MTANDAO wa Chama cha Watetezi wa Kutetea watu wanaojishughulisha na
Utetezi wa Haki za Binadamu (THRD-Coalition) umewataka watetezi
kushirikiana kimakundi katika kufanya kazi hizo pale wanapoona mazingira
yao ya usalama yapo hatarini.
Wito huo ulitolewa na Mratibu wa Kitaifa wa THRD-Coalition, Onesmo
Olengurumwa, katika warsha ya siku tatu iliyoanza jana jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kuwajengea uwezo na mbinu mbalimbali za kufanya kazi
zao kwa umakini bila kupata matatizo.
Olengurumwa alisema ushirikiano huo utawafanya kuwa na nguvu zaidi na usalama tofauti na mtu anapokuwa mmoja mmoja.
Kwa mujibu wa Olengurumwa ni mazingira hayo hatarishi ndiyo
yamefanya kuundwa kwa mtandao huo kwa kuwa ukweli ni kwamba watetezi
hawana wa kuwatetea kama ilivyo kwa makundi mengine.
Alisema mafunzo hayo yatawajengea mbinu za namna gani ya
kukabiliana na mazingira ya kufanya kazi na kutolea mfano sakata
lililomkuta Dk. Stephen Ulimboka na baadhi ya waandishi wa habari mkoani
Iringa.
“Ni vizuru watetezi tukafahamu kwamba kuna baadhi ya watu hawapendi
kazi zetu, hivyo ni vyema tukajijengea mazingira mazuri kuona tunaishi
kwa usalama,” alisema mratibu huyo.
Kuhusu changamoto, Olengurumwa alisema kutokana na mfumo wa
uendeshwaji wa serikali wamejikuta wakifanya kazi katika mazingira
magumu.
Pia aliwaasa watetezi kuwa na msimamo, kwa madai kwamba kuna baadhi
yao wanachanganya suala la utetezi na mambo ya siasa jambo ambalo
hawataweza kufanya kazi zao vilivyo.
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Azavel Lwaitama,
alipongeza hatua ya kuanzishwa kwa mtandao huo ambao alidai Kenya
uliwasaidia baadhi ya maafisa kutoka Tume ya Uchaguzi ya nchini hiyo
kutoroka ili kuepuka kudhuriwa kipindi cha uchaguzi wao.
Kwa mujibu wa Lwaitama mafunzo
hayo yatawawezesha washiriki kujua namna gani ya kutunza hata siri zao
walizozihifadhi katika kompyuta zao, picha kwenye kamera, na mawasiliano
ya kwenye simu.
Mtandao wa THRD-Coalition unajumuisha watu mbalimbali ikiwemo
waandishi wa habari, wanaharakati kutoka mashirikia mbalimbali, ambapo
umeanzishwa tangu mwaka 2010 na upo chini ya Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu.
No comments:
Post a Comment