Mjumbe wa NEC kutoka mkoa wa Tabora Bw.John Mchele,katikati ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema na mjumbe wa NEC Mheshimiwa William Ngeleja |
Na Mwandishi Wetu,Tabora.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Bw.William Ngeleja amewatahadharisha waendesha Bodaboda nchini kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwa manufaa yao binafsi na kwamba kufanya hivyo watajikuta wanapoteza muelekeo wa maisha kutokana na kuyumbishwa kila kukicha.
Bw.Ngeleja aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Tabora wakati wa semina ya kukiimarisha Chama cha Mapinduzi kwa wenyeviti,makatibu tawi na kata na baadaye kukabidhi msaada wa Pikipiki kwa Chama cha Waendesha Bodaboda mkoa wa Tabora iliyotolewa na Mbunge wa vitimaalum(CCM) mkoani humo Bi.Munde Tambwe.
Alisema kwa siku za hivi karibuni imeshuhudiwa makundi ya waendesha Bodaboda hapa nchini wamekuwa wakitumiwa na wanasiasa kwenye misafara ya maandamano mbalimbali ikiwa ni sehemu ya wanasiasa hao kujiongezea umaarufu na hata wengine kuwatumia kama chanzo cha vurugu kwa kigezo cha kudai haki.
Kupitia Vyama vyao vya Waendesha Bodaboda Ngeleja aliwaasa kutumia fursa hiyo kama sehemu ya kujiimarisha kiuchumi badala ya kutumiwa na wanasiasa kama mtaji katika maandamano yao ambayo kwa hatua za mwisho huwa ni vurugu na mapambano na vyombo vinavyolinda usalama wa raia na mali zao.
"Kwa mfano wenzetu wa upinzani wamewaona nyinyi ni Chambo au mtaji wa kutafuta umaarufu na mwisho wa siku wanawatelekezeni mkiwa hamna la kufanya na pia tumeshuhudia wenzenu wengi katika mikoa mbalimbali wanapata matatizo kwa ajili ya hawa wanasiasa wasiolitakia mema taifa,naomba muwaepuke jamani sio watu wazuri hao"alisisitiza Ngereja.
Akizungumzia dhamira ya kutoa msaada wa pikipiki hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili kwa Chama cha Waendesha Bodaboda mkoani Tabora,Mbunge wa vitimaalum mkoani humo Bi.Munde Tambwe alisema ni moja ya ahadi aliyoitoa baada ya uongozi wa Chama hicho kumuomba awasaidie katika mradi wao waliouanzisha kwa siku za hivi karibuni.
Munde alisema amekuwa bega kwa bega na uongozi wa Chama hicho cha Waendesha Bodaboda katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na kwamba mapema aliwashauri kuanzisha mradi wa pikipiki zao wenyewe badala ya kuwa na pikipiki za watu wengine ambao wanawaajiri kwa kupata ujira usiokidhi mahitaji yao.
Aidha Munde alisema katika makabidhiano ya msaada huo kuwa anaiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma vijana hao wanaoendesha Bodaboda kuwafutia kabisa kodi wanayotozwa kwani bado hawajawa na uwezo kutokana na kujitafutia riziki za kila siku ambazo alidai kuwa bado hazijakidhi hata mahitaji ya kawaida ya binadamu.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda mkoani hapa Amir Kipusi alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Mbunge huyo huku akiomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia kufanikisha mradi wao ambao bado wanahitaji kupata pikipiki zaidi ya 20.
No comments:
Post a Comment