Pages

KAPIPI TV

Friday, June 20, 2014

MWANAFUNZI DARASA LA NNE AKATWA MAPANGA NA MFANYAKAZI WA NYUMBANI-URAMBO


Na Allan Ntana, Urambo

MTOTO Perezi Christian (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne
katika shule ya msingi Motomoto iliyoko katika kata ya Vumilia wilaya
ya Urambo mkoani Tabora amekatwakatwa  mapanga mikononi na miguuni na
mfanyakazi wa nyumbani.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa akiwa wodini alikolazwa Perezi mama
mzazi wa mtoto huyo Regina Fumbo (45) ambaye ni muuguzi katika kituo
cha afya Zogolo kilichoko katika tarafa ya Nyasa wilayani Nzega
alisema mtoto wake amekatwakatwa mapanga na mfanyakazi wa shambani
anayeitwa Abdallah Alfan muha mwenye umri wa kati ya miaka 39-44.

Alisema awali hapakuwa na ugomvi wowote kabisa kila alichotaka alikuwa
anapewa, alichukua uamuzi huo kwa hasira tu kwani tayari alikuwa
ameahidiwa kulipwa hela alizokuwa ameomba kwa bosi wake ambaye ni baba
mzazi wa mtoto huyo Bw. Christian Mlela.

‘Hili tukio limenisikitisha sana, nilipigiwa simu nikiwa kazini kwangu
kule Nzega, nikajua mtoto wangu sitamkuta hai tena, nilikuja mbio
mpaka wodi ya wanaume alipolazawa, kwa kweli hali yake haikuwa nzuri,
namshukuru Mungu sasa hivi anaendelea vizuri, na huyo mtuhumiwa
ameshakamatwa na polisi’, alisema.

Mtoto Perezi alipohojiwa na mwandishi wa  KAPIPIJhabari.COM akiwa wodini
katika hospitali ya wilaya Urambo alisema kabla ya kukatwa mapanga
babake hakuwepo, mtuhumiwa huyo alipokuja alidai baba hataki kumpa
hela yake yeye anajali kazi zake tu, sasa ngojea, ndipo akaanza
kumkata kata.

‘Ninaumia sana, sijui kama nitapona ili niendelee na shule kama
nilivyokuwa, jamani naomba madaktari wanisaidie nipone haraka kabla
shule hazijafunguliwa mwezi ujao’, alisema mtoto Perezi  kwa
masikitiko makubwa mbele ya mwandishi.

Baba mzazi wa Perezi ambaye ni Katibu Meneja wa Chama cha Msingi
Kasela katika kijiji cha Motomoto alipohojiwa na mwandishi wa gazeti
hili alidai walikuwa wamekubaliana amlipe sh 200,000 watakapouza
tumbaku msimu huu na tayari walikuwa wameshaikausha hivyo wakawa
wanasubiri kupima uzito wake na kujua gredi ili wakauze.

‘Huyu bwana alianza kunidai hela hata kabla ya kuuza tumbaku kama
tulivyokubaliana, nikamwomba avumilie kidogo ili nimtafutie kwani yeye
alidai anataka kurudi kwao Kigoma, lakini awali nilimpa hela kidogo za
kujikimu kiasi cha sh 20,000’, aliongeza.

Aidha aliongeza kuwa tayari wameshatoa taarifa kituo cha polisi Urambo
na mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya hatua
zingine za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

No comments: