Waziri Masoud:Sioni sababu yakujiuzulu. Asema dhoruba iliizamisha Mv.
Skagit .Balozi Seif asema tukio limeitia doa serikali. Waafrika Kusini,
Waisrael wazamia kuifuata
Na Waandishi wetu
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano,
Hamad Masoud Hamad, amesema haoni sababu ya kujiuzulu nafasi yake,
kufuatia janga la kuzama kwa meli ya MV.Skagit iliyopoteza maisha ya
zaidi ya watu 68.
Waziri huyo alieleza hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari
alipokuwa akielezea kadhia ya ajali hiyo, ambapo katika mkutano huo
waziri wa Uchukuzi wa Tanzania bara Harrison Mwakyembe na Naibu wake
Lazaro Nyalandu nao walihudhuria.
Waziri Masoud alisema meli hiyo ilizama kutokana na janga la
kimaumbile, kufuatia upepo mkali uliosababisha mawimbi na hatimaye
kuzama kwa boti hiyo.
Alisema haoni sababu ya msingi ya kujiuzulu kufuatia ajali ya kuzama
kwa meli hiyo licha ya kutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu
kuzama kwa meli ya MV. Spice Islander.
Alikiri kuwepo kwa maoni ya watu kumtaka ajiuzulu na kuwaeleza watu wa
aina hiyo kuwa hakuna mtu anayeweza kuzuia majanga ya kimaumbile kama
upepo yasitokezee.
"Kumekuwa na watu wanaotoa maoni juu ya suala la kujiuzulu, lakini bado
hakuna mtu anayeweza kuzuiya upepo usitokee kwani hauko katika mamlaka
yake",alisema waziri huyo.
"Kuna wengine wanasema tumemkosa kule sasa watanipatia kwa hili,
nimeshapata taarifa kuwa kuna ‘private member’ watapeleka hoja katika
Baraza la Wawakilishi ya kujiuzulu, nimeshasikia na wimbo huu unaimbwa
tena na natumiwa meseji kuulizwa nitajiuzulu wakifa wangapi kwani mimi
napenda kuua", alisema.
Waziri Masoud alisema kutokana na ajali hiyo haitakuwa busara kuona kwa
wakati huu kuanza kuzungumzia suala hilo na badala yake waendelee
kushirikiana na serikali yao kuona wanaiunga mkono katika kusaaidia
maafa hayo.
Akizungumzia juu ya watalii waliopatwa katika ajali hiyo alisema ni 15,
ambao wanatoka nchini Ubelgiji, Israel, Uingereza na Marekani ambapo
hali zao zipo vizuri baada ya serikali kuwapatia misaada mbali mbali na
inatarajia kufanya utaratibu wa kuwarejesha nyumbani kwao.
KAULI YA BALOZI SEIF
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa
serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesikitishwa na tukio la pili la kuzama
kwa meli ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Balozi Seif alisema tukio la kuzama Mv.Skagit limeiweka serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibra yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa kwenye wakati
mgumu kwani baada ya kuzama MV. Spice Islander I, ilijipanga
kuhakikisha tukio lile halijirejei.
Alisema ni jambo la kushangaza sana, kujitokeza tukio la kuzama kwa
meli likifanana na kama lile la mwaka jana, ambapo mikakati ya
kuhakikisha halijitokezi iliwekwa.
Balozi Seif alisema kujitokeza tena kwa tukio hilo ndani ya kipindi cha
mwaka mmoja kunaifanya serikali kuonekana haiko makini katika kusimamia
mambo yake.
Balozi alisema hivi sasa serikali inafanya juhudi za kuhakikisha
inafanikiwa kukamilisha uokozi ambapo kwa mujibu ya idadi ya
waliokuwemo katika meli hiyo walikuwemo watu 290 ambapo watu 146
waliokolewa wakiwa hai pamoja na maiti 67, huku 77 ikiwa bado
hawajapatikana.
WABUNGE
Wabunge wa Bunge la Tanzania walifanya ziara maalum kuwatembelea
majeruhi wa ajali ya Mv.Skagit katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja
pamoja na eneo la Maisara ambapo miili inayoopolewa hufikishwa katika
eneo hilo kwa kutambuliwa na jamaa zake.
Katika hospitali ya mnazi mmoja Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa
jimbo la Chambani, Salum Hemed, waliwafariji wajeruhiwa waliokua
wamelazwa katika wodi maalum iliyotengwa kwa ajili yao huku wakipatiwa
matibabu.
WAZAMIAJI WAANZA KAZI
Mamlaka ya Usafiri wa Bahari (ZMA), imesema kuwa wataalamu sita wa
uzamiaji kutoka mataifa ya Afrika Kusini na Israel wameanza kuisaka
meli ya Mv. Skagit iliyozama Jumatano iliyopita karibu na kisiwa cha
Chumbe.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Abdullah Kombo, alilithibitishia
Zanzibar Leo kuwa wataalamu hao jaa wameanza kazi ya kuzamia chini ya
kina cha baharini kuisaka meli.
Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali zilizotolewa na
wataalamu hao zinaeleza kuwa Mv. Skagit ipo chini ya bahari umbali wa
mita 28.
"Wazamiaji wamefika katika eneo meli ilipo zama na wamebaini meli hiyo
ipo chini umbali wa mita 28, muelekeao wa digirii 06`26.23 kusini na
digirii 039` 10.40. mashariki",alisema Kaimu huyo.
Alifahamisha kuwa watalaamu hao wa uzamiaji baharini ambao wamepiga
kambi Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, wameamua kufanyakazi ya ujasiri
kama njia ya msaada na kwamba wamekuwa wakishirikina na vikosi vya
Tanzania katika kazi hiyo.
Miongoni mwa vikosi wanavyoshirikiana nanyo ni pamoja na Kikosi Maalum
cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kikosi cha Majini cha Jeshi (NAVY) na
wazamiaji wengine wa kienyeji.
CHANZO CHA AJALI
Kaimu huyo alisema chanzo cha kuzama kwa MV. Skagit kimetokana na hali
mbaya ya hewa wakati kikianza safari yake kutoka jijini Dar es Salaam
kuelekea bandari ya Malindi iliyopo Zanzibar.
Alisema wakati chombo hicho kikikaribia kisiwa cha Chumbe, kulikumbana
na mawimbi makali yaliyotokana na dhoruba iliyotoka upande wa kusini.
Kombo aliwataka wananchi kutofautisha mazingira yaliyosababisha kuzama
kwa MV. Spice Islander na tukio la kuzama kwa MV. Skagit ambapo tukio
la juzi lilisababishwa na hali mbaya ya hewa iliyotokana na kuchafuka
kwa bahari.
Kaimu huyo alisema kwa mara ya mwisho MV.Skagit ilifanyiwa ukaguzi
(survey), mwishoni mwaka uliopita na kwamba kiliridhisha na kupewa
idhini ya kusafirisha abiria na mizigo.
Akizungumzia juu ya tuhuma za marekebisho ya uundwaji wa meli hiyo,
alisema hawezi kueleza jambo lolote kwani harakati zote za usajili wa
meli hiyo zilikuwazimeshafanyika awali kabla ya kukaimu nafasi hiyo.
"Mimi naingia taratibu hizo zimeshafanyika hivyo siwezi kuthibitisha hilo", alisema Kombo.
MISAADA YAANZA KUTOLEWA
Kufuatia kuzama kwa mei hiyo misaada ya pole imeanza kutolewa ambapo
jana Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF), kila mfuko uliwasilisha shilingi milioni 10 kama ubani
kwa wafiwa na majeruhi.
Misaada hiyo alikabidhiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi katika ofisi yake ndogo iliyopo katika jengo la Baraza la
Wawakilishi liliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Balozi aliishukuru mifuko hiyo kwa misaada yao hiyo waliyoitoa na kuwaonea huruma wale waliofikwa na janga hilo.
No comments:
Post a Comment