Pages

KAPIPI TV

Wednesday, March 13, 2013

MFADHILI WA MTANDAO WA UWINDAJI WA TEMBO APANDISHWA KIZIMBANI.

Na mwandishi wetu-Serengeti.
Machi 12,2013.

MTUHUMIWA anayedaiwa kufadhili mtandao wa uwindaji na ununuzi wa pembe
za ndovu maeneo mbalimbali ya nchi  mwenye asili ya Rwanda
amepandishwa katika mahakama ya wilaya ya Serengeti akiunganishwa
katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili waliokuwa askari polisi
kutoka mkoa wa Kagera.

Mtuhumiwa huyo aliyeunganishwa kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2013 ni
Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda)ambaye alitajwa
na watuhumiwa wengine kwenye kesi hiyo baada ya kukamatwa na vipande
18 vya meno ya tembo kuwa  ni mfadhili wa mtandao  wa ujangili na
mnunuzi wa meno ya tembo.

Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Amoni Kahimba
mwendesha mashitaka wa polisi Pascal Nkenyenge aliomba kubadilidha
hati ya mashitaka kwa kumwongeza mshitakiwa  wanne baada ya kukamatwa.

Katika hati hiyo awali iliwataja washitakiwa watatu ambao wamefikishwa
mahakamani hapo mara tatu kuwa ni  Boniphace John Kurwa (31)mkazi wa
Geita ,Gerard Tuji Kabalega(33) David Duma Delama(36)ambao walikuwa
askari polisi Bukoba na  Biharamulo.

Mwendesha mashitaka aliiambia mahakama kuwa wanakabiliwa na mashitaka
ya kula njama na kufanya biasshara haramu ya nyara za serikali kinyume
na kifungu namba 84(1)cha sheria ya wanyama pori namba 5 ya mwaka 2009
,pamoja na kifungu 14(b)na 57(1)na 60(20ya kuhujumu uchumi
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma maelezo ya shitaka alisema januari 5 mwaka huu,muda na wakati
usiojulikana mjini Mugumu washitakiwa watatu walikutwa na meno ya
tembo vipande 18 vyenye uzito wa kilo 104 vyenye  thamani ya
sh.67,750,000 mali ya serikali.

Washitakiwa walikana shitaka moja la kula njama ya kufanya biashara
haramu ya nyara,na mashitaka mengine hawakutakiwa kujibu lolote kwa
kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuyasikiliza mpaka kibali cha
Mkurugenzi wa mashitaka ambacho hakijatolewa.

.Kutokana na udhaifu wa hati ya mashitaka ilivyoandaliwa  Hakimu
Kahimba amelazimika kuonya  upande wa mashitaka kuwa makini na kuagiza
kufanya marekebisho katika hati ya mashitaka hayo.

Aliwataka  kufuata taratibu za kisheria kwani mashitaka yaliyoandaliwa
dhidi ya washitakiwa ni dhaifu na hayatoshelezi kwani yanalenga
kuifanya mahakama iweze kuwaachia washitakiwa.

“Mahakama iko hapa kutoa haki kwa pande zote ,nimekuwa wazi kueleza
jambo hili mbele ya mahakama,ningeweza kukaa kimya nikaendelea
kusikiliza kesi, si jambo la busara nikakaa bila kueleza mapungufu
hayo,sipendi mahakama siku ya kutoa hukumu ilaumiwe kwa mambo kama
haya”alisema hakimu Kahimba.

Alimwagiza mwendesha mashitaka atoe taarifa kwa mpelelezi wa
kesi,mpelelezi wa mkoa(RCO),wilaya(OC CID)na wote wanaohusika kufanya
marekebisho ya mashitaka .

Alibainisha kuwa mashitaka yajieleze wazi kila mtuhumiwa alikamatwa
anafanya nini,wapi na muda upi kwa kila kosa badala ya maelezo ya
jumla kuwa wote walikamatwa wanafanya makosa hayo.

Washitakiwa waliomba kulegezewa masharti ya dhamana ambapo
walikubaliwa na hakimu kwa kuruhusu kati ya wadhamini wawili mmoja
atoke Serengeti mwingine nje ya wilaya ,hata hivyo walishindwa
kutimiza  masharti na kesi imeahirishwa hadi march 25 mwaka huu na
washitakiwa wamerudishwa mahabusu.

Masharti mengine yaliyobaki kama yalivyo ni kuwasilisha fedha taslimu
sh.31 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi
hicho iliyofanyiwa uthamini na mthamini wa serikali.

Washitakiwa wawili wakazi wa mjini Mugumu bado wanaendelea kusakwa
baada ya kutoroka siku ya tukio.

No comments: