Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
BUNGE
limeazimia kuwajibishwa kwa mawaziri Profesa Sospeter Muhongo, Profesa
Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema,
kutokana na sakata la uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow,
iliyokuwa Benki Kuu (BoT) kwa kutaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi
wao.
Mbali
na hao, yumo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Aidha,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuwa Serikali itatekeleza maazimio
yote manane yaliyopitishwa jana jioni na Bunge baada ya mjadala mkali wa
siku tatu na mvutano wa siku moja juzi katika kupitisha maamuzi hayo
ambayo yalifikiwa kwa maridhiano.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe
alisoma maazimio hayo manane jana bungeni baada ya kufikiwa kwa
maridhiano kati ya Kamati yake, Kambi ya Upinzani, Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Serikali.
Maazimio
Katika
azimio la pili, Zitto alisema viongozi hao wa umma na maofisa wa ngazi
za juu serikali wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo
vya kijinai katika sakata hilo, linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania (IPTL).
“Kwa
kuwa vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na
maofisa wa ngazi za juu serikalini, vinakiuka pia maadili ya viongozi wa
umma kuwanyima viongozi na maofisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia
nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
“Hivyo,
basi Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi wao
kutengua uteuzi wao,” alisema Zitto.
PAC
katika mapendekezo yake bungeni, ilitaka Muhongo, Maswi, Jaji Werema,
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele na Waziri Mkuu Pinda
wawajibike kutokana na sakata hilo, lakini wabunge wengi walisema Masele
na Waziri Mkuu Pinda hawakuhusika katika sakata hilo.
Aidha,
kwa mujibu wa Zitto, Bunge limeazimia kuwa Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya
ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki
kwa mujibu wa sheria za nchi kwa watu wote waliotajwa kuhusika na
vitendo vyote vya jinai, kuhusu miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow, na
watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi mbalimbali unaondelea
katika vitendo hivyo vya jinai.
Miongoni
mwao ni mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi, James
Rugemalira wa VIP Engineering Ltd, Jaji Werema, Profesa Muhongo, Maswi,
wajumbe wa Bodi ya Tanesco, ambao inasemwa kuwa walihusika kwa namna
moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha
katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP na VIP Engineering and
Marketing Ltd.
*Wabunge
Azimio jingine la Bunge ni kuazimia Kamati za Kudumu za Bunge
kuwawajibisha viongozi wake kwa kuwavua nyadhifa zao kutokana na kushiriki kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo.
Hao
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Andrew Chenge, Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco.
Chenge
na Ngeleja wametajwa kunufaika na fedha za mwanahisa Rugemalira kwa
Chenge kupewa Sh bilioni 1.6 na Ngeleja Sh milioni 40.2, kwa mujibu wa
taarifa ya CAG na PAC.
“Hivyo
basi, Bunge linaazimia kwamba Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue
hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane
wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa Kamati husika za
Kudumu za Bunge,” alisema Zitto.
*Majaji
Kuhusu ushiriki wa majaji katika kashfa hiyo, alisema Katiba ya
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka utaratibu mahsusi wa
kushughulikia nidhamu ya majaji, ambao kwa mujibu wa Katiba hiyo,
unamtaka Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za
utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Alisema
kwa kuwa utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya majaji kwa mujibu wa
Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati wa
tuhuma dhidi yake unaendelea;
“Hivyo
basi, Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa nidhamu
wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes
Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania,” alisema Zitto.
Aidha,
Bunge limeazimia mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja
Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika
baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na
utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni
taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
*Sheria
Katika
azimio jingine, Bunge limeazimia kwamba Serikali iandae na kuwasilisha
Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la
kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti
vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai
wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo
hivyo.
Pia
Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge kuhusu mikataba mibovu ya
kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua umeme,
hivyo basi Serikali imetakiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la
Bajeti.
“Bunge
linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya
kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa
fedha za shirika hilo,” aliongeza Zitto katika maazimio hayo
yaliyoridhiwa na Bunge zima baada ya kuandaliwa na watu 21.
*Pinda
Akiahirisha
mkutano huo wa 16 na 17 wa Bunge, Waziri Mkuu Pinda alisema CAG
atapewa kazi mahsusi ya kufanyika kazi kujua kama fedha za Tegeta Escrow
zilikuwa za umma, kwa maana alisema sehemu inaweza kuwa za Tanesco,
IPTL au Serikali.
Source:Habarileo
No comments:
Post a Comment