Na Magreth Magosso, Babati
IMEELEZWA kuwa moja kati ya changamoto zinazokwamisha malengo ya kuongeza utalii wa ndani inatokana na gharama kubwa za usafiri wa kuwafikisha watalii maeneo mbalimbali ya hifadhi za Taifa ikilinganishwa na hali halisi ya vipato vyao na hivyo kushindwa kumudu gharama za utalii wa ndani kwa baadhi ya wananchi waliowengi.
Kauli hiyo imetolewa na Mhifadhi utalii wa hifadhi ya
Tarangire David Maige ambaye aliwaeleza Waandishi wa habari kutoka mkoani Kigoma waliotembelea hifadhi hiyo ambapo aliweka bayana kuwa hali duni inayosababishwa na kipato kidogo kwa wananchi
wanaoishi maeneo jirani hifadhi hiyo imekuwa kikwazo kikubwa cha kushindwa kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo ndani ya hifadhi.
Alisema ili kufikia lengo la kuongeza utalii wa ndani Serikali inapaswa kuangalia namna ya kutatua tatizo la
usafiri kwa kupunguza kiwango cha kodi ya ushuru kwa magari binafsi ili yaweze
kutoa huduma nafuu kwa wananchi walio tayari kutembelea hifadhi, licha ya Shirika la hifadhi ya Taifa kutatua changamoto ya maeneo ya
malazi ya wageni kulingana na kipato cha wananchi.
“Gharama zipo juu , kwa siku mtalii anatakiwa kutoa kiasi cha
shilingi laki tatu, na utalii wa hifadhi ya Tarangire sehemu kubwa ni hutumia gari
kutokana na wanyama wakali waliopo ndani ya hifadhi ni vyema wananchi waje kwa vikundi ili kumudu gharama za
usafiri” alisema Maige
Naye Kaimu mhifadhi
mkuu wa hifadhi hiyo Upendo Massawe
alisema takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2010/2011 waliotembelea hifadhi
walikuwa 43,181 huku mwaka 2012/2013
watalii 65,038 walitembelea hifadhi ambapo idadi hiyo ni chache
ukilinganisha na wakazi wanaoishi katika mkoa wa Arusha na mikoa jilani.
Aidha imebainika kuwa, hifadhi nyingi nchini zinakabiliwa na
changamoto ya janga la ujangili, uvamizi
wa mapito ya wanyama, ongezeko la idadi ya watu katika vijiji vinavyozunguuka
hifadhi na kusababisha kusongeza ndani mipaka ya hifadhi, uharibifu wa vyanzo vya
maji na mazingira kwa ujumla.
Kutokana na changamoto hizo jamii inatakiwa kukubali kutumia
elimu inayotolewa na shirika hilo kwa kuleta mabadiliko chanya ya kutunza na
kuhifadhi mazingira na wanyama kwa kushirikiana na shirika hilo kwa kuwadhibiti wale
wanaohusika kukiuka taratibu, kanuni na sheria, sambamba na Serikali kuangalia
upya ongezeko la watu katika maeneo ya hifadhi.
No comments:
Post a Comment