Pages

KAPIPI TV

Tuesday, November 27, 2012

PICHA BAADA YA AJALI ILIYOSABABISHA KIFO CHA MSANII SHARO MILIONEA


TUNAOMBA RADHI KWA PICHA HII

 Jana majira ya saa mbili usiku, msanii na mchekeshaji maarufu nchini Hussein Mkiety au maarufu kama Sharo Milionea alifariki dunia kufuatia  ajali mbaya ya gari wakati akitokea Dar es Salaam kuelekea wilayani Muheza, Tanga.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Costantine Massawe, Hussein
Ramadhani au Sharo Milionea alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye nambari za usajiri T478 BVR, na  alipofika maeneo ya Segera gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa, likagonga mti na hatimaye kusababisha kifo chake ambapo marehemu alitokea mbele ya kioo cha gari na kutupwa mbali na gari lake.

Alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza. 

Hata hivyo akifafanua ajali hiyo kamanda Massawe aliongeza kuwa hakuna kona kali wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopatia ajali hiyo huku akiweka bayana Gari lake imehifadhiwa mahali salama kwakuwa limeharibika vibaya na kwamba kwenye gari alikuwa yeye mwenyewe.


Habari kuhusu kifo chake zilianza kuenea jana usiku ambapo kwa upande wa rafiki yake wa karibu Kitale alisema alikuwa akiipiga simu ya Sharo Milionea iliyokuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na kisha kupigiwa simu na Tundaman, Mzee Majuto na Mjomba wake Sharo kumtaarifu juu ya kifo hicho.

“Sisi binadamu tunaweza kuwaza hivi lakini Mungu naye akawaza lake kwahiyo sisi tunaziombea familia hizi Mungu azipe faraja ya kweli na faraja ya kweli nadhani inatoka kwa Mungu,”Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania , TAFF Simoni Mwakifwamba ameiambia TBC.

Kwa upande wake Steve Nyerere alisema kifo cha Sharo Milionea kimetokea wakati ambao alikuwa ameanza kufanikiwa. “Sharo umri wake na mambo aliyoanza kuyafanya ni makubwa. “Sharo alishaanza kupata matumaini yaani ni sawasawa unatupa mbegu halafu uitegemee inaanza kuchepua. 

Sharo alishaanza kuchepua, anachepua ile mbegu yake, ameanza kujisaidia yeye kama yeye sababu katika maisha lazima kwanza uanze kujisaidia wewe kama wewe halafu pili uiangalie jamii uone inahitaji nini kwako. Sharo mejipatia usafiri maskini ya Mungu, pa kulala, na maisha yote ya kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga kuwaona wazazi kwa kutumia gharama yake.”Steve alisema jambo la msingi ni kumwachia Mungu na kuondoa mawazo mabaya kuhusiana na kifo chake.

Umoja wasanii wa filamu nchini umesema umepata pigo kubwa hasa kwakuwa bado wana msiba wa msanii mwingine wa filamu, John Stephano ambaye anatarajia kuzikwa leo. 
Aidha kwa upande mwingine Umoja huo umesema baada ya mazishi hayo leo watasafiri kwa mabasi mawili kuelekea wilayani Muheza kwaajili ya mazishi.

No comments: