Anna Nkinda – Maelezo
11/9/2014 Serikali imeombwa
kuangalia uwezekano wa kutoa huduma ya matibabu ya ugonjwa wa saratani
za wanawake kwenye Hospitali zingine nchini kwani hivi sasa huduma hiyo
inatolewa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pekee.
Ombi hilo limetolewa leo na
wanawake wanaokabiliwa na tatizo la ugonjwa wa saratani ya mlango
wa kizazi na matiti wakati wakiongea na waandishi wa habari
waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa saratani za wanawake unaofanyika
katika Hoteli ya Court Yard jijini Dar es Salaam.
Wanawake hao walisema inachukua
muda mrefu pale ambapo utagundulika una ugonjwa wa saratani hadi kupata
matibabu lakini kama huduma hiyo itatolewa katika Hospitali zingine
itarahisisha kwa mgonjwa kupata matibabu kwa wakati.
Mmoja wa wanawake anasumbuliwa na
saratani ya titi alisema wanawake wengi wanafikiria ukiugua saratani
unakwenda kufa jambo ambalo siyo kweli kwani yeye ameishi na ugonjwa huo
kwa muda wa miaka 16 sasa.
“Nawashauri wanawake wenzangu
waende kufanya vipimo vya mara kwa mara kwani kuna vipimo ambavyo
ukipima utajua kama unatatizo au la na kama utakutwa na
ugonjwa utapata dawa mapema”, alisema mgonjwa huyo.
Naye mmoja wa wanawake anayeumwa
ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi alisema dalili ya kwanza
aliyoiona ni kutokwa na damu ukeni akaamua kwenda kufanya vipimo na
baada ya kukutwa na tatizo akapata matibabu katika Taasisi ya Saratani
ya Ocean Road.
“Nawashauri wanawake wenzangu
wakiona dalili za ugonjwa huu wasikae kimya na kujidanganya kwa kutumia
dawa za miti shamba bali wawahi Hospitali mapema ambako watapata
matibabu na kupona. Mimi nilipata tatizo la ugonjwa huo mwaka 2011
nilitibiwa na kupona”, alisema.
Kwa upande wake Dkt. Sara Maongezi
ambaye ni Mkurugenzi wa uboreshaji Afya kutoka Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema Saratani ya mlango wa kizazi ni moja ya
saratani inayoongoza kwa kuua wanawake wengi nchini.
Alisema mkutano huo ambao
umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi,
Zambia, Madagasca, Rwanda na Burundi unalengo la kuwafanya wanawake
waweze kuufahamu ugonjwa huo ili waweze kujikinga kwa wale ambao
hawajapata na kwa walioupata waweze kuwahi mapema Hospitali kwa ajili ya
kupata huduma za matibabu.
“Baada ya Mkutano huu tutatoka
na maazimio ambayo tutayafanyia kazi na kuona jinsi gani tunaweza
kuboresha utendaji wetu wa kazi za kuielimisha jamii kuhusu ugonjwa
huu”, alisema Dkt. Maongezi.
Dkt. Maongezi alisema, katika
nchi za Afrika ya Mashariki takwimu zinaonyesha Tanzania inaongoza kuwa
na wagonjwa wengi wa saratani za wanawake lakini bado hakuna ukusanyaji
sahihi wa takwimu kwani wagonjwa wengi wanafia majumbani na wanaofika
Hospitali kupata matibabu ni wachache.
Walengwa wa mkutano huo ni
wanawake wanaoishi na saratani pamoja na Asasi zinazofanya kazi za
saratani lengo lake ni kwa wadau hao kuweza kuilemisha jamii ili iweze
kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo.
Mkutano huo umeandaliwa na
Women’s Empowerment Cancers Advocacy Network, (WE CAN) kwa kushirikiana
na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii pamoja na wadau wengine wa Saratani .
No comments:
Post a Comment