Pages

KAPIPI TV

Tuesday, January 15, 2013

JOEL BENDERA APONGEZA KAZI ZA VODACOM FOUNDATION


DSC 8818 e0207
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera akimkaribisha ofisni kwake Afisa wa Vodacom Foundation Ally Mbuyu huku Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim na Meneja wa Vodacom Foundation Grace Lyon wakishuhudia. Maofisa hao wa Vodacom walimtemebelea Bendera kumweleza mradi wa Mwei ambao wiki hii utasaidia wajasiriamali wanawake wadogo wapatao 200 wa Luhembe, Wilayani Kilosa.



Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera amepongeza juhudi za kampuni ya Vodacom za kusaidia maendeleo ya Ustawi wa Jamii nchini hususan wanawake ambao kimsingi wanauhitaji mkubwa katika kujiendeleza kiuchumi.

Bendera ametoa pongezi hizo ofisni kwake Mjini Morogoro wakati alipotembelewa na maofisa wa Vodacom kutoka idara ya kusaidia jamii ya Vodacom Foundation na Idara ya Mahusiano kwa lengo la kumpatia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kampuni hiyo wa kusaidia wajasiriamali wanawake wadogowadogo uitwao MWEI(M-pesa Women Empowerment Initiative) mkoani Morogoro.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kampuni ya Vodacom imekuwa mfano mzuri miongoni mwa makampuni ya biashara hapa nchini.

“Kwa kweli siyasemi haya kwa upendeleo juhudi za Vodacom katika kusaidia jamii ni nzuri na zinaonekana na ni imani yangu kwamba mtaendelea kufanya hivyo kwa masilahi ya wananchi na maendeleo ya nchi.”Anasema Bendera 

Kuhusu mradi wa Mwei Mkuu huyo wa Mkoa ameuelezea mradi huo kama mkombozi wa wanawake kutokana na jinsi unavyowafikia na kuwasaidia wanawake.
“Mnawasaidia watu ambao hawafikiwi na mabenki na hata wakifikiwa hawakopesheki na taasisi za kifedha kutokana na udogo wa biashara na mitaji yao licha ya juhudi kubwa wanazozifanya katika kujikwamua kiuchumi.”Alisema Bendera na kuongeza “Wanawake mnaowafikia lazima watambue kuwa hii ni bahati inayowakoa kimaisha katika kustawisha na kuendeleza biashara zao.”Aliongeza Bendera.

Kwa upande wake Meneja wa Vodacom Foundation Grace Lyon alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba MWEI inawapatia wanawake mikopo isiyo na riba wala dhamana huku kigezo kikubwa kinachohitajika ni uthibitisho wa ukaazi wake kutoka serikali ya kijiji hatua ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika kuwawezesha wanawake kukua kiuchumi.

“Katika safari yetu hii ya Kilosa tutawafikia wanawake zaidi ya 200. Vodacom kwa makusudi imebuni mradi huu katika azma yake ya kusaidia wanawake wajasiriamali wadogowadogo ili kuwasaidia kuinua biashara zao. Wanawake tunaowafikia ni wanaofanya bishara ndogondogo ikiwemo ususi, uchuuzi, mama lishe n.k.”Alisema Grace

Grace amesema uwezeshaji wanawake ni eneo moja miongoni mwa maeneo manne ambayo Vodacom Foundation inayapa kipaumbele katika mchango wake kwa juhudi za serikali za kusaidia maendeleo ya nchi. Maeneo mengine ni afya, elimu na mazingira. Tumeshasaidia zaidi ya miradi 130 sehemu mbalimbali nchini. 

Nae Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim amesema Vodacom inatambua wajibu wake kwa jamii nje ya baishara inazofanya hapa nchini kama sehemu ya kujali ushirikiano na uungwaji mkono sokoni inaoupata kutoka kwa watanzania.

Vodacom ni kampuni inayoheshimu umuhimu wa kusaidia jamii kama sehemu ya biashara yake, inatumia kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka katika kusaidia jamii ikiwa pia ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.”Alisema Mwalim

‘Ni wazi kwamba kuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya Serikali na Vodacom kunachochea zaidi utashi huo, misaada yetu kwa jamii ni jambo lililowazi katika miongozo ya biashara zetu kusaidia wale wanaotuzunguka.”Alisema Mwalim

Hii ni mara ya pili kwa Vodacom Foundation kusaidia wajasiriamali wanawake mkoani Morogoro kupitia MWEI. Ilishawahi kufanya hivyo mwaka 2010 ilipowafikia wanawake wajasiriamali wapatao 258 kwa kuwapatia zaidi ya Shilingi 10 Milioni kama mikopo nafuu isiyo na riba wala dhamana.

No comments: