Jeshi la polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora jana liliwafikisha mahakamani tena makada watano wa Chadema wanaokabiliwa na kesi ya kummwagia tindikali kada wa Ccm Mussa Tesha na kusomewa shitaka upya.
 
Washtakiwa hao waliwasili jana saa 12:45 wakitokea Tabora na kufikishwa mahakamani majira ya saa 1:15 usiku huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi ambapo wafuasi wa Chadema wakiwa wamefurika mahakamani.
 
Akiwasomea shitaka mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Igunga Bw.Ajali Milanzi,mwendesha mashtaka mrakibu msaidizi wa polisi Cosmas Mboya aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao wanashtakiwa kwa kosa la kumwagia tindikali Bw.Mussa Tesha mkazi wa Igunga mjini na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake.
 
Aliongeza kuwa washtakiwa hao walitenda kosa kinyume na kifungu namba 225 sura ya 16 kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,ambapo  aliimbia mahakama kuwa washtakiwa Evodius Justian mkazi wa Bukoba,Osca Kaijage mkazi wa Shinyanga,Seif Kabuta mkazi wa Nyasaka Mwanza,Rajabu Kihawa mkazi wa Dodoma na Henly Kilewo mkazi wa Dar es salamu wanakabiliwa na shitaka la kumshambulia na kumwagia tindikali Bw.Mussa  Tesha  wakati wa kampeni  za  uchaguzi mdogo jimbo la Igunga mwaka 2011.
 
Mwendesha  mashtaka huyo  Bw. Mboya aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao mnamo septemba tisa mwaka 2011 majira ya usiku maeneo ya msitu wa Hanihani wilayani Igunga walimmwagia tindikali Tesha  mwilini mwake maeneo ya mdomo ,pua,uso na bega la kulia.
 
Baada ya kusomewa shitaka hilo washtakiwa wote walikana na wako nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa   na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya shilingi milioni kumi na kesi hiyo imeahirishwa hadi septemba 10 mwaka huu itakapotajwa tena.
 
Kwaupande  wake  wakili anayewatetea washtakiwa hao watano  Bw.Peter Kibatara akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo  alisema kuwa anaishukuru mahakama kuu Tanzania kanda ya Tabora  kwa kuonyesha ujasiri na kutimiza majukumu yake kama ilivyo kwa kufuata haki na sheria.
 
“Namshukuru jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Simon Lukelerwa kwa kuwa na weredi wa kutoa uamuzi ulio sahihi na kwa kufuata haki na sheria kwani ni maamuzi yaliyoshiba pia naishukuru mahakama ya wilaya ya Igunga kwa kuweza kuwapatia dhamana washtakiwa kwani ni haki yao muhimu na ya msingi sana”alisema Kibatara.
 
Aidha mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora Bw.Kansa Mbaruku alisema kuwa amefurahishwa na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu ya Tabora kwani imezingatia sheria kikamilifu.
 
“Huu ni mwendelezo wa Gharama za haki hivyo tunaamini wanachadema kuwa katika harakati za kuikomboa nchi hii kuna gharama zake ambazo ndizo hizi,hivyo sisi hatuwezi kuvunjika moyo na kukosa nguvu katika kupigania haki za msingi za wananchi na kulikomboa taifa hili kwani lina rasilimali nyingi lakini wananchi hawanufaiki nazo”alisema Mbaruku.
 
Awali washtakiwa hao walifutiwa shitaka lililokuwa likiwakabili la kumwagia tindikali Mussa  Tesha  katika  mahakama  hiyohiyo na baadae kukamatwa tena na kupelekwa Tabora ambapo walisomewa shitaka la ugaidi na baadae  mahakama kuu ya Tanzania  kanda  ya  Tabora iliwafutia shitaka na kuamuru warudishwe Igunga na kusomewa shitaka lililokuwa likiwakabili mwanzo la kumwagia tindikali Bw.Tesha.