Pages

KAPIPI TV

Friday, April 5, 2013

MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA AUAWA AKICHUNGA NG’OMBE-SIKONGE

Na Allan Ntana, Sikonge

MTOTO mwenye umri wa miaka 14, aitwaye Ngwege Ngoroma Paul, mwanafunzi
wa darasa la sita katika shule ya msingi Songambele, mkazi wa kijiji
cha Mtakuja wilayani Sikonge, mkoani Tabora, ameuawa na kisha mwili
wake kuchomwa moto na watu wasiofahamika baada ya kumpora ng`ombe
aliokuwa akichunga.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, diwani wa kata ya
Kiloleli, Bonifasi Mtani, alisema tukio hilo lilitokea wiki iliyopita
tarehe 25 machi, mwaka huu majira ya saa nne asubuhi.

Mtani aliongeza kuwa mtoto huyo alifikwa na mauti baada ya kwenda
kuchunga Ng`ombe 13 mali ya baba yake mzazi Ngoroma Paul Ngwengwe
(36).

Diwani huyo alisema kuwa baada ya mtoto huyo kwenda machungoni na
kukaa huko hadi majira ya saa kumi na mbili za jioni, alikutana na
watu wanne ambao inaonyesha kuwa walimnyonga hadi kufa na kisha
wakamchoma moto na kutokomea na ng`ombe wote kusikojulikana.

Aidha aliongeza kuwa kutokana na msako uliofanyika, baada ya siku nne
kupita, ng`ombe hao walipatikana katika kijiji kilichoko kwenye msitu
wa hifadhi ya Impembapasi, wilayani humo, wakiwa wanaswagwa na watu
wanne ambao hawakutambulika majina yao majira ya saa 11:00 jioni.

“Baadhi ya wananchi waliweka mitego sehemu mbalimbali za barabara na
misitu ndipo walipofanikiwa kuona kundi hilo la ng’ombe na watu wanne
wasiofahamika waliokuwa na mifugo hiyo walitimua mbio kuingia msituni
na kuwaacha ng`ombe hao.” alisema diwani huyo.

Diwani huyo aliongeza kuwa tukio hilo liliripotiwa kituo cha polisi na
upepelezi unaendelea, lakini akatoa wito kwa wazazi na walezi kuacha
tabia ya kuwatumikisha watoto ama wanafunzi katika kazi za kuchunga
mifugo na kazi ngumu za mashambani kwani kazi hizo zinawanyima haki
yao ya kupata elimu.

“Natoa wito kwa wazazi na walezi wote kuacha tabia ya kuwatumia
wanafunzi au watoto wadogo kuchunga mifugo kwani inahatarisha maisha
yao kama hili la kuuawa na kuporwa mifugo au kuliwa na wanyama wakali
na hili ni tukio la pili kwa kipindi cha mwaka huu tu.

No comments: