Pages

KAPIPI TV

Thursday, October 18, 2012

ASKARI POLISI AUAWA KINYAMA VURUGU ZA ZANZIBAR

Na . Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohammed-Maelezo

Askari mmoja wa Jeshi la Polisi F.2105 Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini majira ya saa 6.30 usiku katika eneo la Bububu. 

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema mauaji hayo yamesababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana.

 Kamishna Mussa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu waliofanya mauaji ya Coplo Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani kama sheria za nchi zinavyowaelekeza. 

Amesema mpaka hivi sasa watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu za jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea.

 Ameongeza kuwa kutekwa kwa Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar Said ambae alikuwa dereva wake katika hatua za mwisho maeneo ya Mazizini walipokwenda kununua umeme.

 “Sheikh Farid alimuamuru Said amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme na wakati huo akaendelea na mazungumzo na watu wengine walikuwemo ndani ya gari nyingine ndogo ya NOAH ambayo nambari zake hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta” alisema Kamishana Mussa.

Amesema fujo hizo zilisababisha hasara kubwa kwa Serikali, Chama tawala na wananchi ikiwemo kuchoma na kuharibu miundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za CCM za Kisonge na Muembeladu kwa kuzichoma moto baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka la pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani.

Hata hivyo amedai hali ya Mji wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote. 

Amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, na kutoa taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na mauaji ya Coplo Said Abdulrahaman.

 IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments: