Na Mwandishi wetu, Tabora
VYAMA vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) vimeanza kueleza kiini cha wananchi wengi bila kujali itikadi
zao kuwaamini na kuwaunga mkono kwa kuwapigia kura nyingi katika uchaguzi wa
serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Viongozi wa vyama hivyo wamesema kitendo cha vyama
vya CUF, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI na NLD kuunganisha nguvu zao na wanachama wao
wote pasipo kujali itikadi zao za dini, kabila, chama, rangi, elimu, ukanda au
ukubwa wa chama kimewafanya wananchi wengi kuwa kitu kimoja na kujadili mipango
yao ya maendeleo kwa pamoja.
Wakizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wananchi
uliofanyika jana katika Mtaa wa Rehani kata ya Ng’ambo katika Manispaa ya
Tabora viongozi hao wamesema kuwa fitna za viongozi wa CCM ndizo zilikuwa
zinawafanya watengane katika itikadi zao za dini,vyama na ukabila, lakini sasa
baada ya kuungana katika UKAWA hakuna fitna tena za itikadi wala makundi, sasa
wanawaza maendeleo tu na namna ya kuiondoa CCM.
‘UKAWA imetuunganisha sasa tumekuwa kitu kimoja,
hatuna itikadi tena za vyama, kabila, dini wala ukanda, ndio maana tumeanza
kukubalika sana na kupata ushindi mkubwa na bado, hata wana CCM watatuunga
mkono tu’, alisema Ijihad Msabaha Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgumia kata ya Ng’ambo
kupitia CUF katika Manispaa ya Tabora.
Aidha Msabaha alisema kitendo cha wananchi wengi
kuiunga mkono UKAWA na kuwapa ushindi mkubwa katika maeneo mengi hapa nchini ni
mwanzo tu, funga kazi inakuja katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa Madiwani, Wabunge
na Rais.
Mwenyekiti wa
Mtaa wa Msufini katika kata hiyo Bw.Kambi Idd Baruani (CUF) alisema UKAWA
imeunganisha wananchi wote na imerudisha heshima ya kisiasa iliyokuwa imeanza
kupotea ‘‘umoja ni nguvu”, sasa wananchi kaeni mkao wa kula, tumepata chombo
imara cha kutuunganisha Watanzania wote, wenzetu ambao hamjaingia katika umoja
huu ingieni sasa kazi ndio inaanza, CCM bye bye!.
Akizungumzaa katika mkutano huo wa shukrani, Kada mhamasishaji
maarufu na Meneja wa kampeni za UKAWA kupitia CHADEMA Bw.Elia Daudi alisema UKAWA
imeondoa chuki zote za kisiasa, itikadi za dini na ukabila na vyama vyote
vimekuwa kitu kimoja, sasa wana kazi moja tu ya kuwatumikia wananchi.
Aidha alisema kushindwa kwa CCM katika uchaguzi
uliopita hawapaswi kutafuta mchawi bali ni kitendo chao cha kutokubali ushauri
kwa mambo yenye maslahi kwa nchi, kutodhibiti wala rushwa, kukumbatia viongozi
wezi wa rasilimali za nchi jambo ambalo linakwamisha maendeleo na kutelekeza baadhi
ya makada na waasisi wake.
‘Ninyi Watanzania mnaong’ang’ania CCM mliacha kitu
gani kule, miaka yote hicho mlichoacha mbona hamjakipata…mna iamini sana CCM
kwa lipi, kwa nini msiwaambie waache wizi wa mali za umma na rushwa…kwa nini
muamini chama kinachokumbatia wala rushwa na wezi, wakati umefika sasa wa
kuiondoa CCM madarakani’, aliongeza.
Mjumbe wa serikali ya Mtaa Kaze Hill kata ya Ng’ambo
Bw.Mapenzi Simoni Mbwambo kupitia CHADEMA alibainisha wazi kuwa mafisadi sasa
hawaiogopi serikali ya CCM kwa sababu haiwabani ipasavyo bali inawabembeleza tu
hivyo akawataka wananchi kuunga mkono UKAWA kwa kuwa ndio kiboko ya wezi wa
mali za umma wote hapa nchini.
Baada ya kupata uongozi Mwenyekiti wa Mtaa wa Kizigo
katika kata hiyo kupitia CHADEMA Bw.Paul Malilo na Bi.Zaina Ismail mjumbe wa
Mtaa wa Mgumia (CUF) walieleza kuwa sasa
wameanza kuwatumika wananchi kwa vitendo kwa kuanzia wamewaomba wananchi
wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo wajiunge katika vikundi, tayari
mikopo hiyo inashugulikiwa kutoka taasisi mbalimbali.
Nao Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani Bw.Maganga Haruna
(CUF) na Mjumbe wa Mtaa wa Filta-Kitete Bw.Ezra Abisai (NCCR Mageuzi) walieleza
kuwa ahadi ya kuwaletea maendeleo wananchi imeshaanza kufanyiwa kazi, wapo mbioni
kuanzisha miradi 2 katika kata hiyo na wameanza kufuatilia matumizi ya michango
inayotolewa shuleni na walimu wakuu wanaotoza michango kiholela pasipo
kuwashirikisha wazazi.



No comments:
Post a Comment