Pages

KAPIPI TV

Sunday, December 9, 2012

AJALI TENA IRINGA YAUA ZAIDI YA WATU KUMI, YAJERUHI 61.

KWA UFUPI
Askari polisi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo alisema kwamba, wakati dereva huyo akiwa ameshuka chini, ghafla lilianza kurudi nyuma“Ilibidi arukie na kwenda kukanyaga breki, lakini ikashindikana na basi hilo likatumbukia kwenye korongo na kupinduka mara tatu,” alisema askari huyo.
Basi la Usokomi Tours mara baada ya kupata ajali mkoani Iringa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya kumi na majeruhi 61

 WATU tisa wamefariki dunia na wengine 61 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria mkoani Iringa, kupata hitilafu ya breki na kutumbukia kwenye korongo.

Ajali hiyo ilitokea saa 8 mchana jana katika  eneo la Mlima Ihemi, Wilaya ya Iringa Vijijini, ikihusisha basi la abiria maarufu kwa jina la Usokomi Tours.
Basi hilo lilikuwa likitokea Iringa mjini kuelekea Kijiji cha Usokomi wilayani Mufindi.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Faustine Gwanchele alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu hao na majeruhi na kuongeza kuwa,  maiti zimehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo.

Dk Gwachele alisema kuwa, alipokea maiti tisa, zote zikiwa ni za wanawake ambapo sita zilitambuliwa.
Alisema kuwa, kati ya majeruhi 61 waliofikishwa hospitalini hapo na kutibiwa, 33 waliruhusiwa huku 28 wakilazwa, baada ya hali zao kuonekana zinahitaji matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa mmoja wa askari polisi waliokuwa kwenye eneo la tukio, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva kuliegesha gari hilo wakati wakiwa kwenye foleni wakisubiri kuruhusiwa wapite kutokana na barabara hiyo kuwa kwenye ujenzi.
Alisema kuwa, dereva wa gari hilo alishuka akifikiri kondakta wake ameweka kizuizi kwenye tairi, ili kulizuia lisirudi nyuma.
Askari polisi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo alisema kwamba, wakati dereva huyo akiwa ameshuka chini, ghafla lilianza kurudi nyuma.

“Ilibidi arukie na kwenda kukanyaga breki, lakini ikashindikana na basi hilo likatumbukia kwenye korongo na kupinduka mara tatu,” alisema askari huyo.

Alisema basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 64, lakini inaelekea lilikuwa na idadi kubwa zaidi ya hao, wakiwa wamesongamana.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Mchungaji John Mwakione, ambaye alitibiwa na kuruhusiwa alizilaumu mamlaka za usimamizi barabarani kwa kushindwa kuwa makini.
Desemba 3, ajali nyingine ilitokea  eneo la Tanangozi  mkoani humo na kusababisha  vifo  vya  watu  watano, wanne  wakiwa  wa familia  moja .
Ajali  hiyo  ilitokea saa nane mchana wilayani  Iringa katika kizuizi cha barabara  ambapo unafanyika ukarabati wa Barabara  Kuu ya Iringa - Mafinga  mkoani Iringa.
Mashuhuda  wa  tukio   hilo  walisema kwamba chanzo  cha ajali  hiyo ni dereva wa gari dogo aina ya Rav 4  kuligonga kwa nyuma  lori  lililokuwa na tela kwa nyuma, ikielezwa kuwa dereva wa gari hilo alikuwa katika mwendo wa kasi ambapo alishindwa kulimudu, ndipo lilipoligonga lori hilo. 
Ajali hiyo ilipoteza maisha ya Ezekiel Mwaiteleke, mkewe, watoto wake wawili na mfanyakazi wao waliokuwa wakitokea Dar es Salaam, kwenda Kyela mkoani Mbeya,ambao  walifariki papohapo na maiti  zote  kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.

No comments: