Pages

KAPIPI TV

Thursday, November 8, 2012

MAHAKAMA KUU YA ZANZIBAR YAAMURU VIONGOZI WA UAMSHO WAENDELEE KUBAKI RUMANDE

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
ZANZIBAR ALHAMISI NOVEMBA 8, 2012. Viongozi wa Jumuiya mbili za Kiislam Kisiwani Zanzibar wanaotuhumiwa kwa makosa tofauti ya kutoa lugha za uchochezi na kusababisha ghasia na vitendo vya uvunjifu wa amani uliopelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara ambao leo walifikishwa Mahakama Kuu ya Vuga mjini Zanzibar, wamerudishwa tena Rumande.
Kesi hiyo ambayo inawakabili Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikhe Faridi Hadi Ahmedi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na  Ghalib Ahmada Omar iliitwa mahakama kuu kwa kutajwa baada ya kuahirishwa mwezi uliopita.
Hata hivyo, kabla ya kutajwa tena kwa kesi hiyo, huku kukiwa na ulinzi mkali wa Makachero wa Polisi na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, ndani ya Mahakama hiyo kulizuka mabishano makali ya kisheria huku kila upande ukionyesha ujuzi wao wa kisheria.
 
Kwa upande wa Mawakili wa Watuhumiwa Bw. Salum Toufik na Bw. Abdallah Juma Kaka, wakiwasilisha hoja mbalimbali za uvunjifu wa haki za watuhumiwa ikiwemo ya kunyolewa ndevu wakiwa Rumande katika Chuo cha Mafunzo jambo ambalo ni kinyume na uhuru wa kuabudu kwani wamesema ndevu kwa mashehe ni sehemu ya ibada.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ramadhani Nassibu, akinukuu vifungu vya sheria vilivyopo kwenye Katiba ya Zanzibar na kusema kuwa kama kuna haki zinazovunjwa na chombo chochote ama mtumishi wa Serikali kuna mahala pengine pa kupeleka malalamiko hayo.
Baada ya mabishano hayo, Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru watuhumiwa wote warudishwe tena rumande hadi Novemba 20, mwaka huu itakapokuja tena katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kutajwa.

..............0784 886488, 0715 886488, 0767 886488 Insp. Mhina

No comments: