Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuujulisha umma matokeo
ya sensa ya tembo iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu ili
kuiwezesha Serikali kutambua hali ya rasilimali ya wanyamapori ndani na
nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Wizara kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi
imefanya sensa katika Maeneo ya Mfumo ikolojia wa Selous – Mikumi na
Ruaha – Rungwa pekee kwa kuwa ni maeneo yenye tembo wengi nchini.
Matokeo ya sensa hii yanaonyesha
kwamba Mfumo wa ikolojia wa Selous-Mikumi kwa sasa una tembo wapatao
13,084 na Ruaha–Rungwa una tembo wapatao 20,090. Takwimu hizi zinaonesha
kupungua kwa idadi ya tembo na hasa katika mfumo ikolojia wa
Selous-Mikumi ikilinganishwa na Sensa za awali.
Takwimu za muda mrefu zinaonesha
kwamba mwaka 1976 katika mfumo ikolojia wa Selous–Mikumi kulikuwa na
tembo 109,419. Idadi hii ilipungua kufikia 22,208 mwaka 1991 kutokana na
wimbi la ujangili uliokuwepo katika kipindi cha mwaka 1984 -1989.
Hata
hivyo, idadi hiyo iliongezeka na kufikia 70,406 mwaka 2006 baada ya
Operesheni Uhai iliyofanyika mwaka 1989 na 1990 na juhudi za kimataifa
za uhifadhi ikiwemo kusitisha biashara ya meno ya tembo
Aidha, idadi ya tembo nchini
ilipungua hadi kufikia jumla ya tembo 38,975 mwaka 2009 na kuendelea
kupungua hadi kufikia tembo 13,084 hivi sasa.
Hali kama hiyo inaonekana pia
katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha-Rungwa ambapo sensa ya mwaka 1990
ilionesha kuwa na tembo 11,712 kutokana na wimbi la ujangili. Idadi hii
iliongezeka na kufikia 35,461 mwaka 2006. Hata hivyo, idadi hiyo
imepungua na kubakia tembo 20,090 hivi sasa.
Kwa matokeo haya inaonesha kuwa
katika mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi idadi ya tembo imepungua kwa
asilimia 66 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na
jumla ya tembo 38,975. na katika Mfumo ikolojia wa Ruaha–Rungwa Tembo
wamepungua kwa asilimia 36.5 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009
ambapo kulikuwa na jumla ya tembo wapatao 31,625.
Kupungua huku kunathibitishwa na
idadi ya mizoga ya tembo iliyohesabiwa wakati wa zoezi la sensa. Jumla
ya mizoga 6,516 na 3,496 ilihesabiwa katika mifumo ikolojia ya
Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa. Katika zoezi hili Wizara ilitumia vigezo
vya uwiano wa mizoga na tembo hai waliohesabiwa (carcass ratio) kubaini
vyanzo vya vifo hivyo. Katika hali ya kawaida, uwiano wa asilimia 7 – 8
unaashiria vifo vya asili kama vile ugonjwa na uzee. Zaidi ya asilimia
hiyo inaashiria vifo visivyo vya asili.
Sensa iliyofanyika mwaka huu imeonesha uwiano wa asilimia 30 kwa
mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi na asilimia 14.6 kwa Ruaha–Rungwa. Kwa
mujibu wa matokeo hayo, idadi kubwa ya vifo vya tembo vimetokana na vifo
visivyo vya asili.
Uchambuzi wa kina umebainisha kuwa
asilimia 95 na 85 ya mizoga iliyoonekana katika mifumo ikolojia ya
Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa ni ya zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Hii inaonesha kuwa juhudi za
makusudi zilizofanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria na
operesheni maalum mbalimbali za hivi karibuni zimesaidia kupunguza
wimbi la ujangili kwa kiasi kikubwa.
Aidha, kukamatwa kwa meno ya tembo
yenye uzito wa kilogramu 32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi cha
2008 hadi Septemba 2013 ni ishara tosha kuwa ujangili ni mojawapo ya
sababu kubwa za kupungua kwa idadi ya tembo nchini.
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa
mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na shoroba za wanyamapori.
Mathalan, katika Pori Tengefu la Kilombero ambalo ni sehemu ya ikolojia
ya Selous – Mikumi, mwaka 2002 lilikuwa na tembo 2,080, katika sensa ya
mwaka huu, hukukuwa na tembo hata mmoja.
Ongezeko la bei katika masoko ya
biashara haramu ya meno ya tembo hususan katika nchi za Mashariki ya
mbali ni kichocheo na kisababishi kikubwa.
Kufuatia hali hii, Wizara
inaimarisha ulinzi wa wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi
na usalama na taasisi nyingine za kanda na kimataifa pamoja na
kuelimisha na kushirikisha wananchi katika masuala mbalimbali ya
uhifadhi.
Ili kuimarisha na kuboresha
shughuli za uhifadhi, Wizara iko katika hatua za mwisho za kuanzisha
mamlaka mpya ya wanyamapori. Vilevile sheria za uhifadhi zinapitiwa ili
kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa kijeshi kwa watumishi wa sekta ya
wanyamapori.
Wizara inapenda kuwatambua na
kuwashukuru wafadhili wote waliofanikisha sensa hii iliyogharimu kiasi
cha dola za kimarekani 160,000 ikiwa ni fedha za serikali na wafadhili.
Wafadhili hao ni Shirika la Misaada ya Kiufundi la Ujerumani (GIZ)
kupitia Frankfurt Zoological Society (FZS) na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia Mradi wa TANAPA wa SPANEST.
Imetolewa na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu (MB)
10/01/2014
|
No comments:
Post a Comment