Pages

KAPIPI TV

Wednesday, December 12, 2012

WAANDISHI WA HABARI WAOMBWA KUELIMISHA JAMII UMUHIMU WA MIFUKO YA AFYA.

Na Hastin Liumba, Tabora
 

WAANDISHI wa habari wameombwa kufuatilia utendaji wa mifuko ya Afya ya
Jamii katika halmashauri zote hapa nchini na kuandika habari zake ili
kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kujiunga na mifuko hiyo na faida
watakazopata punde watakapojiunga.


Rai hiyo imetolewa juzi na Mganga Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dr. Leslie
Mhina,  aliyewakilishwa na  Bumija Muhando katika semina ya siku
moja  iliyohusisha
waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali na waratibu wa mifuko ya afya
ya jamii kutoka katika halmashauri zote za mkoa wa Tabora.


Akifungua mafunzo hayo, Mganga mkuu, alisema kuwa waandishi wa habari ni
watu muhimu sana katika harakati za kuelimisha jamii juu ya  masuala
mbalimbali yanayoihusu jamii, hivyo akawataka kufuatilia kwa makini
utendaji wa mifuko ya afya ya jamii katika halmashauri zote na kuandika
habari zake ili jamii ielewe nini kinachofanyika na faida watakazopata
wakijiunga na mifuko hiyo.


‘‘Naomba msikilize kwa makini sana mafunzo haya, kwani naamini ninyi
waandishi mtatusaidia sana kutangaza na kuhamasisha shughuli za mifuko hii
kwa wananchi, na kupitia habari zenu, wigo wa wanachama katika mifuko hii
utaongezeka’’ alisema Mganga mkuu.


Aidha Mganga Mkuu alibainisha lengo la mafunzo hayo kwa washiriki kuwa ni
kuwapa ufahamu juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mfuko wa taifa wa
bima ya afya, majukumu ya waratibu wa mifuko ya afya ya jamii (CHF),
uandaaji ripoti za CHF na namna ya utoaji huduma, lengo likiwa ni kuongeza
ufanisi kwa waratibu wa CHF na kuboresha huduma zinazotolewa na mifuko hii
ili wananchi wengi zaidi wajiunge.


‘‘Napenda niwakumbushe waratibu wote wa mifuko ya NHIF na CHF kuwa mna
majukumu makubwa ya kuhakikisha wanachama wa mifuko hii wanapata huduma
nzuri na stahiki ili kuwavutia wanachama wengine kujiunga, angalau mwaka
ujao tufikie lengo la kusajili 30% ya wananchi wote wa mkoa huu wa
Tabora’’, alibainisha Mganga mkuu.


Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kanda ya magharibi,
Emanuel Adinan, akifunga mafunzo hayo, alisema kuwa waandishi wa habari ni
wadau muhimu sana katika ufanisi wa mifuko ya afya ya jamii, kwani wana
nafasi kubwa sana katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kupitia kalamu zao.


Aidha, Adinan aliongeza kuwa lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi na
wanachama wote kupata huduma nzuri kupitia mfuko wa bima ya afya, hivyo
akaomba waandishi wa  habari wasaidie kuelimisha na kuhamasisha jamii  juu
ya umuhimu wa mifuko hii katika kumkomboa mwananchi kiafya, pasipokuangalia
kama ni mwajiriwa wa serikali, binafsi au la.


Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari na waratibu wa mifuko ya afya ya jamii
(CHF) yameandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kanda ya
magharibi  na kuendeshwa na Dr. Chijo Matekere,  Emanuel Adinan (Meneja
wa NHIF) na Hipoliti Lello.

No comments: