Pages

KAPIPI TV

Saturday, January 12, 2013

MAJI YA SUMU KUTOKA MGODI WA NORTH MARA YATISHIA MAISHA YA VIUMBE HAI MKOANI MARA.

KUVUJA KWA MAJI YANAYODAIWA YA SUMU KUTOKA MGODI WA NORTH MARA KWA ZUA HOFU.
 

Na Anthony Mayunga-Mara

HOFU imewatanda wakazi wa vitongoji vya Kwinyunyi na Kegonga A,kijiji
cha Matongo wilayani Tarime kufutia maji yanayodaiwa kuwa ya sumu
kutoka bwawa la mgodi wa African Barrick North Mara kuvuja na kuingia
eneo la jamii.

Kuvuja kwa maji hayo kunadaiwa ni kutokana na kuwa ujenzi wa bwawa
hilo ambalo kampuni hiyo inadaiwa kurithi kutoka kwa kampuni zingine
zaidi ya 2 zilizotangulia kujengwa chini ya kiwango.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wajumbe wa serikali ya kijiji hicho
waliliambia Mwandishi wa habari hizi kuwa  tatizo hilo
limeishafikishwa Nemc na mamlaka zingine.

“Kilio chetu ni cha muda mrefu sana …lakini serikali imekuwa ikipiga
chenga kukishughulikia hatujui ni kwa nini … 2009 watu ,mifugo na
mazingira walipata madhara kutoka Mto Tighite mpaka leo ni chenga
tu”alisema mjumbe wa serikali ya kijiji jina tunalo.

Alikwenda mbali sana na kudai kuwa mamlaka za serikali zimekuwa
zikichangia jamii kudhurika na kujenga mahusiano mabaya kati yao na
mwekezaji”matatizo ya maji ya sumu si ya leo lakini wanatupuuza
matokeo wananchi wanaichukia kampuni”alisema.

Alibainisha kuwa desemba 20 ,2012 wataalam mbalimbali kutoka Mwanza na
Dar es salaam wa Nemc na bonde la ziwa Victoria walishuhudia matatizo
hayo na wananchi wakapaza sauti ,wakachukua vipimo lakini hawakuwahi
kutoa majibu.

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo jina limehifadhiwa asema  kuwa
bwawa hilo linavuja kwa sababu waliotangulia walilijenga bila kuweka
hata mipira mizito .

“Hili ni tatizo lazima liangaliwe kwa umakini maana linagusa maisha ya
viumbe hai…maana kilichokuwa kinafanyika hapa ni kiini macho kwa
kampuni kuleta mawe yanayopasuliwa kwa baruti na kumwaga hapa…hayawezi
kudhibiti maji yanayovuja”alisema mfanyakazi huyo.

NEMC.

Mkurugenzi wa utekelezaji na uzingatia wa Nemc Dk,Robert Ntakamulenga
alipouliza kwa njia ya simu amekiri kuwa tatizo hilo lipo na
wanafuatilia.

“Kwa sasa siwezi kusema hatua gani zimechukuliwa na ofisi…lakini wiki
ijayo kikosi kikubwa kitakwenda huko chini ya uenyekiti wa Ofisi ya
Makamu wa Rais Mazingira”alisema .

Alisema kikosi hicho kitashirikisha sekta ya madini,maji na uongozi wa
wilaya ya Tarime kwa lengo la kuona tatizo na namna ya utatuzi
wake”nadhani baada ya hapo ndipo tutakuwa na cha kusema”alisema.

Hata hivyo mmoja wa wataalam wa Mazingira kutoka Nemc jina
limehifadhiwa alisema kuwa tatizo la mgodi huo litaendelea kusumbua na
kuleta madhara kwa kuwa uanzishaji mradi haukuzingatia upanuzi baadae.

“Mgodi umeanza miaka mingi sana…haukuzingatia upanuzi wake na sasa
unazidi kuongezeka bwawa la kuhifadhia majji ya sumu lilichimbwa
wakati mradi ukiwa mdogo sasa inakuwa kazi kuhimili maji hayo…lazima
yatavuja na yataendelea kuvuja,the big challenges”alisema.

Alisema kwa sasa kampuni hiyo inataka kuongeza eneo la bwawa kwa kuwa
hilo limejaa na linavuja,lakini huo uzalishaji unaendelea,na kudai
timu hiyo huenda ikapata ufumbuzi.

Kwa upande wa kampuni ya African Barrick Gold mine North Mara Saimoni
Shayo ambaye  anashughulikia mahusiano alipoulizwa hatua ambazo
wamechukua kudhibiti hali hiyo ,alikwepa kulisemea kwa madai kuwa
wanaopaswa kulizungumzia ni Nemc na bonde la Ziwa Victoria.
“Kimsingi hatupendi kulisemea sisi kwa kuwa tunafanya kazi kwa mjibu
wa sheria za nchi na matatizo yameishazifikia mamlaka hizo,nadhani hao
wakwambie..lakini ninachojua hakuna maji yanayotiririka”alisema.

Hata hivyo ziara ya wataalam wa Nemc na wengine desemba 20,2012
ilikuwa ni kukagua eneo ambalo mgodi ulilenga kupanua bwawa hilo kwa
madai kuwa walishaongea na wananchi ambao walikana kukutana na kampuni
hiyo.

Badala yake walikutana na tatizo la maji yanayotiririka na kuchukua
vipimo ambavyo majibu yake hayajatolewa.

Mei 2009 maji yanayodaiwa kuwa ya sumu kutoka mgodi wa Gokona yalivuja
na kuingia mto Tighite na kusababisha madhara makubwa kwa watu,wanyama
,wadudu na mazingira.

Kamati tatu za bunge za Ardhi,Madini na afya chini ya Job
Ndugai(kwasasa naibu Spika)zilitembelea eneo hilo na kutoa maagizo
mbalimbali,hata hivyo wananchi hawajawahi kupewa ripoti nini
kilibainika na wafanye nini.

No comments: