Pages

KAPIPI TV

Saturday, September 27, 2014

WANAFUNZI WA KIKE WASHINDWA KUFANYA MTIHANI BAADA YA KUKUMBWA NA UGONJWA WA AJABU-KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma

Wanafuzi 16 wa kike katika shule ya sekondari ya Mugombe  wilaya ya Kibondo Mkoani hapa,wameshindwa kufanya mtihani wa majaribio wa kidato cha Nne baada ya kupatwa na hali ya kuchanganyikiwa akili ghafla katika mazingira ya kutatanisha.

Wakizungumzia hilo kwa nyakati tofauti mbele ya waandishi wa habari shuleni hapo, Tilifania Jonathan na Suzana Charles walisema Septemba 23,2014  majira ya mchana baada ya kumaliza mtihani wa tano walihisi maumivu  makali ya kichwa pamoja na kukosa nguvu mwilini kwa ghafla na kujikuta wanaanza kukimbiakimbia hovyo.

Akielezea hilo Mkuu wa shule hiyo Tanu Selemani alikiri  kuwepo kwa tukio hilo  kwa wanafunzi wa kike tu,ambapo rasmi walianza wanafunzi wawili  mnamo  17,septemba mwaka huu na hali kuwa mbaya zaidi tarehe 26,septemba na kusabaisha baadhi yao  kurudishwa nyumbani kwao hatua iliyofanya pia  kukosa kufanya  baadhi ya mitihani.
 
“Tulidhani ni mzaha lakini muda ulivyozidi hali ilikuwa mbaya zaidi ,tuliwafunga kamba za  mikono na miguu ili kudhibiti kukimbia holela na wengine kumi hawajarudi shuleni hadi leo  wapo majumbani kwao na wazazi hawajarudisha mrejesho juu ya afya zao aah ni tukio la kwanza” alisema Seleman.
 
Hata hivyo   wanafunzi wapatao kumi  kati yao bado wapo majumbani na watano walifanyiwa maombi na mchungaji wa kanisa moja la kilokole la wilayani humo Mwamko Lutego ambapo alidai walikutwa na nguvu za pepo na kufanikiwa kuyafukuza kwa mujibu wa imani ya dini yao huku ikithibitika kuwa hali zao zimeanza kuimarika.

Diwani wa kata ya Kumsenga Simoni Kanguye ambaye alifuatana na  timu ya wauguzi na mganga wa wilaya  pamoja na mchungaji huyo  katika kufuatilia hali na kutathimini uhalisia wa chanzo cha maradhi hayo ya aina yake,alisema  hali hiyo imewashangaza sana kwakuwa baada ya kuwapima wanafunzi hao walikuwa hawana ugonjwa wa aina hiyo.

Aidha shule hiyo ni ya mchanganyiko pia ina mabweni ya wanafunzi wa jinsia zote,lakini adha hiyo huwakumba wanafunzi wa kike pekee.

No comments: