Pages

KAPIPI TV

Wednesday, January 16, 2013

CHADEMA SASA WAANZA KULIPUANA


582442 10152382144810063 1077508772 n 8b1ed
Na: Boniface Meena
KATIKA kuonyesha hali si shwari ndani ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa chama hicho, Juliana Shonza amesema ameamua kumshtaki Mwenyekiti wake, John Heche kwa kumuita kuwa ni msaliti wa chama na kwamba anatumiwa na CCM na kuamua kumfukuza nafasi yake bila kutoa nafasi ya kusikilizwa.


Pia, amemlipua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa akidai kuwa amefanya ufisadi ndani ya chama kwa kujikopesha Sh140 milioni ambazo hajazilipa hadi sasa.
Mbali na hilo, amemshukia Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa kudai kuwa anatoa kauli za kukurupuka ambazo zinakiyumbisha chama hicho kikuu cha upinzani nchini.


Shonza alitoa kauli hizo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juu ya tuhuma zilizotolewa na mwenyekiti wa Bavicha na kuhusu kufukuzwa kwake ndani ya chama akiwa na wenzake Mtela Mwampamba na Habibu Mchange.


“Heche na Mbowe wamenifedhehesha kwa kauli zao na wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa Watanzania, hivyo nitapambana nao kuhakikisha haki yangu inapatikana,” alisema Shonza.


Shonza alisema kwamba yeye bado ni makamu mwenyekiti wa Bavicha na mwanachama halali wa Chadema kwa kuwa hadi anazungumza hakuwa amepewa barua ya kufukuzwa kwa kuwa kikao kilichotoa uamuzi huo ni batili.


Alisema kikao kilichoitwa ni cha kamati tendaji na kufikia maamuzi ya kumfukuza kilikuwa batili kwa kuwa katiba pamoja na mwongozo wa Bavicha ulikiukwa, kitu kinachosababisha aeleze kuwa uamuzi uliotolewa na kikao hicho yalikwishapangwa na viongozi wa kitaifa.


“Nasisitiza kwamba ni ukweli uliowazi kwamba ajenda na maazimio ya kikao hicho yalikwishaamuliwa hata kabla ya kikao hicho, kwa sababu taarifa za kufukuzwa kwetu zilikwishaanza kusikika kwenye mitandao ya kijamii kabla hata ya kamati tendaji batili,”alisema Shonza.


Alisema mkakati wa Heche na vibaraka wake umejikita kutukuza ukanda ndani ya chama waziwazi, akieleza kuwa watu waliofukuzwa ndani ya chama hicho wanatokea Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini haswa Mbeya wakati vijana wa Kaskazini wameachwa kwa madai kuwa wametoa ushirikiano.


“Natarajia kuomba ufafanuzi wa kikatiba juu ya shutuma zilizotolewa dhidi yangu na Heche kwa kuwaaminisha Watanzania uongo wake,”alisema Shonza.


Kuhusu Mbowe
Alisema kuwa amesikitishwa na kauli ya kiongozi wake huyo katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba, madai aliyoyatoa ni ya kitoto kwani ni kitu cha kushangaza kwa kuwa yeye Juliana hayajui ni madai gani hayo.


Alisema kama madai ambayo Mbowe anadai ni ya kitoto ni ya yeye kuhoji kwa nini chama hakiweki akiba kwenye akaunti kwa ajili ya uchaguzi wa 2015 kama ilivyokubaliwa kwenye baraza kuu basi itakuwa ni ajabu.


Kuhusu Dk Slaa
Alisema inashangaza kwa mwenyekiti wa chama anafumbia macho hatua ya Dk Slaa kujikopesha pesa ya ruzuku ya Watanzania zaidi ya Sh140 milioni, kwani ni kinyume na utaratibu uliopo.

 MWANANCHI

No comments: