Pages

KAPIPI TV

Thursday, July 12, 2012

JESHI LA POLISI MKOANI TABORA LAFANIKIWA KUWAKAMATA WALIOUA MKE NA MUME"Sungusungu kumi na moja nao watiwa mbaroni kwa kuhusika na mauaji ya watu watatu Igunga"

 Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha akiwaonesha panga lilnalodaiwa kutumiwa na wauaji katika tukio la mauaji ya mke na mume huko katika kijiji cha Inala kata ya Ndevelwa manispaa ya Tabora.
 Mwili wa marehemu Khalid Said aliyeuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wawili waliowavamia nyumbani kwao.
Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini akipata maelezo kutoka kwa mtoto wa marehemu hao wawili waliouawa kikatili nyumbani kwao kijiji cha Inala kata ya Ndevelwa manispaa ya Tabora.

Siku moja mara baada ya kufanyika kwa tukio la mauaji ya watu wawili mke na mume huko katika kijiji cha Inala kata ya Ndevelwa Manispaa ya Tabora,Jeshi la Polisi mkoani humo limewakamata watu watatu ambao wanadaiwa kuhusika na tukio hilo la kikatili.

Akizungumza na mtandao huu kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha baada ya kuwataja waliouawa kuwa ni Khalid Said na mkewe Amina Ally, amethibitisha kuwatia mbaroni watu hao ambapo wamehusika katika kutenda tukio hilo kuwa ni Mheshimiwa Sakalambe Maganga ambaye ni mkazi wa Inala,Jumanne Mohammed(30) mkazi wa Mbalala Kigwa wilaya ya Uyui na mwingine ni Mabula Masanja(33)mkazi wa Mbuyuni Kigwa.

Aidha kamanda Rutha alieleza kuwa baada ya kupata taarifa za ugomvi uliokuwapo baina ya Marehemu Khalid na mtuhumiwa wa kwanza Mheshimiwa  Maganga waliamua kumhoji na hivyo alitoa maelezo kuwa ni kweli yeye alihusika kuwakodi vijana wawili kuja kufanya tukio hilo kwa ujira wa ng'ombe wawili au milioni moja huku akiwataja vijana hao,lakini akidai kuwa hakuwatuma kuua bali ni kuwapa vitisho familia ya marehemu  hadi wahame katika eneo la ardhi ya urithi waliyokuwa wakigombea kwa muda mrefu.

Kamanda Rutha alisema harakati za kuwasaka vijana hao zilianza na hatimaye kufanikiwa kuwakamata eneo la kijiji cha Kigwa wilaya ya Uyui ambao nao walikiri kuhusika na tukio hilo la kinyama huku akifafanua kuwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni.

Katika tukio jingine Jeshi la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kuwakamata askari wa jadi wapatao kumi na mmoja maarufu kama Sungusungu kwa kuhusika na tukio la mauaji ya watu watatu huko wilayani Igunga.

Kamanda Rutha amedai Sungusungu hao walifanya kosa la mauaji ya watu hao watatu wakiwatuhumu kuiba simu ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 40,000/= 

Sungusungu hao imedaiwa baada ya kuwamata watu hao watatu waliwapeleka porini kuwatesa hatua ambayo ilifuatiwa na kuwachoma moto baada ya kuwapatia kipigo kilichosababisha vifo vyao.

Aidha kamanda Rutha alisema kuwa Sungusungu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kutoka sasa.



    

No comments: