Pages

KAPIPI TV

Wednesday, December 17, 2014

CHAMA CHA WAVUVI WATAKA WAFIDIWE-KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma

Chama cha wavuvi   Mkoa wa kigoma ,wameitaka wizara ya uvuvi na mifugo iweke bajeti ya  kuwafidia wahanga wa  janga  la kuibiwa zana za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa nia ya kuwapunguzia machungu ya madhira ya kuhujumiwa  na wahalifu katika shughuli za uvuvi  ziwani takribani  miaka 30.

Hayo yalijiri jana katika mkutano wa wazi uliofanyika katika mwalo wa Kibirizi  baina ya wavuvi  ,wamiliki wa mitumbwi  na uongozi wa  juu la Jeshi la Polisi  la hapa ,ukitaka  kuboresha mahusiano na ushirikiano wa dhati wa kukabiliana na changamoto ya kutekwa kwa wavuvi na uporwaji wa zana  ziwani  humo.

 Hamimu Wanyika  ni miongoni mwa wahanga walioathiriwa na changamoto hiyo alisema alianza shughuli za uvuvi mwaka 1984 na matukio ya uporajwi wa zana za wavuvi zilianza rasmi mwaka 1999 , na ameibiwa( injini) mashine 20 ambapo kwa  mwaka 2014  amebaki na mtumbwi mmoja usiokuwa na injini .

“hivi sasa nakodi injini moja 350 kwa siku 20 nina wake wanne,watoto 25 ,mmoja yupo chuo kikuu Dar-es-salaam ,wawili kidato cha Nne ,saba ni wanaume  wanabangaiza mitaani ,nimeshindwa kusomesha hawa wa kike ntawaoza tu nifanyeje,mwishoni mwa mwaka wizi huwa mkubwa mama acha tu” alisema mhanga huyo.

 Mwenyekiti wa ulinzi wa mazingira mwalo wa kibirizi ( BMU) Juma Hasani alisema kero hiyo ina miaka 30 na inapoteza ajira kwa vijana ,ambapo mtumbwi mmoja huajiri watu 12 na kushauri kamati za ulinzi na usalama wa Nchi zinazopakana na ziwa hilo, washirikiane na wawajibike kuzibiti wahalifu wakati tukio linatokea eneo husika.

Naye Katibu wa Umoja wa wavuvi kigoma(UWAKI) Mohamed Kasambwe alisema idara ya polisi ni chachu ya kuzorotesha adha hiyo,kutokana na wananchi wanaotoa miongozo ya kukomesha uhalifu huwazushia kesi za uongo kwa  kuwatupa mahabusu na wengine kudaiwa ni wahamiaji haramu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa wavuvi Sendwe Ibrahimu alisema changamoto ya wizi ziwani imechangia  injini  800 za wavuvi  kuibiwa na kuitaka wizara husika itenge bajeti kwa ajili ya kuwafidia wahanga sanjari na halmashauri husika ichangie mafuta ya dharura kwa boti la doria ili kuzibiti majambazi katika tukio husika.

Ofisa Uvuvi Manispaa Harouni Chanda alisema awali manispaa ya kigoma ujiji ilikuwa ikikusanya zaidi ya milioni 50 kwa mwaka 2012/13 lakini kutokana na janga hilo wanakusanya chini ya milioni 20 kwa mwaka 2013/14  na kudai wametoa lita 1000  za mafuta kwa idara ya polisi kwa  lengo la kuongeza nguvu ya kupunguza uhaba huo.

Akijibia hayo Kamanda wa Polisi Jafari Mohamed alisema lengo la kukutana na wahanga ni kuweka mkakati wa kuokoa mali za wavuvi kwa wakati ,ambapo serikali haiwezi kuokoa janga kwa wakati kutokana na ukosefu wa fedha za kununua  mafuta  ya `speed boti ya doria kigoma ni shida.

Akubali kuunda kamati ya dharura miongoni mwa wavuvi kwa kushirikiana na Ofisa wa majini Nathaniel Lyambiko ,ambapo watakuwa na akiba ya mafuta na timu ya kikosi kazi ya kubaini wahalifu na namna ya kujipanga katika maeneo tete na kukabiliana na wahalifu husika.

Mkuu wa Mkoa wa kigoma Lt.Issa Machibya  hivi karibuni alitoa  agizo  lisemalo hivi`` kila halmashauri ihakikishe ifikapo 30,Novemba ichangie lita 1000 za mafuta  ili kuondoa adha ya usafiri wa kupambana na wahalifu wakati wa tukio “ .

 kipindi cha machi -Octoba  uporaji wa  zana za wavuvi umefanyika katika mwalo wa kibirizi na muyowozi ,ambapo Novemba 15,23 na 26  injini 15 zilishaporwa na kila injini huuzwa sh.milioni 7 sanjari na kupoteza ajira kwa vijana 180 ,hali inayotishia kuibuka kwa makundi ya kihalifu katika manispaa ya  kigoma Ujiji.

No comments: