wakazi wa Kibugumo na jamii ya India inayoishi nchini Tanzania kupitia Bango Sangho.

Alisema ushirikiano huo anatarajia kuona ukiendelea kwa manufaa ya jamii zote mbili za Kibugumo na Bango Sangho.
DSC_0190
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Kibugumo kwenye hafla ya kukabidhi madawati 50 na majengo mawili yaliyokarabatiwa na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO.
DSC_0228
Baadhi ya wajumbe wa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO wakimsikiliza mgeni rasmi kwenye hafla hiyo.
DSC_0231
Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi madawati 50 pamoja na majengo mawili yaliyokarabatiwa na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO katika shule ya msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
DSC_0168
Mwenyekiti wa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO, Amit Nandy akielezea nia na madhumuni ya umoja huo ambao utaendelea kusaidia jamii zenye uhitaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa ikiwa ni pamoja na kudumusha ushirikiano baina ya nchi ya Tanzania na India.
DSC_0103
Kaimu Afisa Elimu Manispaa ya Temeke, Angelina Ngasazwa akitoa neno la shukrani kwa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO kwa msaada walioutoa shule ya msingi Kibugumo.
DSC_0245
Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile akiongoza ugeni huo kuelekea eneo la tukio kwa ajili ya zoezi la kukabidhi majengo mawili yaliyokarabatiwa na umoja wa Bango Sangho.
DSC_0254
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw akikata utepe kuzindua moja ya majengo ya shule ya msingi Kibugumo yaliyokarabatiwa na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO kwenye hafla fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki Kigamboni jijini Dar. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (wa tatu kushoto), Mwenyekiti wa umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO, Amit Nandy (wa pili kushoto) Pintu Dutta na Dipankr ambao ni wajumbe wa umoja huo.
DSC_0255
DSC_0260
Balozi wa India nchini, Mh. Debnath Shaw na Mbunge wa jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile wakikagua moja ya jengo la darasa lililokarabatiwa na kuwekwa madawati mapya na umoja wa jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo hapa Tanzania, BANGO SANGHO.
DSC_0266

No comments: