Pages

KAPIPI TV

Tuesday, August 13, 2013

TAMASHA LA NANE LA VYOMBO VYA HABARI ARUSHA KUFANYIKA SEPTEMBA 8.

  Mwandishi wetu, Arusha
 TAMASHA la nane la vyombo vya habari mkoa wa Arusha, linatarajiwa kufanyika Septemba 8 katika viwanja vya General tyre Arusha na kushirikisha waandishi kutoka jijini Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro na mkoa wa Manyara.
Tamasha hili, ambalo hufanyika kila mwaka, limedhaminiwa na kampuni ya bia nchini(TBL).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chama cha Waandishi wa habari za michezo mkoa wa Arusha(TASWA) Mussa Juma, alisema  zaidi ya waandishi wa habari na wadau wa habari 500 wanatarajiwa kushiriki katika Tamasha hilo.
Juma alisema kwa upande wa michezo timu ambazo zitashiriki ni TASWA FC kutoka jijini Dar es Salaam, TASWA Arusha, Radio Sunrise, Radio 5, Radio Triple A, Arusha One Radio na Chuo cha Uandishi wa habari Arusha ambao ndio mabingwa watetezi.
Alisema pia kutakuwa na timu ambazo zimealikwa ambazo ni timu ya TBL Arusha ambao ndio wadhamini wakuu wa Tamasha hilo, timu ya Wazee Klabu,Kitambi Noma, Timu ya Pepsi na timu ya NSSF Arusha.
Juma alisema katika tamasha hilo, ambalo huandaliwa na TASWA na kampuni ya Ms Unique, kutakuwa na michezo ya soka, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mpira wa mikono na mbio za magunia.
Alisema Septemba 7 bonanza hilo, litatanguliwa na semina ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoa wa Arusha kuhusiana na sheria za michezo, masuala ya afya na jinsi ya kutumia michezo katika kutangaza utalii.
Hata hivyo, Juma alisema bado wadhamini wanaombwa kujitokeza kudhamini tamasha hilo.

No comments: