Balozi wa Sudan Tanzania, Dk. Yassir Mohammed Ali |
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne
Maghembe jana alikutana na Balozi wa Sudan Nchini, Dk. Yassir Mohammed
Ali, ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo mafupi, hususani matumizi ya
maji ya Mto Nile.
Waziri Maghembe alisema Tanzania haina mpango wa kuharibu maji
ya Mto Nile kama wengi wanavyofikiri, zaidi ya kutaka kuhakikisha hatua
sahihi zinachukuliwa ili kutatua tatizo la kupungua kwa kina cha maji
kutokana na matumizi ya kibinadamu kukithiri na hivyo kuhatarisha uwepo
wa mto huo.
“Tanzania inachangia asilimia 28 ya maji ya Mto Nile na inatumia
kiasi kidogo sana cha maji hayo kwa matumizi yake kwa asilimia 0.072
tu, huku ujazo wa mto huo ukiwa ni mita za ujazo bil 89, kuna haja ya
kupata uwiano mzuri wa matumizi ya maji hayo tofauti na ilivyo sasa.”,
alisema Prof. Maghembe.
Prof. Maghembe alisisitiza msimamo wa Tanzania ni kuhakikisha
matumizi mazuri na sahihi, utunzaji na ulinzi wa maji ya Mto Nile ili
kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa watu wote sasa na baadae.
Huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, na kuahidi Tanzania
itaendelea kutoa ushirikiano kwa Jumuiya hiyo na Afrika Mashariki na
Kati ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na mto huo.
Balozi, Dk. Yassir alisema amefurahishwa na mtazamo wa Tanzania
kwa kuhakikisha utunzwaji na matumizi mazuri ya maji ya Mto Nile na
kuipongeza kwa kutoa ushirikiano chanya katika kuleta maendeleo ya Sekta
ya Maji Afrika Mashariki na Kati.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa tamko la
Tanzania kuendelea na mazungumzo ya Mkataba wa Maji ya Mto Nile na
kusema Tanzania haijapanga kujitoa katika mchakato huo, bali unategemea
kupelekwa Bungeni mwezi Novemba kwa ajili ya kuujadili kabla ya
kuupitisha.
Waziri Maghembe leo yupo Sudan, jijini Khartoum katika Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri wa Maji (Nile-COM) unaofanyika leo
No comments:
Post a Comment