Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai (wa kwanza kushoto)
wakielekea kwenye ukumbi wa mkutano kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa
semina ya uimarishaji Chama kwa mabalozi wa Lindi Mjini tarehe
29.12.2014.
Mke
wa Rais na Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM Mama Salma Kikwete akiongea na
wajumbe zaidi ya 1000 waliokuwa wanahudhuria semina ya uimarishaji wa
Chama Cha Mapinduzi kwa mabalozi wa Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai
akifungua rasmi semina ya siku moja ya kuimarisha Chama kwa mabalozi wa
Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai
akifungua rasmi semina ya siku moja ya kuimarisha Chama kwa mabalozi wa
Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
Baadhi ya washiriki wa semina ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa
mabalozi wa Lindi Mjini wakifurahia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai wakati akifungua semina hiyo
huko Lindi tarehe 29.12.2014.
Mke
wa Rais na Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM Mama Salma Kikwete akiaagana na
Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai
aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi rasmi wa semina ya siku
moja ya mabalozi wa Lindi Mjini tarehe 29.12.2014.
Baadhi
ya watoa mada (waliokaa mstari wa mbele) kwenye semina ya kuimarisha
Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya mabalozi wa Lindi Mjini tarehe
29.12.2014.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Matukio ya kutishia
amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi wa nyumba kumi
watafanya kazi zao kwa uaminifu kwani wao ni viongozi wa kwanza walio
karibu na wananchi hivyo basi wanatakiwa kuwafahamu wakazi wa maeneo
yao.
Hayo yamesemwa jana na
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ally Vuai
wakati akifungua semina ya siku moja ya uwezeshaji wa chama hicho kwa
mabalozi (viongozi wa mashina) wa wilaya ya Lindi mjini.
Vuai alisema Balozi ni
kiongozi wa kwanza anayetakiwa kujua idadi ya wakazi wake, kazi
wanazozifanya na majina yao kitendo ambacho kitasaidia kuimarisha
usalama wa eneo husika lakini miaka ya hivi karibuni wameacha kufanya
kazi hiyo kwa uadilifu na kuviachia vyombo vya dola pekee.
“Jukumu la kulinda amani
ya nchi na usalama wa taifa letu ni la kila mtu, lakini hivi sasa kazi
hiyo vimeachiwa vyombo vya dola pekee, mabalozi fanyeni kazi ya
kuwatambua wakazi wa maeneo mnayoishi hii itasaidia kumtambua mualifu
pale atakapofika katika eneo lenu”, alisema Vuai.
Alisema kikao cha kwanza
cha CCM ni kikao cha shina hivyo basi mabalozi ni viongozi wa muhimu
ndani ya shina wanatakiwa kutetea ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 na
kutowaachia viongozi wakuu wa chama pekee kufanya kazi hiyo.
Vuai alisisitiza, “Muwe
na uthubutu wa kujibu hoja potofu za wapinzani na kutokubali wawapotoshe
wananchi juu ya mafanikio yaliyofanywa na Serikali. Kipindi
cha uchaguzi kikifika endeleeni kuwahimiza na kuwasimamia wananchi
wakapige kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura”.
Aliwataka mabalozi hao
kuhakikisha wakati wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga
kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani
wawahimize wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
majina yao.
Kwa upande wake Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini
Mama Salma Kikwete alisema mabalozi ni msingi na nguzo ya chama bila ya
mabalozi chama hakiwezi kwenda vizuri ni kama vile binadamu anaweza kuwa
na kila kitu lakini kama hana miguu hawezi kutembea.
Aliwapongeza kwa ushindi
walioupata wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za
mitaa na kusema kuwa upendo na mshikamano ni msingi wa ushindi na usiri
na uadilifu ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi.
“Katika semina hii
mtafundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi na wajibu wenu kwa
Chama na Jamii inayowazunguka hivyo basi muwe wasikivu na kuyashika
yale mtakayofundishwa na watoa mada”, alisisitiza Mama Kikwete.
Akiongea kwa niaba ya
wajumbe walioshiriki semina hiyo Rashid Thabit kutoka kata ya Rahaleo
alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yatawasaidia katika
utendaji wao wa kazi.
“Tunakushukuru MNEC kwa
ajili ya kuandaa mafunzo haya ambayo yametupa uelewa na wajibu na kazi
zetu kama mabalozi. Uwepo wako wakati wa uchaguzi uliopita ulitufanya
tukashinda kwani tulishiriki pamoja nawe katika kampeni za kuwanadi
wagombea wetu”.
Nawaomba wajumbe
wenzangu tusibweteke na ushindi huu bali tuongeze kasi na bidii na
kuweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani
ili tuweze kulikomboa jimbo la Lindi mjini kutoka mikononi mwa Chama Cha
Wananchi (CUF)”, alisema Thabit.
Semina hiyo ya siku moja
iliyohudhuriwa na wajumbe 993 kutoka kata zote 18 za wilaya hiyo
iliandaliwa na Mama Kikwete ambaye aliwaahidi mabalozi kuwapa mafunzo
hayo ili wajue majukumu yao ya kazi. Mada zilizojadiliwa ni kazi na
wajibu wa mabalozi na katiba mpya iliyopendekezwa.
No comments:
Post a Comment