Serikali
ya Ujerumani, pamoja na ahadi ya Euro milioni moja ya kusaidia Uhifadhi
wa Pori la Akiba Selous, imehimiza mataifa mengine kusaidia Uhifadhi wa
Pori hilo kutokana na ujangili wa tembo uliokithiri.
Pori la Akiba Selous, lenye ukubwa
wa kilometa za mraba 50,000, ni mojawapo kati ya maeneo saba yaliyo
kwenye orodha ya Urithi wa Dunia nchini Tanzania. Maeneo mengine ni
Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Eneo la
Hifadhi ya Ngorongoro, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo
Mnara, Michoro ya Miambani Kondoa, na Mji Mkongwe Zanzibar. Malengo
makuu na faida ya kuweka eneo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia ni pamoja
na:
• Kuwa na nguvu ya pamoja kimataifa ya kusimamia uhifadhi wa eneo;
• Kujulikana kimataifa kama kivutio chenye sifa maalum cha utalii;
• Kutumika kwa tafiti mbali mbali za uhifadhi pamoja; na
• Kuvutia misaada ya kimataifa ya kiuhifadhi.
Kamati ya Urithi wa Dunia
imeainisha vigezo 10 vinavyowezesha eneo kuorodheshwa kwenye Orodha ya
Urithi wa Dunia.Pori la Akiba Selous liliorodheshwa mwaka 1982 kwa
kukidhi vigezo viwili kati ya hivyo, ambavyo ni:
• Eneo muhimu sana kwa bioanuai ikiwemo idadi kubwa ya tembo kuliko pori lolote duniani; na
• Eneo lenye aina na muingiliano mpana wa uoto wa asili
ikiwemo mimea zaidi ya aina 2100 na misitu mikubwa aina ya miombo
kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.
Katika Mkutano wa 38 wa Kamati ya
Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Doha-Qatar (15-26 Juni 2014), Pori
la Akiba Selous ni mojawapo ya maeneo yaliyoingizwa kwenye orodha ya
maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini.
Lengo la kuingiza eneo kwenye
orodha ya maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini ni kuongeza uelewa wa
jamii kitaifa na kimataifa kuhusu matatizo yanayolikabili eneo hilo ili
kuwezesha upatikanaji wa misaada ya hali na mali ilikulirejesha katika
hadhi yake ya asili.
Tangu Pori la Akiba Selous liwekwa
kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia, hali yake kwa ujumla
iliendelea kuwa nzuri na ya kuridhisha. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2010
Pori hili pamoja na maeneo mengine nchini yamekumbwa na wimbi kubwa la
ujangili, hususani wa tembo. Hali hii imesababisha kupungua kwa idadi ya
tembo katika mfumo ikolojia wa Selous, kutoka tembo 70,000 mwaka 2006
hadi kufikia tembo 13,084 mwaka 2013.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya
Tanzania ilichukua hatua za haraka kudhibiti hali hii katika Pori la
Akiba Selous kwa :
• Kuliongezea uwezo wa rasilimali fedha kwa kurejesha utaratibu wa awali wa kubakiza asilimia 50 ya mapato;
• Kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kuhifadhi tembo na
kuunda vikosi maalum vya pamoja miongoni mwa taasisi za wanyamapori vya
kupambana na ujangili katika kanda 11 nchini. Mojawapo ya kanda hizo ni
kwa ajili ya mfumo wa ikolojia ya Selous;
• Kuboresha shughuli za uhifadhi rasilimali ya wanyamapori
kwa kubadili mfumo wa usimamizi wa uhifadhi wa wanyamapori kwa kuanzisha
Mamlaka ya Wanyamapori itakayowezesha Pori la Akiba la Selous kupata
fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za uhifadhi;
• Kuongeza idadi ya wahifadhi wanyamapori 105 ambao 40 kati
yao walipangiwa eneo la kazi la Pori la Akiba Selous. Aidha, usaili wa
kuajiri wahifadhi wengine 437 umefanyika na kati yao 200 watapangiwa
kazi katika Pori la Akiba la Selous; na
• Kuongeza idadi ya vitendea kazi yakiwemo magari mapya 8,
helikopta moja, ukarabati wa mitambo na magari, kuboresha huduma za
jamii kwa watumishi pamoja na kukarabati miundo mbinu ya barabara,
nyumba za watumishi na viwanja vya ndege.
Kutokana na hali ya ujangili
mkubwa uliosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo,Kamati ya
Urithi wa Dunia ilituma timu ya wataalam mwezi Desemba 2013 kwa ajili ya
kufanya tathmini ya ukubwa wa tatizo na kupendekeza hatua stahili za
kuchukua kunusuru hali hii.
Baada ya kutembelea Pori la Akiba Selous na
kupata maoni ya Serikali na wadau mbalimbali wa uhifadhi, Kamati ya
Urithi wa Dunia ilipendekeza Pori la Akiba Selous liwekwe kwenye orodha
ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini kama ilivyokuwa kwa eneo la
Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara mwaka 2004. Pendekezo
hili limeridhiwa na Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia
unaoendelea Doha katika Falme ya Qatar.
Katika mkutano huu,eneo la Magofu
ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara limeondolewa kutoka orodha ya
maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini baada ya juhudi kubwa za
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na jamii ya kimataifa kuchukua
hatua stahili kurekebisha upungufu uliosababisha eneo hili kuwekwa
kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini. Pori la
Akiba Selous kuwekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo
hatarini ni fursa ya kuweza kupata misaada kutoka jamii ya kimataifa kwa
ajili ya kukabili tatizo la ujangili wa tembo.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Kamati
ya Urithi wa Dunia imetoa muda wa mwaka mmoja kwa Serikali ya Tanzania
kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kukomesha ujangili wa tembo
katika Pori la Akiba la Selous na hatimaye kuliondoa kwenye orodha ya
maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini.Kutokana na uamuzi huu,
Serikali ya Ujerumani imeahidi kutoa euro milioni moja na kuhimiza
mataifa mengine yatoe misaada ya kifedha na kiufundi kwa Tanzania ili
iweze kukabili tatizo hili sugu haraka iwezekanavyo.
Vile vile mataifa
mengine ikiwemo Ureno, Algeria, Senegali, Lebanon na Colombia yameungana
na Ujerumani kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kuisaidia Tanzania
kutimiza azma yake.
IMETOLEWA NA MSEMAJI WA WIZARA
23.06.2014
No comments:
Post a Comment