Pages

KAPIPI TV

Friday, November 23, 2012

SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA
MAZUNGUMZO NA WAANDISHI WA HABARI (PRESS CONFERENCE)
IJUMAA,  TAREHE 23 NOVEMBA, 2012
MAHALI:     UKUMBI WA MAKUMBUSHO YA TAIFA
Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia ni kampeni kabambe ya kimataifa inayoongozwa na Kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika Uongozi “Women’s Global Leadership” tokea mwaka 1991.
Chimbuko:  
Chimbuko la Siku 16 za kupinga Ukatili  wa Kijinsia ni mauaji ya kinyama ya wadada wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominika mwaka 1960. Kuanzia Novemba 25 mwaka 1991, Umoja wa Mataifa uliitenga siku hii kama Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake. Maadhimisho haya yanafikia kilele tarehe 10 Desemba ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kuadhimisha Tamko Rasmi la Haki  za Binadamu, ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na vile vile kutia msisitizo kwamba ukatili kama huu ni uvunjwaji wa haki za binadamu.  Siku hizi 16 pia hutoa mwanga juu ya siku zingine muhimu kama Novemba 29 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni Siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 6 ni siku ya kukumbuka mauaji ya kikatili ya Montreal ya mwaka 1989, ambapo (Wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake).
Siku hizi 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia zimekuwa zikitumika na wadau ulimwenguni kote kama mbinu mahsusi za kutoa wito kwa jamii ili kumaliza aina  zote za ukatili wa kijinsia kwa kufanya yafuatayo:-
·        Kujenga uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia kama uvunjwaji wa haki za binadamu kijamii, kitaifa, kikanda na kimataifa.
·        Kuimarisha kazi za kupinga ukatili wa kijinsia katika ngazi za chini na kujenga daraja kati ya kazi za maeneo mbalimbali yanayoshughulikia ukatili dhidi ya wanawake.
·        Njia ya kubadilishana taarifa na uzoefu katika kuzuia na kupambana na  ukatili dhidi ya wanawake kati ya wadau.
·        Njia ya kuonyesha mshikamano ulimwenguni kote kupinga ukatili wa kijinsia.
·        Kama chombo cha kutumia kupaza sauti  ili wadau wote waweze kutekeleza wajibu wao katika kupiga vita ukatili  wa kijinsia.
Kila mwaka kumekuwa na kauli mbiu kuhusiana na ukatili dhidi ya  wanawake.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “FUNGUKA: KEMEA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE. SOTE TUWAJIBIKE”. Kwa mwaka huu kauli mbiu inasisitiza kuchukua hatua kwa kukemea ukatili dhidi ya wanawake.  Taifa likiwa limejaa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa makundi fulani ya watu hususan wanawake taifa hilo linabaki kuwa taifa lisilokuwa na mshikamano na amani, miongoni mwa wananchi wake. Hivyo basi hatuna budi sote kama jamii kukemea jambo hilo la ukatili ili kuweza kudumisha mshikamano, amani na maendeleo.
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka kwa kasi kubwa, mathalani takwimu za utafiti uliofanywa na WiLDAF mwaka 2012 kwenye magazeti zilionyesha kwamba  taarifa  6,001 za ukatili ziliripotiwa kwenye magazeti ikilinganisha na 3,542 za mwaka 2011.  
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Idara ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2010 inaonyesha kwamba;
§  Asilimia 39 ya wanawake wanaafiki kwamba  mume ana haki ya kumpiga mkewe iwapo mke atajibishana naye.
§  Asilimia 37 ya wanawake waliohojiwa wanaafiki kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe kwa sababu ya kuondoka nyumbani bila ya kumuaga mumewe.
§  Asilimia 40 ya wanawake wanakubali kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe pale mwanamke anapozembea kuangalia watoto.
§  Asilimia 30 ya wanawake wanakubali kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe iwapo atakataa kufanya tendo la ndoa.
§  Asilimia 18 ya wanawake wanaafiki kwamba  mume ana haki ya kumpiga mkewe ikiwa ataunguza chakula.
§  Asilimia 53 ya wanawake wanaafiki kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe kwa sababu nyingine yeyote ile.
Ukatili  wa Kijinsia  umekuwa ukifanywa kwa njia mbali mbali kama vipigo, ukeketaji, ubakaji, mauaji ya wanawake na watoto wa kike, mauaji ya Albino, kurithi wajane, ukatili nyumbani n.k. Ukatili una athari mbaya  kwa wanawake, kwani huathiri afya zao kimwili na kisaikolojia na hivyo hupelekea  kudidimiza maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla wake.  Aidha ukatili wa kijinsia husababisha msongo wa mawazo, kutokujiamini, ulemavu wa kudumu na wakati mwingine kifo.  Bado tunaamini mabadiliko chanya  yanaweza kutokea na hivyo kuwa na jamii isiyokuwa na  ukatili wa kijinsia. Changamoto kama mfumo dume, mila na desturi zilizopitwa na wakati, umaskini pamoja na elimu duni ni lazima tupambane nazo vilivyo ili kutokomeza ukatili wa kijinsia. Ni lazima  tuzingatie kwamba  hata kama sisi wenyewe siyo wahanga wa ukatili, tuna wajibu wa kutokaa kimya tunapowaona jirani, marafiki na watu tunaowafahamu wanafanyiwa ukatili wa kijinsia. 
Kutokana na hali hii, Tanzania kama nchi nyingi duniani imekuwa ni sehemu ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Kwa hapa Tanzania, kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia, inaratiwa na  Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kwa shirikiana na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) pamoja na Kikosi kazi cha maandalizi ya Siku 16 ambacho kinajumuisha  pamoja na idara mbali mbali za serikali zikiwamo wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania. Kampeni hii inafanyika katika kanda mbalimbali na kuzinduliwa rasmi kote nchini tarehe 26/11/2012. 
Ifuatayo ni orodha ya kanda mbalimbali  na waratibu wake nchi nzima. Kanda ya Mashariki (Dar es salaam, Morogoro na Pwani)  inaratibiwa na WiLDAF, Kanda ya Kati (Dodoma na  Singida) inaratibiwa na Mtandao wa Kutokomeza Ukeketaji wa Wanawake (AFNET), Kanda ya Magharibi (Kigoma na Tabora) inaratibiwa na Jeshi la Polisi, chini ya mtandao wa wanawake polisi (TPFNet)Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Arusha) inaratibiwa na Shirika linalojihusisha na Ukeketaji (NAFGEM), Kanda ya ziwa (Mwanza, Shinyanga na Mara) inaratibiwa na shirika la KIVULINI pamoja na Action Based Community Foundation (ABC Foundation) na Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi, Mbeya, Iringa na Songea) inaratibiwa na Kituo cha Wasaidizi wa Msaada wa Kisheria Iringa.
Katika kanda ya Mashariki yaani Dar es salaam, Pwani na Morogoro Shughuli zifuatazo zitafanyika;
Uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Utafanyika tarehe 26 Novemba, 2012, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP Hall), mgeni rasmi atakuwa ni NaibuWaziri wa  Sheria na Katiba  Mheshimiwa Angelah Kairuki. Katika siku hii mada mbalimbali kuhusu ukatili wa kijinsia zitajadiliwa zikiwamo :-
·        Fomu Mpya ya Polisi Namba 3
·        Ripoti ya Utafiti Kuhusu Ukaitli wa Kijinsia na Makosa ya kujamiiana kulingana na Sheria ya Kanuni za Adhabu,  Sura ya 16.
·        Dhana ya ukatili wa kijinsia na Dhima ya Jeshi la Polisi kuitokomeza.
·        Hali halisi ya huduma za afya kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
Aidha, Fomu ya Polisi namba 3 (Mpya) itazinduliwa rasmi.  Aidha  msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia utazinduliwa. Msafara huu uaanza Dar es salaam siku ya tarehe 26 Novemba na kwenda Kilimanjaro, Singida, Shinyanga, Mwanza na kuishia Mara (Tarime), wilabya ambayo imekubuhu kwenye suala la ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike.
Aidha, katika siku hii ya uzinduzi Msaada wa Kisheria na maonyesho mbali mbali pamoja na elimu ya afya vitatolewa bila malipo.
Kutakuwa na shughuli mbalimbali za kampeni kupinga ukatili wa kijinsia zitakazofanywa na Mashirika na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia. Baada ya uzinduzi wa tarehe 26 Mashirika yatakayokuwa na shughuli katika siku 16 ni pamoja na;
·        27/11/2012          Jeshi la Polisi
Katika harakati ya kupunguza uhalifu Polisi watatembelea kila nyumba – Dar es salaam kuhamasisha jamii kukemea ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, kubandika matangazo dhidi ya  ukatili wa kijinsia kwenye magari n.k.
·        28/11/2012          Jeshi la Polisi
Katika harakati ya kupunguza uhalifu Polisi watatembelea kila nyumba – Dar es salaam kuhamasisha jamii kukemea ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, kubandika matangazo dhidi ya ukatili wa kijinsia kwenye  magari, n.k.
·        28/11/2012          World Vision
Watakuwa na Kampeni kuhusu Afya ya Mtoto sasa, Mgeni rasmi- Waziri Mkuu.
Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro Kempinski.
·        29/11/2012          TAWLA
Diamond Jubilee
Mjadala kuhusu Ukatili wa Kijinsia
Mgeni Rasmi Dk. Asha Rose Migiro.
·        30/11/2012          Jeshi la Polisi
Katika harakati ya kupunguza uhalifu Polisi watatembelea kila nyumba katika jiji la Dar es salaam kuhamasisha jamii  ili kukemea ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, kubandika matangazo dhidi ya ukatili wa kijinsia kwenye magari n.k.
·  28-30/11/2012      WiLDAF
Kusimamia na kufuatilia  msafara wa kupiga vita ukatili wa kijinsia
·        3-4/12/2013        Jeshi la Polisi
Katika harakati ya kupunguza uhalifu Polisi watatembelea kila nyumba – Dar es salaam kuhamasisha jamii kukemea ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
·        5/12/2013                        Equality for Growth (EFG)
Uzinduzi wa Kupiga vita ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Ilala watatembelea masoko mbalimbali ya wilaya hii.
·        6/12/2013                        EngenderHealth/CHAMPION Project.
Uzinduzi wa Kupiga vita ukatili wa kijinsia mkoa wa Iringa. Watatembelea vijiji 20 vya Iringa.
·        8/12/2013                        Children Dignity Forum CDF
Watatoa msaada wa kisheria Mkoa wa Pwani, pia wataendesha shughuli mbalimbali kupiga vita ukeketaji katika Mkoa wa  Mara, Wilaya ya Tarime.
·        10/12/2013          Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Kwa kushirikiana na wadau wengi wataratibu maadhimisho ya  Siku ya Haki za Binadamu tarehe 10/12/2011 hapa hapa Dar es salaam na kuhitimisha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Mwisho kabisa ninapenda kutoa wito kwa jamii kwamba kila mmoja wetu anaweza kukemea na kuchukua hatua dhidi ya ukatili dhidi ya wanawake. Dhamiria kutofanya ukatili, zungumza wazi kuhusu ukatili wa kijinsia, saidia wanawake na watoto wanaofanyiwa ukatili, jiunge na makundi yanayokemea ukatili.   Kwa pamoja tuzinduke, tukemee ukatili dhidi ya wanawake, sote tunawajibika.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa  na:-
Dk. Judith N. Odunga
MRATIBU  KITAIFA
Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika  (WiLDAF)
S. L. P 76215,
DAR ES SALAAM,
SIMU:             2701995,
Barua pepe:    wildaf_tanzania@yahoo.com

No comments: