Pages

KAPIPI TV

Wednesday, December 3, 2014

HALMASHAURI TENGENI BAJETI ZA KUDHIBITI UTAPIAMLO-KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma

INADAIWA kuwa,ili kukabiliana na unyafunzi(Utapiamlo),halmashauri za wilaya Nchini, hazina budi kuitengea bajeti ya fedha  kitengo cha Lishe, kwa dhima ya kuelimisha umma  namna ya kuandaa vyakula vyenye viini lishe na athari  ya ukosefu wa viini lishe kwa wanawake wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Hayo yalibainika kigoma Ujiji,katika mafunzo ya  kazi kwa watumishi wa idara ya afya kutoka katika mikoa ya Tabora na Kigoma kwa kushirikisha  uongozi wa idara ya mipango na fedha za halmashauri husika ,wabaini athari za ukosefu wa lishe kwa lengo la kuiwekea bajeti ya fedha  kitengo cha Lishe,ili kuratibu shughuli zake kwa walengwa .

Akifafanua hilo Ofisa Lishe Mwandamizi Taifa Bupe Mtoga alisema  mafunzo hayo ya siku tatu yana tija ya kubadilishana ufahamu na namna ya kukabiliana na ugonjwa wa utapiamlo  unavyochangia  vifo kwa watoto wenye umri wa 0-5 na wajawazito   kupoteza maisha wakati wa kujifungua na kujifungua watoto kabla ya wakati.

Alisema 42% ya watoto wamedumaa na kila kundi la wanawake 10 wana utapiamlo na 40% ya wananchi hawatumii chumvi yenye madini joto ,hivyo serikali ina mpango endelevu wa kuhakiki kila halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya kuratibu shughuli za lishe kwa kila wilaya na mwisho wa mwaka mkoa uji tathimini katika hilo.

Kwa upande wa Ofisa lishe wilaya ya Igunga mkoani Tabora  Mary Mallya na James Ngalaba wilaya ya Kasulu  Mkoa wa kigoma,kwa nyakati tofauti waliongeza kwa kusema,wananchi wamezoea kula chakula cha aina moja tu , aina ya wanga, protini na kudharau vyakula vyenye vitamin kama mbogamboga na matunda.

 Walisema jamii itumie mazao wanayolima kurutubisha afya kwa kula vyakula vyenye viini vya lishe ambapo ni muhimu katika siku 1000 za kwanza za maisha ya mtoto,ndipo msingi wa ukuaji wa kimwili na akili katika kipindi cha kutunga mimba hadi anapotimiza umri wa miaka miwili .

Akizindua semina hiyo Katibu Tawala wa kigoma Eng.John Ndunguru alisema,serikali kwa kushirikiana  na  Unicef,chuo cha kilimo Sokoine (SUA) na tasisi ya chakula na lishe una mpango wa miaka 10 dhidi ya kuratibu na  kutoa vitamin A  mara mbili kwa mwaka.

Alisema ugumu wa maisha  na ukosefu wa elimu sahihi ya kubaini aina ya vyakula vyenye kiini lishe inachangia kaya nyingi za nchi zinazoendelea kula aina moja ya chakula na kusisitiza maofisa lishe kupitia dawati lishe la wilaya husika watumie fursa ya mafunzo hayo kukabiliana na utapiamlo katika maeneo yao.

Baadhi ya wakazi wa kigoma Jamira Damian na Winifrida Bwire walipohojiwa kama wanaelewa lishe bora  kwa nyakati tofauti walisema ni  pamoja na nafaka za aina mbalimbali,mbogamboga, matunda ,vyakula vya mizizi ,maziwa ,dagaa,mayai,samaki na nyama, ambavyo vinapatikana kigoma na kuasa jamii ,isihadaike na vyakula vya viwandani.
 
Mkakati wa taifa  wa mwaka 2015-16  kila halmashauri ziajiri ofisa lishe ambao wataratibu na kuhakiki kuanzia ngazi ya kaya hadi wilaya  sanjari na uanzishwaji wa dawati la lishe,kwa kuingizwa katika mpango wa bajeti ,ambapo lishe bora kwa mtoto mchanga huanza siku 1000 tangu kuitunga mimba,kuzaliwa hadi atakapotimiza umri wa miaka mitano.

No comments: