Na Mwandishi wetu, Sikonge
JITIHADA
za mkuu wa mkoa wa Tabora Bi. Fatma Mwassa kuhakikisha mkoa huo unakuwa
na kituo cha kisasa cha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana ili
kuboresha maisha yao zimeanza kuzaa matunda baada ya kituo hicho kuanza
kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali katika
wilaya ya Sikonge mkoani humo.
Hayo
yalibainishwa jana katika ziara maalumu iliyofanywa na mkuu huyo wa
mkoa akiambatana na watendaji wakuu wa serikali ya mkoa na halmashauri
ya wilaya ya Sikonge walipotembelea kituo hicho na kushiriki kazi mbali
mbali pamoja na vijana walioko katika kambi hiyo.
Katika
ziara hiyo Bi. Mwassa na wasaidizi wake walishuhudia shughuli
mbalimbali zilizofanywa na vijana hao kwa ustadi mkubwa katika kituo
hicho ikiwemo ubunifu wa kutengeneza vitu mbalimbali, utengenezaji na
utundikaji wa mizinga ya nyuki, ujenzi wa mabanda ya kufugia nyuki,
ufyatuaji matofali aina ya ‘interlock’, bustani za mboga mboga katika
mtindo wa ‘green-house’, useremala na mengineyo.
Akiwa
katika kituo hicho ambacho kutokana na umaarufu wake vijana hao
wamekipa jina la ‘TULU GREEN CITY’, Mwassa alisema kuwa mpaka sasa
vijana hao wamefanya mambo makubwa kwa mda mfupi jambo linaloashiria mwanzo mzuri huku akiwapongeza wataalamu wote wanaowasaidia vijana hao.
Aidha,
Mwassa aliongeza kuwa vitu vyote vitakavyotengenezwa na vijana hao
vitakuwa vikiuzwa kwa watu mbalimbali ikiwemo halmashauri zote za mkoa
huo ili kuwanufaisha zaidi vijana hao na kwa kuanzia tayari tumeshapokea
oda toka sehemu mbalimbali za kununua matofali hayo na vifaa vingine
vitakuwa vikiuzwa katika maonesho ya kibiashara.
Aidha , Mwassa alibainisha kuwa Tanzania tumeamua kuingia kwenye mfumo wa matokeo makubwa sasa unaojulikana kwa jina la ‘BIG RESULTS NOW’ lengo
likiwa kuwapa vijana ujuzi katika nyanja mbalimbali ili wawe chachu ya
maendeleo kupitia uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa kadhaa wa kadha
sambamba na kuwafundisha vijana wenzao.
Mwassa
alibainisha kuwa nguvu kazi ya vijana hao imeanza kuiva, kazi
zinafanyika kwa uhakika na matumaini juu ya vijana hao ni makubwa, na
kuongeza kuwa kuanzia mwezi Desemba mwaka huu wanatarajia kuanza
ufugaji, kilimo cha mtama, alizeti, viazi vitamu, mbogamboga na mazao
mengine yanayostahimili ukame sambamba na ujenzi wa jengo la utawala na
karakana.
‘Hii
ni fursa muhimu sana kwa vijana wetu wasiipoteze, naomba wana Tabora
waniunge mkono ili ndoto zangu za maendeleo kwa vijana na mkoa kwa
ujumla zitimie na hatimaye tubadilishe uzalishaji katika mkoa huu’,
alisema.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika kituo hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Sikonge Robert Kamoga, alipongeza wazo la kuanzishwa kituo
hicho katika wilaya hiyo na kubainisha kuwa kero za ajira kwa vijana
sasa zitapungua kwa sababu vijana hao watajiajiri wenyewe na kuajiri
vijana wenzao, hivyo akatoa wito kwa jamii kutembelea kituo hicho ili
kujifunza.
Naye
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Shedrack
Mhagama, alisema kuwa wamedhamiria kuwawezesha vijana kupata ujuzi
utakaowawezesha kutengeneza ajira zao wenyewe ili kujiongezea kipato
kupitia uzalishaji mali, ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku, kilimo na
ujenzi, hivyo akawashauri wazazi wawaruhusu vijana wao wajiunge na kituo
hicho.
Vijana
walioko katika kituo hicho Remi Alisemi (22) na Raymond Peter (23)
wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa, walitoa shukrani zao kwa kuanzishwa
kijiji hicho cha mfano na kusema kuwa kimekuwa mkombozi wa maisha yao
kwani awali walikuwa wazururaji tu huku wengine wakiwa wavuta bangi,
vibaka, wabwia unga na hawakuwa na ujuzi wowote ule tofauti na walivyo
sasa.
No comments:
Post a Comment