Pages

KAPIPI TV

Thursday, June 19, 2014

WAFUGAJI KIBONDO WALALAMIKIA KUPIGWA NA ASKARI WA HIFADHI MUYOWOSI

Na Magreth   Magosso, Kigoma   


Meneja wa Hifadhi ya Kigosi Game Reserves  eneo la Muyowozi wilayani Kibondo Mkoani Hapa Mathias  Ngasila amekana kuwatuma askari wa hifadhi hiyo,kwenda kuwapiga virungu na kuwatoza fedha bila kuwapatia risiti  wafugaji wenye asili ya Kitusi  wanaofanya shughuli hizo pembezoni mwa  hifadhi hiyo.


Kauli hiyo imedhihirika kwenye mkutano  maalum wa viongozi wa  Chama cha Mapinduzi   mkoani hapa kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya hiyo Venance Mwamoto katika ofisi za utawala wa hifadhi hiyo kwa lengo la kuweka uwazi wa mipaka yao kwa umma ili kuboresha  mahusiano kati ya wanakijiji na mwekezaji katika hifadhi hiyo.

Akizungumzia changamoto hiyo Mwenyekiti wa ccm Mkoa Kigoma Dr.Warid Kabourou  na  Katibu mwenezi   Bw.Kalembe Masoud  kwa nyakati tofauti walisema wafugaji hao wamepeleka kilio chao katika ofisi za ccm mkoa, baada ya jitihada za madiwani,wenyeviti wa vijiji sanjari na mbunge wao kushindwa kutatua mgogoro huo kuanzia mwaka 2003-2014.

Walisema  kitendo cha askari wa hifadhi hiyo kutumia madaraka  yao kuwapiga na kupora fedha  ni kinyume na taratibu  za  utawala bora  na pia ni  ukiukwaji wa haki za binadamu mbali  na kuihujumu serikali   ikiwa  ni  pamoja  na wananchi kuhisi kwamba  wanabaguliwa  kutokana na asili yao,huku wakishauri hifadhi hiyo iwashirikishe wananchi  katika kuweka mipaka yao .

 Kwa upande wa wahanga wa tukio hilo Jonathan Joel na Mwimila Madirisha kwa nyakati tofauti walisema awali  katika  historia fupi wananchi  waliishi kijiji cha Ilunde  kwa  zaidi ya karne tatu ndipo 1981 walitangaziwa ujio wa mwekezaji,lakini mwaka 1985 serikali ilijenga shule  na huduma zingine za kijamii ikiwemo zahanati ikiashiria kuwa si hifadhi bali ni eneo rasmi la makazi ya watu.

Walisema mwaka 2003 waliondolewa na serikali bila kupewa  eneo jingine la kufanyia shughuli zao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao kutokana na kutangatanga kutafuta maeneo mengine na hatimaye waliambiwa wapeleke mifugo kwenye lanchi ya mifugo ya  wilaya ya Uvinza ambayo haina sifa ya kuboresha mifugo kutokana na kutokuwa na malisho ya kutosha na magonjwa mbalimbali ambayo ni tishio kwa uhai wa mifugo yao.

“ mifugo  ya serikali ya uvinza  ilikufa kwa ndorobo na nyoka wakubwa waliokuwa wakidhuru mifugo ,alafu wanasema tuweke mifugo huko tutaishije bila mifugo sasa tupo kando ya Ziwa la nyamagoma lakini  bado tunafilisiwa na watu wa hifadhi, walibainisha  wahanga hao.

Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Kibondo Venance Mwamoto alibainisha kuwa ,kigoma haina dhiki ya maeneo kiasi cha kuwafanya wafugaji  kuangaika na kukiri kuwa  changamoto ipo kwenye mgawanyo wa ardhi hiyo ambapo zinachangiwa na sheria ya ardhi na sera zilizopitwa na wakati.

Akijibu tuhuma hizo Meneja wa hifadhi hiyo Mathias Ngasila alikanusha  Askari wake  kutofanya ukatili huo na kukubali kufanya hivyo endapo wafugaji watakutwa na hatia ya kuingiza mifugo katika eneo lake na  kutoa  mawasiliano kwa viongozi wa wahanga hao namna ya kutoa taarifa kwake ili kudhibiti hilo.

Mtandao huu umebaini kuwa hifadhi hiyo ilianza kufanya shughuli zake mnamo mwaka 2004 hadi  2014  bila kuweka alama  za  kuelekeza umma ukomo wa eneo lake ambapo ingesaidia wafugaji wasipatwe na vipigo  na mwenyekiti wa ccm kuandaa barua ya kuwataka waziri  wa ardhi na maliasili wafike hapo ili kuondoa utata huo.

No comments: