Meneja wa Mkoa wa Lindi, Fortunata Raymond akielezea namna Mfuko wa Afya ya Jamii unavyofanya kazi Mkoani humo.
Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi akisisitiza jambo
baada ya kupata maelezo ya huduma za Mfuko huo ikiwa pamoja na
kuupongeza kwa kazi nzuri.
Ofisa
Mdhibiti Ubora wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Timothy Mwasajone
akitoa ushauri wa namna ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Na Mwandishi Wetu, Lindi
SERIKALI imeutaka Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya kuendesha huduma za elimu ya kuepukana na magonjwa
yasiyoambukiza katika mikoa yote hususani vijijini pamoja na upimaji wa
afya bure ili wananchi watambue afya zao na hatimaye kuongeza
uzalishaji katika sekta za kilimo na uvuvi na biashara kwa ujumla.
Agizo hilo lilitolewa na Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Godfrey Zambi wakati wa maonesho
ya Nane Nane Kitaifa yanayoendelea mkoani Lindi ambapo Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya umeshiriki na unatoa huduma mbalimbali zikiwemo za elimu
kwa Umma, usajili wa wanachama, upimaji afya bure ikiwemo saratani ya
matiti.
Aidha alisisitiza kuwa mbali na
huduma hizo nzuri zinazotolewa na Mfuko, ni vyema wananchi pia wakapata
elimu juu ya umuhimu wa kujiunga na Mifuko ya Afya ya Jamii ili
wanapougua wapate matibabu bila ya usumbufu wowote.
“NHIF mnafanya kazi nzuri sana
nawapongeza, na hata huduma mliyoileta huku Lindi katika kipindi hiki
cha siku nane naamini wananchi wa maeneo haya watanufaika na huduma hizi
hususan ya upimaji wa afya bure, hivyo ninachowaomba sasa ongezeni kasi
hasa kwa kwenda vijijini ambako ndiko kuna kundi kubwa la wananchi,”
“Wakati mkifanya hizi huduma pia
wahamasisheni wananchi kujiunga na Mifuko hii ya Afya ya Jamii ili
wanapougua wapate huduma hata kama hawana fedha mfukoni,” alisema Naibu
Waziri.
Aidha alitoa mwito kwa wananchi
wa Mkoa wa Lindi, Mtwara na wananchi wanaoishi jirani na mikoa hiyo
kuhakikisha wanaitumia vyema fursa hii wakati wa maonesho haya kufika
katika banda la NHIF ili kupata huduma ambazo zinatolewa bila malipo kwa
wananchi lakini zimeghramiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Naye Mkurugenzi wa Masoko na
Utafiti Raphael Mwamoto, alisema kuwa NHIF kwa sasa inaendesha huduma
hizi katika mikoa yote kwa lengo la kuwafanya wananchi kutambua umuhimu
wa kujua afya zao lakini pia umuhimu wa kupata huduma za matibabu
kupitia Mifuko ya Afya ya Jamii.
Alisema kuwa kwa upande wa elimu
juu ya faida za kujiunga na Mifuko ya Jamii, NHIF inao mpango wa elimu
ya Kata kwa Kata ambayo inafanyika zaidi katika maeneo ya vijijini ili
kuwahamasisha wananchi kujiunga na kunufaika na Mifuko hii.
“Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
kwa sasa una ofisi zake kila Mkoa Tanzania ikiwemo Ofisi ya Zanzibar,
hivyo shughuli za elimu kwa umma na upimaji wa afya za wananchi
hufanywa mara kwa mara na maofisa wa Mfuko walioko katika Ofisi zetu za
mikoani” alisema.
Pia Ndugu Mwamoto aliendelea
kusema kwamba matumizi sahihi ya fedha za tele kwa tele za CHF pamoja na
fedha za matibabu zinazolipwa na NHIF katika vituo vinavyotoa huduma
kwa wanufaika wa CHF na NHIF ni jambo muhimu sana. Alisema……..….’’ Fedha
zinazolipwa na Mfuko pamoja na CHF ni fedha nyingi ambazo zikitumika
vizuri zinaweza kuboresha huduma za afya hasa upatikanaji wa dawa maeneo
ya vijijini, kuna Halmashauri ambazo zimefanikiwa sana katika hili kwa
mfano Nachingwea, Iramba, Igunga. Zingine ni Halamsahauri za
Songea,Tanga ,Rombo,Singida na Mwanga. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
unaziomba Halmashaouri zingine nchini kote ziige mfano huu’’,
No comments:
Post a Comment