1. Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liweze kujadili na
kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa
fedha 2012/2013. Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu vinne vya
Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinaelezea makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika,
napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa
mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb);
Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb); Mhe. Dkt. Harrison George
Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb); Mhe. Balozi
Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb). Aidha,
napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa naibu mawaziri katika
Wizara mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya
Salum (Mb); Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface
Simbachawene (Mb.); Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles
John Tizeba (Mb.); Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela
Jasmine Kairuki (Mb.); Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe.
Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe.
James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge.
4. Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia, Mhe.
Alhaji Adam Kimbisa (Mb.); Mhe. Shy Rose Banji (Mb.); Mhe. Abdulah
Alli Hassan Mwinyi (Mb); Mhe. Charles Makongoro Nyerere (Mb); Mhe. Dkt
Twaha Issa Taslima (Mb); Mhe. Nderkindo Perpetua Kessy (Mb); Mhe.
Bernard Musomi Murunyana (Mb); Mhe. Anjela Charles Kizigha (Mb.); Mhe.
Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye
Bunge la Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu watatuwakilisha vyema kwa
maslahi na manufaa ya Taifa letu.
5. Mheshimiwa Spika,
maandalizi ya Bajeti hii yamehusisha wadau na Taasisi mbalimbali.
Napenda kuwashukuru walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha
matayarisho yake. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya
Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Mtemi Andrew John Chenge,
Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa
ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii.
Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo
yao ambayo yamezingatiwa katika Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika, napenda
kumshukuru Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Mahusiano na Uratibu kwa ushirikiano alionipatia wakati wa
maandalizi ya Bajeti. Aidha, nawashukuru Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe.
Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb). Namshukuru
Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah; Naibu Katibu Wakuu, Ndugu Laston
T. Msongole; Dkt. Servacius B. Likwelile; na Ndugu Elizabeth Nyambibo
kwa mchango wao mkubwa katika matayarisho ya Bajeti. Vilevile,
nawashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Dkt. Phillip Mpango, Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya
Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya bajeti hii.
Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha
kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na nyaraka
mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
7. Mheshimiwa Spika, napenda
kuwashukuru Wakuu wa Idara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Fedha na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao.
Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii
kwa wakati. Nawashukuru pia wataalamu na wale wote waliotoa
mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo
yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
8. Mheshimiwa Spika, Tanzania
imekuwa mwenyeji wa Mikutano ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika kwa Mwaka 2012 iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Mei hadi
tarehe 2 Juni 2012 na kufunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mikutano hii
ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350 kutoka ndani na nje ya
Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa Tanzania kutangaza fursa
mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha, washiriki wa ndani
kutoka sekta binafsi walipata nafasi ya kufahamu fursa za mikopo
zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Napenda kutoa wito kwa
sekta binafsi kutumia fursa hizo kikamilifu.
9. Mheshimiwa Spika, Bajeti
ya mwaka 2012/13 imelenga kukabiliana na changamoto zinazokabili
uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza fursa za kukuza uchumi,
kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na mfumuko wa bei,
kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi,
kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kuwekeza
katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili
kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika
uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA
MWAKA 2011/12
10. Mheshimiwa Spika,
baada ya utangulizi huo, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji
wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2011/12
uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji wa vipaumbele vya
Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16);
Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
(MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja
wa Misaada Tanzania (MPAMITA); Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010;
Mkakati wa Taifa wa Madeni; pamoja na kuimarisha usimamizi wa kodi na
matumizi ya fedha za Umma.
11. Mheshimiwa Spika,
misingi na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12, pamoja na mambo
mengine, ililenga kukamilisha malengo ya Serikali ya kukabiliana na
changamoto za kupunguza makali ya maisha kwa wananchi; kuendelea
kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya
uwekezaji wa ndani na nje; kuendeleza sekta binafsi ili kupanua wigo
wa kodi; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa; na
kutenga rasilimali na kutekeleza miradi katika maeneo ya kuongeza kasi
ya ukuaji wa uchumi.
12. Mheshimiwa Spika,
maeneo mengine yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya bajeti
hiyo yalikuwa ni: kutekeleza mipango na mikakati maalum ya kuharakisha
ukuaji wa uchumi; kutafuta mikopo ya masharti nafuu na ya kibiashara;
kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya
Binafsi ili kupanua fursa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo; Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; kuhakikisha kwamba maduhuli ya Serikali
yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali;
pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za
huduma za jamii, hususan elimu na afya ambazo zimekuwa na upanuzi
mkubwa wa huduma.
Hatua za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12
Kupunguza Makali ya Maisha
13. Mheshimiwa Spika, katika
utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuchukua
hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi kwa
lengo la kupunguza makali ya maisha kunakotokana na kupanda kwa bei za
bidhaa na huduma. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: kurekebisha namna
ya kukokotoa gharama za mafuta na kutangaza bei elekezi kila mwezi na
kuanzisha utaratibu wa uagizaji mafuta kwa pamoja (bulk procurement).
Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya upandaji wa bei ya mafuta hapa
nchini.
14. Mheshimiwa Spika, Serikali
imetumia shilingi bilioni 296 kutekeleza mpango wa dharura wa
kukabiliana na tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa kutumia
mitambo ya kukodi. Utekelezaji wa jitihada hizi umeongeza megawati 324
kwenye Gridi ya Taifa. Kadhalika, Serikali ilitumia Dola za Marekani
milioni 183 kugharamia ujenzi wa mitambo ya kufua umeme wa megawati 100
kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao umekamilika na uko kwenye hatua
za majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza ambao bado ujenzi
unaendelea.
15. Mheshimiwa Spika, Serikali
imetumia shilingi bilioni 27 kugharamia ununuzi na usambazaji wa tani
120,000 za mahindi katika masoko kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa
chakula kwa baadhi ya maeneo. Aidha, Serikali ilitoa vibali vya kuagiza
sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili
kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya sukari. Kadhalika, Serikali
ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na Benki Kuu kwa Taasisi za
Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58. Vilevile, Serikali
ilipandisha kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinapaswa
kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizi
zimesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
16. Mheshimiwa Spika,
katika kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali imechukua hatua
mbalimbali za kuongeza fursa za ajira. Hatua hizo ni pamoja na:
kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kuwezesha sekta binafsi kukua;
kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika
Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga
Bancorp, na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa mikopo ya muda
mrefu ya ujenzi wa nyumba na makazi. Hatua nyingine zilizochukuliwa na
kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya
barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na kuwezesha wananchi kupitia
programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna Taasisi mbalimbali
ambazo zimechangia kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA, Shirika la
Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Taasisi ndogondogo za Fedha, VICOBA,
Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya mikopo inayosimamiwa na Benki
Kuu. Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri Walimu wa Shule za
Sekondari na Msingi 25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo 4,499 na
Watumishi wa Kada ya Afya 6,916.
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
17. Mheshimiwa Spika,
Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya
Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia kuidhinishwa kwake mwaka 2010. Kupitia
Mpango huu, taratibu na kanuni za mawasilisho na malipo ya kodi na
ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu umeongeza ufanisi
kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika ulipaji wa kodi. Hadi
sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa na walipa kodi wengine
2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya mtandao. Aidha, Serikali
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha mfumo unaounganisha
usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za biashara ili kurahisisha
ulipaji wa kodi. Mfumo huu umeunganisha jumla ya benki 25. Kadhalika,
Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na “NMB mobile” kwa ajili
ya kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.
18. Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea na jitihada za kupunguza urasimu katika utoaji wa
mizigo bandarini kwa kuanzisha utaratibu wa kuwasilisha nyaraka kwa
njia ya mtandao kabla ya mizigo kuwasili. Utaratibu huu umelenga
kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa nyaraka na kupelekea
kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na usafirishaji mizigo nje ya
nchi. Serikali imepunguza vizuizi vya usafirishaji mizigo ndani ya
nchi kutoka 50 vilivyokuwepo kufikia 15, isipokuwa vituo vya mizani na
forodha. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kufanya biashara na
usumbufu wanaopata wafanyabiashara.
Sera za Mapato
19. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuboresha mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi
kwa kuchukua hatua za kiutawala, kisera pamoja na marekebisho ya
viwango vya kodi na sheria.
20. Mheshimiwa Spika,
Serikali ilifanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani, SURA 148 ili kuboresha uzalishaji katika sekta za Kilimo,
Mifugo, Viwanda, Biashara na Utalii. Marekebisho hayo ni pamoja na
kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vipuri vya zana za kilimo;
chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za kutengenezea nyavu za kuvulia samaki;
pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwarejeshea kodi wageni kwa bidhaa
walizonunua nchini wakati wanaondoka.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha
wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya
nyumba za kuishi za Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
isipokuwa kwenye vifaa vya misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima
na shule.
22. Mheshimiwa Spika, Serikali
pia ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa
kufuta kodi ya Zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi ili kuongeza
utoaji wa huduma za usafirishaji wa mazao ya samaki kutokea hapa nchini
badala ya kupitia nchi za jirani. Aidha, marekebisho yalifanyika
katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kwa kupunguza ushuru wa
bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama
za uzalishaji.
23. Mheshimiwa Spika,
Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220 ilifanyiwa marekebisho
kwa kutoa msamaha wa ushuru unaotozwa kwenye mafuta yanayotumika
katika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa
mafuta na gesi ili kupunguza gharama. Aidha, marekebisho
yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya
mwaka 2004 kufuatia kuridhia kwa Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama
kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta za Viwanda,
Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile, marekebisho
yalilenga katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
24. Mheshimiwa Spika,
hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha na kuhakikisha
mashine za kielectroniki – EFD zinatumika ipasavyo; kuimarisha mfumo wa
kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa wateja
na vya kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo ya malipo ya kodi; na
kuboresha mfumo wa uthaminishaji kwa kuimarisha ukaguzi wa hesabu za
walipa kodi.
Mwenendo wa Ukusanyaji Mapato
25. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2011/12, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya
shilingi bilioni 13,525.9 kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumia
kiasi hicho kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Vyanzo vya mapato
vilikuwa kama ifuatavyo: mapato ya ndani yalikadiriwa kufikia kiasi cha
shilingi bilioni 6,775.9; mapato kutoka Serikali za mitaa yalikadiriwa
kufikia kiasi cha shilingi bilioni 350.5; misaada na mikopo ya kibajeti
ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 869.4; misaada na
mikopo ya miradi ya maendeleo na ya kisekta ilikadiriwa kufikia kiasi
cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya
kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1,664.9; na
mikopo ya kulipia dhamana na hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia
kiasi cha shilingi bilioni 810.9.
26. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri, hadi
Aprili 2012 makusanyo yamefikia jumla shilingi bilioni 5,684.5. Kiasi
hiki ni sawa na asilimia 80 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni
7,126.4 kwa mwaka 2011/12.
27. Mheshimiwa Spika,
makusanyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,227.5 ambayo ni sawa na
asilimia 84 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 6,228.8.
Kulingana na mwenendo wa makusanyo ya mapato ya kodi kwa kipindi cha
miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha
2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 6,307.8
na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.
28. Mheshimiwa Spika,
mapato yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi bilioni 451.6 ikiwa ni
asilimia 83 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 547.1 kwa mwaka.
Kutokana na mwenendo huo, Serikali inatarajia hadi Juni 2012 kufikia
lengo.
29. Mheshimiwa Spika, mapato
ya Serikali za Mitaa yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 143, sawa na
asilimia 40.8 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 350.5 kwa mwaka.
Hadi Juni 2012, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni
200 kutokana na chanzo hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la mwaka.
Kutokufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato haya kumechangiwa na
kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada za leseni.
Misaada na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje
30. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/12, Serikali ilikadiria kupata kiasi cha shilingi bilioni
869.4 kama misaada na mikopo ya kibajeti ambapo hadi sasa Serikali
imepokea shilingi bilioni 916.3, ikiwa zaidi kwa shilingi bilioni 46.9.
Ongezeko hili limetokana na baadhi ya wafadhili kutoa fedha zaidi ya
kiwango walichoahidi. Kwa upande wa misaada na mikopo ya miradi ya
maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta, hadi kufikia Aprili 2012
ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya
bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 3,054.1. Upungufu huu umesababishwa
na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi na kuchelewa kupokea
taarifa ya fedha hizi kutoka kwa washirika wa maendeleo na Wizara na
Taasisi zinazotekeleza miradi husika.
Mikopo ya Ndani
31. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali imekopa kiasi cha
shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva
ikiwa ni asilimia 64 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 819.1.
Aidha, Serikali ilipanga kukopa shilingi bilioni 393.4 sawa na asilimia
moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya maendeleo.
Hadi kufikia Aprili 2012, Serikali ilikuwa imekopa shilingi bilioni
232.6 sawa na asilimia 59 ya makadirio ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
32. Mheshimiwa Spika, mwaka
2011/12 Serikali ilikadiria kukopa kiasi cha Dola za Marekani milioni
822, sawa na shilingi bilioni 1,271.6 kama mikopo ya kibiashara. Katika
kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali ilisaini Mkataba wa
mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 310 na Benki ya Standard ya
Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili 2012, jumla ya Dola za Marekani milioni
229 ambazo zilitumika kulipia madeni ya barabara ya mwaka 2010/11.
Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro milioni 61 na Benki ya
HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme
wa megawati 60 Nyakato Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa mkopo
wa Dola za Marekani milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya
Uingereza ambapo Dola za Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa
Mwezi Juni 2012. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150
kitapatikana na kutumika mwaka 2012/13.
33. Mheshimiwa Spika, Serikali
imepata Mshauri Mwelekezi ambaye ataishauri Serikali katika zoezi la
kujiandaa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni
(Sovereign Credit Rating). Maandalizi haya yataiwezesha nchi kufanyiwa
tathmini yanatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika
kwa zoezi hilo kutawapatia wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha
Serikali kupata mikopo yenye masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.
Sera za Matumizi
34. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kutekeleza sera za matumizi
kulingana na upatikanaji wa mapato ya ndani, misaada pamoja na mikopo
ya ndani na nje. Aidha, Serikali iliendelea kuboresha usimamizi na
udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji
wa mishahara, matumizi katika miradi ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo,
ununuzi wa umma na kuendelea kudhibiti malimbikizo ya madeni. Serikali
imeandaa mkakati wa kulipa na kudhibiti madeni yatokanayo na malimbikizo
ya madai ya watumishi; wakandarasi; wazabuni; na madeni mengineyo.
Madeni hayo yatalipwa baada ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
35. Mheshimiwa Spika,
katika jitihada za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, Serikali
iliendelea kutekeleza programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za
umma katika Serikali Kuu na Serikali za mitaa. Katika utekelezaji wa
programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS katika Halmashauri 133.
Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo ya kibenki - TISS
kwa watumishi wa kada ya Uhasibu katika mikoa 20, Hazina ndogo zote,
Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika.
Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa Wahasibu wa Wizara, Idara, Mikoa
na Balozi zetu 32 katika kuandaa Hesabu za Serikali kwa viwango vya
Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).
36. Mheshimiwa Spika,
kutokana na maboresho hayo, usimamizi wa fedha katika Wizara, Idara,
Taasisi, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa unaendelea kuimarika.
Hali hii inajidhiirisha katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/11 ambapo Hati safi za ukaguzi kwa
Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa zimeongezeka kutoka asilimia 71
hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye shaka zimepungua kutoka asilimia 26
mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 15 kwa mwaka wa fedha 2010/11 na
hapakuwepo na Hati zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009/10 ambapo
Hati hizo zilitolewa kwa Taasisi mbili.
37. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa Balozi zetu Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 71
mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 85 mwaka 2010/11 na hapakuwepo na Hati
zisizoridhisha katika mwaka 2010/11. Aidha, kwenye Mamlaka za
Serikali za Mitaa Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka wa
fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka 2010/11 na Hati zenye shaka
zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 56
mwaka 2010/11.
38. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/12, Serikali imefungua akaunti sita kwa kila
Halmashauri kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu yao. Akaunti hizo ni za
Mapato; Amana; Matumizi ya kawaida; Mishahara; Maendeleo; na Mfuko wa
Barabara. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uendeshaji, urasimu
wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za matumizi, ulimbikizaji wa fedha
kwenye akaunti bila kutumika kwa muda mrefu na kudhibiti fedha
zisitumike katika shughuli ambazo hazikuidhinishwa.
Mwenendo wa Matumizi
39. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa matumizi, Serikali ilikadiria kutumia kiasi cha shilingi
bilioni 13,525.9 katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Mgawanyo wa
matumizi ya Serikali katika kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo; kiasi
cha shilingi bilioni 8,600.3 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na shilingi bilioni 4,925.6 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo.
Matumizi ya kawaida
40. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 matumizi ya kawaida yamefikia
shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia 85.5 ya makadirio ya mwaka
kama ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati ya kiasi hicho, malipo ya
mishahara ya watumishi wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya
Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi
bilioni 2,760.5 sawa na asilimia 84.4 ya lengo la mwaka la shilingi
bilioni 3,270.3. Malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa
shilingi bilioni 316.1 sawa na asilimia 102.4 ya makadirio ya shilingi
bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya mikopo ya nje yalikuwa shilingi
bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya makadirio kwa mwaka. Serikali
ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali
za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Serikali imeendelea
kutoa kipaumbele katika kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka
malimbikizo ya riba.
41. Mheshimiwa Spika, matumizi
mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na
Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,384.9 ikiwa ni asilimia 72.8 ya
makadirio ya shilingi bilioni 3,275.1 kwa mwaka. Kati ya matumizi
mengineyo, kiasi cha shilingi bilioni 284.1 zilitumika kwa ajili ya
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni asilimia 89 ya bajeti ya
mwaka ya shilingi bilioni 317.4, na hivyo kunufaisha jumla ya wanafunzi
93,176. Kadhalika, Serikali ililipa kiasi cha shilingi bilioni 44.0 za
madai ya walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyohakikiwa na
Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Matumizi ya Maendeleo
42. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 2,657.2
ziligharamia miradi ya maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka
ya kutumia shilingi bilioni 4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi
bilioni 1,201.6 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni
1,871.5 sawa na asilimia 64.2. Upungufu huu umetokana na kuchelewa
kupatikana kwa wakati kwa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara.
Jumla ya shilingi bilioni 663.8 ziligharamia miradi ya miundombinu, kati
ya hizo shilingi bilioni 296 zilitumika kwenye miradi ya umeme na
shilingi bilioni 367.8 kwenye miradi ya barabara. Matumizi ya maendeleo
yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa shilingi bilioni 1,450.4
ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 3,054.1 sawa na asilimia
47.
Vitambulisho vya Taifa na Anwani za Makazi
43. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea na azma yake ya kutekeleza mradi wa Vitambulisho vya Taifa
ambavyo vitasaidia, pamoja na mambo mengine, kurahisisha upatikanaji wa
huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha. Mradi huu
unaenda sambamba na uanzishwaji wa anwani za makazi. Vitambulisho hivyo
vitaanza kutolewa katika robo ya kwanza ya mwaka 2012/13 kwa Zanzibar
na Mkoa wa Dar es Salaam.
Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali ya Umaskini
44. Mheshimiwa Spika,
kwa kutambua umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi Serikali imeendelea
kugharamia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi, ambapo utekelezaji
umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali imetumia shilingi bilioni 23.6
kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa hiyo imepangwa kufanyika
tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali iliendelea kugharamia utafiti
wa mapato na matumizi katika kaya. Utafiti huu ulianza mwezi Oktoba
2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2012 na matokeo
yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti huu utatoa picha halisi
ya hali ya umaskini, hususan wa kipato tangu mwaka 2007 hadi mwaka
2012. Hii itasaidia kutambua mwenendo wa umaskini wa kipato na sababu
zilizopelekea mwenendo huo.
Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
45. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka 2011/12, serikali iliendelea kutekeleza MKUKUTA
awamu ya pili unaojielekeza katika maeneo ya kukuza uchumi na kupunguza
umaskini wa kipato, kuboresha maisha na ustawi wa jamii, na utawala
bora na uwajibikaji sambamba na Melengo ya Maendeleo ya Milenia. Ili
kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo, sekta kadhaa huchangia
katika utekelezaji kupitia sera, mikakati na mipango ya kisekta. Kwa
mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II unahitaji ushirikiano wa sekta
mbalimbali za uchumi katika hatua ya upangaji na utekelezaji.
46. Mheshimiwa Spika,
MKUKUTA ni mkakati unaoziweka pamoja juhudi za Serikali na wadau
mbalimbali katika kupambana na umaskini. Aidha, umaskini ni suala pana
linalojumuisha umaskini wa kipato na usio wa kipato. Ni kweli kuwa
umaskini wa kipato umekuwa ukipungua kwa kasi ndogo. Hata hivyo,
Serikali inachukua hatua mbalimbali za kupunguza umaskini kwa kujenga
mazingira bora ili wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za
uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu, afya, miundombinu na
sekta ya fedha.
47. Mheshimiwa Spika,
pamoja na changamoto zilizojitokeza, hususan mtikisiko wa uchumi
duniani, uchumi uliendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha
ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2011, kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa
na asilimia 7.0 mwaka 2010. Aidha, pato la wastani la Mtanzania
limeongezeka kutoka shilingi 770,464 kwa mwaka 2010 hadi shilingi
869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani, ongezeko hili limeongeza uwezo wa
wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na nyumba bora, simu za
mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.
48. Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za huduma ya jamii
kwa lengo la kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Matokeo ya
utekelezaji wa programu hizo zinaonesha mabadiliko chanya. Katika sekta
ya elimu, viwango vya uandikishaji na kumaliza katika ngazi zote za
elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha uandikishwaji katika elimu ya
msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika elimu ya sekondari ni asilimia
35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa mtoto na mama zinaendelea
kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango wa afya ya mtoto na mama.
Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeendelea
kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu ya sekta ya maji
iliyoanza mwaka 2007.
49. Mheshimiwa Spika,
katika kudumisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali iliendelea
kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha sekta ya sheria
kwa kuongeza idadi ya mahakimu wa Mahakama za mwanzo; kuimarisha
mfumo wa sheria na haki za binadamu; kuhamasisha umma kuhusu haki za
binadamu na wajibu wa jamii; na kushiriki katika mpango wa nchi za
Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala ya utawala bora. Aidha,
Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma,
kwa kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Sekta ya Fedha
50. Mheshimiwa Spika,
Serikali imefanya mageuzi mbalimbali katika sekta ya fedha ili
kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na
kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio makubwa.Hadi
kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka na kufikia 49
kutoka benki 43 Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za mkononi
zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka 2011
kutoka 10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo za
kifedha zimefikia 150 mwaka 2011.
51. Mheshimiwa Spika, Serikali
iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo kupitia dirisha la Kilimo lililopo
katika Benki ya Rasilimali Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya
mikopo 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya
mikopo hiyo, 42 ni ya SACCOS, 32 ni kwa ajili ya makampuni na 7 kwa
Taasisi ndogondogo za fedha (MFIs). Mikopo iliyotolewa kwa MFIs na
SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi ya wakulima wadogo wadogo
vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya mtaji
wa Benki ya Kilimo.
52. Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea na utekelezaji wa programu ya mageuzi na maboresho
ya Ushirika nchini ili kuimarisha vyama vikuu vya ushirika na
kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi hususan
waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na
Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama 5,314 mwaka
2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 5.7 na
kufikia wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889 mwaka 2010. Aidha,
Hisa, Akiba na Amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni
236.8 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 399.0 mwaka 2011, sawa na
ongezeko la asilimia 68.5. Mikopo iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka
kutoka shilingi bilioni 539.2 mwaka 2010 hadi shilingi bilioni 627.2
mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 16.3.
53. Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia
21.9 ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili linaenda
sambamba na kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani kwenye benki
pamoja na kupungua kwa ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni kwenye
benki. Sehemu kubwa ya mikopo hii ilielekezwa katika shughuli binafsi
asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9; uzalishaji bidhaa viwandani
asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na mawasiliano asilimia
7.9.
54. Mheshimiwa Spika,
ili kuongeza upatikanaji wa mikopo, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi
kwa ajili ya kuanzisha taasisi ya kuratibu taarifa za wakopaji (Credit
Rerefence Bureau) na mfumo wa kuhifadhi taarifa za wakopaji (Credit
Reference Databank). Mshauri mwelekezi ameanza zoezi la kuweka mitambo
na kutoa mafunzo kwa watumiaji. Aidha, Serikali imeboresha mazingira ya
upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kati kwa ajili ya nyumba, Kilimo
na uwekezaji ambapo kanuni za taasisi za fedha za maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Machi 2012.
55. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/12, Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya
Hifadhi ya Jamii kwa kufanya tathmini ya uwekezaji wa mifuko, uhai wa
mifuko, pamoja na kuandaa mwongozo za uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha,
Serikali imefanya marekebisho ya Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka
ya Usimamiaji wa Shughuli za Mifuko (SSRA) ili kuboresha usimamizi wa
mifuko hiyo.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
56. Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu lilipitisha sheria mpya ya Ubia kati ya Sekta ya
Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 ili kutoa fursa kwa sekta binafsi
kushiriki katika ujenzi wa miundombinu na kuiendesha kwa lengo la kutoa
huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa wananchi. Katika mwaka 2011/12,
Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa Sera ya Ubia ikiwa ni
pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila Wizara na kuandaa miongozo
itakayotumika kuchambua na kuidhinisha miradi ya Ubia kwa mujibu wa
sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za awali kubaini miradi inayoweza
kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa mujibu wa sheria.
57. Mheshimiwa Spika,
dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inatekelezwa kwa
kutumia sheria mbili – Sheria ya Ubia ya mwaka 2010 na Sheria ya
Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 iliyorekebishwa mwaka 2011. Sababu za
kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na mambo mengine ni
kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali kupata Wabia makini
wa uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi. Aidha, katika
mwaka 2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya Ununuzi wa
Umma ambazo zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya Ubia ambayo
inawezesha kupata Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi husika.
Serikali itahakikisha kanuni na taratibu zote za kuidhinisha na
kusimamia miradi ya ubia zinazingatiwa.
58. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali itatoa mafunzo ya uelewa wa
dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi kwa watumishi wa
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi za Serikali, na Halmashauri zote.
Aidha, Serikali itachagua miradi michache ya kuanza nayo ili kupata
uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo. Maeneo tunayotarajia kuanza nayo ni
barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, maji pamoja na ujenzi wa
ofisi.
59. Mheshimiwa Spika,
Napenda kutumia fursa hii kuziomba Wizara, Idara zinazojitegemea,
Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhamasisha Sekta
Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia
taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria.
Usimamizi wa Deni la Taifa
60. Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza azma yake ya kuboresha miundombinu ya kimkakati,
Serikali imeendelea kukopa kutoka nje na ndani ya nchi ili kugharamia
miradi mbali mbali ya maendeleo. Hadi mwishoni mwa Machi 2012, deni la
taifa lilikuwa shilingi bilioni 20,276.6 ikilinganishwa na deni la
shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011 ikiwa ni sawa na ongezeko la
asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15.306.9 zilikuwa ni deni
la nje na shilingi bilioni 4,969.7 ni deni la ndani. Kati ya kiasi cha
deni la nje, shilingi bilioni 12,342.5 zilikuwa ni deni la umma na
kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni 2,964.4 ni deni la sekta
binafsi. Aidha, hadi kufikia Machi 2012, deni la ndani la Serikali
lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni
4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko la asilimia 10.5. Sababu
kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya
kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa dhamana za muda mfupi za
Serikali kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei katika uchumi na kushuka
kwa thamani ya shilingi kuliongeza deni la nje.
61. Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa vizuri, mwezi
Februari, 2012, Serikali ilifanya tathmini ya uhimilivu wa deni (Debt
Sustainability Analysis) likijumuisha dhamana zinazotolewa na Serikali
kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma ambapo matokeo ya tathmini hiyo
yanaonesha kuwa Deni la Taifa linahimilika.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
62. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma yanatekeleza majukumu
yao, Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka 2012 unaoelekeza Wizara mama
na Bodi za Wakurugenzi kuingia katika mikataba ya utendaji, Waraka huo
umeanza kutumika Januari, 2012. Aidha, ukaguzi wa kiutendaji
(Management Audit) katika Taasisi za Serikali umefanyika kwa baadhi ya
Taasisi na Mashirika ya umma kwa kuangalia uzingatiaji wa kanuni,
Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ikiwa ni pamoja
na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya fedha na taratibu za
ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha uendeshaji wa
Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika, Serikali imefanya uhakiki
wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya hayo, mashirika 41
yalikutwa yanajiendesha kwa faida, mashirika 66 yanajiendesha kwa
hasara na mashirika 63 yalikuwa muflisi. Kwa yale ambayo yanaendeshwa
kwa hasara yatawekwa chini ya mfilisi kwa lengo la kuyachambua na
kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa yale yaliyokuwa muflisi
hatua za kuyafilisi zinaendelea.
III. BAJETI YA MWAKA 2012/13
63. Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya mwaka 2012/13 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye
Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13; Awamu ya Pili ya Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo
ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na program za
maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025.
64. Mheshimiwa Spika, pamoja
na miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia pia changamoto zilizojitokeza
wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Changamoto hizo ni
pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika; kupanda kwa bei ya mafuta
katika soko la Dunia; uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo; kupanda
kwa bei za bidhaa na huduma; kutopatikana kwa wakati fedha za
kugharamia miradi ya maendeleo kulikosababishwa na masharti magumu na
urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na kuongezeka kwa malimbikizo ya
madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi na watumishi. Mambo
mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo wa uchumi
wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali imepanga
hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo kama
nitakavyoeleza hapo baadae.
Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13
65. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13, imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:
i. Kukuza Pato halisi la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;
ii. Kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari;
iii. Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha;
iv. Kuongezeka
kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia
18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka
2011/12;
v. Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;
vi. Kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha;
vii. Kukua
kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la
Taifa mwishoni mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko
wa bei;
viii. Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi
minne na nusu;
ix. Kuimarisha
utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kupanua
fursa za kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
x. Kuboresha mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;
xi. Kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
xii. Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na
xiii. Kujenga
uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja
na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.
Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2012/13
66. Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii ifuatayo:
i. Kuendelea kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;
ii. Kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
iii. Kuimarika kwa utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;
iv. Kuendelea kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;
v. Kuendelea kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;
vi. Kuendelea kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na
vii. Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za uwekezaji.
Sera za Mapato
67. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya
ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mapato yatokanayo
na kodi na yasiyotokana na kodi; na kupanua wigo wa makusanyo. Aidha,
Serikali itaendelea kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na
kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa
matumizi ya kawaida kwa kutumia mapato ya ndani. Sera za mapato
zitakazozingatiwa kwenye Bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na;
i. kuboresha
mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa
kupitia upya mfumo wa utoaji stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha
viwango vya kubakiza maduhuli kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;
ii. kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
iii. kuendelea
kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma zinazokusanya
maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
iv. kuendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
v. Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
vi. kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na
vii. Kujenga
uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wakala wa
Ukaguzi wa Madini ili kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya
madini, gesi na petroli.
Hatua za Kuboresha Uzalishaji na Huduma
68. Mheshimiwa Spika, Serikali
imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa
wabunge kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta
za Uvuvi, Viwanda, Kilimo, Mifugo na Utalii. Hatua ambazo Serikali
imepanga kuchukuwa ni pamoja na:
i. Kupitia upya vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za ndani vikiwemo viwanda vya nguo na mafuta ya kula;
ii. Kutafuta
utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya mashine na mitambo
inayosamehewa kodi ili kuondoa usumbufu wanaoupata waagizaji;
iii. Kupitia upya viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na kupunguzwa;
iv. Kupitia
upya maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Skills
Development Levy) na Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence). Kwa
kufanya hivyo, Serikali inalenga katika kupanua wigo wa kodi,
kuwapunguzia mzigo waajiri na kupanua ajira hapa nchini. Aidha, mapitio
ya Leseni za Magari yatazingatia kurejea madhumuni ya kuanzishwa kwa
leseni hiyo; na
v. Kufanya mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa “Best Practice”.
69. Mheshimiwa Spika,
Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya ndani kwa kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM – TAMISEMI kwa
kushirikiana na Shirika la Misaada na Utaalamu la Ujerumani – GIZ
watakamilisha na kusambaza kwenye Halmashauri mfumo wa kompyuta wa
utunzaji kumbukumbu za mali na majengo (Integrated Property Rating
Information Management System - IPRIMS) ili kuboresha ukusanyaji wa
mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote
pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka msukumo
utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja na
mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na
kuwaletea maendeleo endelevu.
70. Mheshimiwa Spika,
kwa kuzingatia sera za mapato zilizoainishwa hapo juu, Serikali
inalenga kukusanya mapato ya ndani (bila kujumuisha Halmashauri)
shilingi bilioni 8,714.7 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Kati ya
kiwango hicho, mapato ya kodi shilingi bilioni 7,080.1 na mapato yasiyo
ya kodi shilingi bilioni 644.6. Mapato yanayotokana na vyanzo vya
Halmashauri shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la
Taifa.
Mikopo ya Ndani
71. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kukopa katika soko la ndani
la fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipia
hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva.
Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia kukopa kiasi cha shilingi
bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni kwa
ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni
1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za
Serikali za muda mfupi zinazoiva. Kiwango hiki kimezingatia viashiria
vya kiuchumi pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zinaendelea
kutoa mikopo kwa Sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Misaada na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu
72. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ili
kuhakikisha Misaada na mikopo inapatikana kwa wakati na kuchangia katika
utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Katika bajeti ya mwaka 2012/13
serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 3,156.7 kutokana
na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya fedha hizo, Misaada
na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa na Dola za Marekani
milioni 495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ikijumuisha mifuko ya kisekta inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,314.2.
73. Mheshimiwa Spika,
pamoja na misukosuko ya kiuchumi na majanga ya kiasili iliyozikumba
nchi Wahisani, bado zimeendelea kutoa misaada na mikopo kwa ajili ya
maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua washirika wetu wa maendeleo
ambao ni: Uingereza, Norway, Canada, Marekani, Uholanzi, Ubelgiji,
China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Japani, Korea ya Kusini,
Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi, India, Italia, Benki ya Dunia, Benki
ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha
la Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi
Fund, na Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru Sana.
Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
74. Mheshimiwa Spika,
sera ya Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka mashirika na nchi
wahisani kwa ajili ya kugharamia Bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo,
kwa kuzingaita mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu kwa
mwaka 2012/13, Serikali inatarajia kupata kutoka nje mikopo yenye
masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni 1,254.1 sawa na Dola
za Marekani milioni 749. Fedha hizi zitatumika kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo
wa mwaka 2012/13 ikijumuisha mchango wa Serikali (counterpart fund)
katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi
wa maji wa Ruvu chini na ujenzi wa barabara. Uamuzi wa kuendelea kukopa
kwa masharti nafuu na ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la
Taifa uliopo.
Sera za Matumizi
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
i. Matumizi yataendelea kuzingatia mapato halisi yanayopatikana;
ii. Nakisi ya bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa, ikijumuisha ruzuku;
iii. Mafungu yataendea kuzingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
iv. Maafisa Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha na ya Ununuzi wa Umma; na
v. Serikali inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la kuyahakiki na kuyapangia utaratibu wa kuyalipa.
Matumizi ya Kawaida
76. Mheshimiwa Spika, Sera
za matumizi ya kawaida kwa mwaka 2012/13 zinalenga pamoja na mambo
mengine katika kugharamia mishahara; madeni ya mikopo ya ndani na nje;
uboreshaji wa huduma za kiuchumi na maendeleo ya jamii; mikopo ya
wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya shule za msingi na sekondari;
ununuzi na usambazaji wa dawa; mahitaji ya Tume ya Kuratibu Mabadiliko
ya Katiba; matengenezo ya mali ya Serikali; ununuzi wa chakula cha
hifadhi; mahitaji ya kawaida kwenye miradi iliyokamilika; pamoja na
kuendelea kulipa madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni.
77. Mheshimiwa Spika, ili
kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu,
kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira, Serikali imetenga fedha
katika maeneo yafuatayo: Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Benki ya
Rasilimali; shilingi bilioni 40 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na
hivyo kufikisha mtaji wa shilingi bilioni 100. Aidha, shilingi bilioni
7.5 zimetengwa kwa ajili ya kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
kwa mujibu wa sheria, ambapo katika awamu ya kwanza vijana 5,000
wanatarajiwa kujiunga. Vilevile, Serikali imetenga jumla ya shilingi
bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni Mikoa, Wilaya na Halmashauri
kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.
Matumizi ya Maendeleo
78. Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa kwa mwaka 2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu Mhe. Stephen Masatu Wasira, aliainisha miradi ya kitaifa ya
kimkakati pamoja na miradi katika maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi.
Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:
a) Miundombinu
i. umeme
- mkazo utawekwa katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa kuongeza
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji ambapo jumla shilingi bilioni
498.9 zimetengwa kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa
ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo
kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani milioni
1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.
ii. usafirishaji na uchukuzi – uimarishaji
wa reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni.
Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na
barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na
majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa
viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya
shilingi bilioni 1,382.9 zimetengwa katika eneo hili.
iii maji safi na salama - kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini. Kiasi cha shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.
iv Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
–
kuimarisha mawasiliano kwa kutumia TEHAMA ili kuboresha upatikanaji wa
huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko
ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa mapato; huduma za afya; elimu;
huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa katika
eneo hili.
b) Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
79. Mheshimiwa Spika,
kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itawekeza katika kilimo
cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na
Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa
kilimo na kukuza kilimo cha misitu. Hii ni pamoja na kuendeleza
shughuli za ufugaji na uvuvi ili ziwe na tija kwa kuboresha mazingira ya
uwekezaji; kwa kufanya hivyo kutapunguza umaskini wa kipato.
80. Mheshimiwa Spika, katika
kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama
wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza
kwa kuhakikisha kwamba nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa;
kuhakikisha kwamba walengwa wanapata pembejeo kwa wakati; Maafisa ugani
kutakiwa kuwa na mashamba yao ya mfano (mashamba darasa) ili
kuwaelimisha wakulima kilimo cha kisasa; kuongeza msukumo kwenye kilimo
cha umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya shughuli zao za kilimo
katika misimu yote badala ya kutegemea mvua;Kuimarisha masoko ya mazao
kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo imeshaanza shughuli zake; na
Mikoa kutakiwa kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na
kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje. Kiasi cha
shilingi bilioni 192.2 kimetengwa katika eneo hili.
c) Maendeleo ya Viwanda
81. Mheshimiwa Spika,
Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi
zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda
vikubwa vya saruji; na viwanda vya eletroniki na TEHAMA pamoja na
kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji
mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta
binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha viwanda
vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi bilioni 128.4 zimetengwa katika
eneo hili.
d) Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii
82. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga kuboresha viwango vya
elimu katika ngazi zote hususan katika maeneo ya utafiti, ufundi
stadi, afya; sayansi na ujuzi maalum kuhusu madini, gesi, urani, chuma
na mafuta; hatua hii inajumuisha ukarabati wa maabara na upatikanaji wa
vifaa vya maabara. Shilingi bilioni 84.1 zimetengwa katika eneo hili.
e) Utalii
83. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa
ni pamoja na kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na
kutoa mafunzo ya utalii, kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha
vyuo vya utalii.
Huduma za Fedha
84. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kifedha hususan mifumo ya
kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na benki za kijamii ili
kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na
uzalishaji. Kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya
kuimarisha mtaji wa Benki ya Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Aidha, Wizara ya Fedha itaendelea
kusimamia maendeleo ya Taasisi za fedha zinazojihusisha na utoaji wa
mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha hili kitengo kilichopo cha
maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa idara kamili.
Usimamizi wa Fedha za Umma
85. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya nne ya Programu ya Maboresho
ya Usimamizi wa Fedha za Umma na kuhakikisha kwamba Sheria ya Fedha za
Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma zinafuatwa kikamilifu ili kuongeza
uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Umma. Maeneo yanayozingatiwa
kwenye programu hiyo ni pamoja na: kuendelea kuboresha Mtandao wa malipo
(IFMS) ili kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma kwa
Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa; utoaji wa mafunzo ya
ulipaji kwa mfumo wa malipo wa kibenki kwa watumishi wa Ofisi za Bunge,
Sekretarieti za Mikoa, Idara ya Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu
-TAMISEMI na Ofisi za Hazina ndogo Mikoa yote. Aidha, Serikali
itaendelea kutoa mafunzo ya kuandaa hesabu kwa kutumia viwango vya
uhasibu vya kimataifa ili kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za
Umma; kuijengea uwezo Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali
katika kuhakikisha kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma
zinazingatiwa ipasavyo; na kujenga uwezo wa Serikali Kuu, Mikoa na
Halmashauri katika eneo la uandaaji wa mipango na bajeti, ukusanyaji wa
mapato, usimamizi wa raslimali, uboreshaji wa mawasiliano na utoaji wa
taarifa za utekelezaji wa bajeti.
86. Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuboresha utaratibu wa kupeleka fedha kwenye
Halmashauri na kutoa taarifa mapema kuhusu matumizi ya fedha
zilizopelekwa. Aidha, fedha zote zitakazovuka mwaka bila kutumika
zitatolewa taarifa kwenye vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la
Madiwani ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.
87. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/13, Serikali itaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi
kwenye Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote ili
kuondoa watumishi wasiostahili kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya
watumishi wa Serikali. Aidha, mamlaka za ajira na maafisa masuuli
wanaelekezwa kusitisha malipo kwa watumishi walioacha au kuachishwa
kazi, kustaafu, kufariki au likizo bila malipo ili kuzuia upotevu wa
fedha za umma.
88. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kutilia mkazo wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za
umma katika Wizara, Taasisi, Wakala, Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa ili kuthibitisha endapo fedha zinazopangwa kukusanywa zinapatikana
na pia fedha zinazotumwa kutoka Hazina zinafika na kutekeleza shughuli
zilizoidhinishwa. Serikali itaboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi
wa fedha za umma zinazokusanywa au kupelekwa kwenye Mikoa na
Halmashauri nchini.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
89. Mheshimiwa Spika, katika kukabliana na changamoto za usimamizi wa Mashirika ya Umma, Serikali inaendelea
kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanya mapitio ya Sheria za
Msajili wa Hazina ambazo ni “Treasury Registrar Ordinance” ya mwaka
1958 na “Treasury Registrar Powers and Functions” SURA 370 ya mwaka
2000 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 ili kuwa na Sheria moja. Lengo
la hatua hiyo ni kuimarisha ofisi kwa kuipa nguvu zaidi za kisheria
kuweza kusimamia ipasavyo utendaji wa Mashirika ya Umma pamoja na
Taasisi ili kuongeza tija.
Kukabiliana na Mfumuko wa Bei
90. Mheshimiwa Spika,
uchumi wetu unakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo mfumuko wa bei
ambao kwa wastani umeshuka kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi
asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012. Kichocheo kikubwa cha mfumuko wa bei
ni kupanda kwa bei za umeme, mafuta na vyakula hususan mchele na
sukari. Kwa mfano kwa mwezi Aprili 2012, chakula kimechangia asilimia
24.7 wakati umeme na mafuta vimechangia kwa asilimia 24.9. Mfumuko wa
bei ambao haujumuishi chakula na nishati bado uko kwenye tarakimu moja
ambayo ni asilimia 8.8. Hivyo, jitihada za Serikali zitaelekezwa katika
kukabiliana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo.
91. Mheshimiwa Spika,
hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali
vya uagizaji wa sukari na mchele kutoka nje na kuendelea kuimarisha
Hifadhi ya Chakula ya Taifa. Aidha, Serikali itawekeza katika kilimo
cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Kilombero, Wami, Kagera na
Malagarasi pamoja na miradi ya kilimo cha umwagiliaji. Hatua nyingine
ni pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na
masoko; kuimarisha mfumo wa masoko kwenye maeneo yanayozalisha chakula
kwa wingi hususan mikoa ya nyanda za juu kusini na mipakani. Kwa upande
wa nishati ya umeme, Serikali itaendeleza vyanzo mbadala vya umeme
kama vile umeme wa gesi, nguvu za jua, upepo, miwa ili kupunguza
matumizi ya mafuta kama chanzo cha nishati.
Kupanua fursa za Ajira
92. Mheshimiwa Spika, ili
kuongeza ajira hasa kwa vijana, Serikali itaendelea kupanua huduma za
fedha ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Kilimo na kuongeza mitaji
kwa Benki za Rasilimali, Wanawake, Posta na Twiga Bancorp. Hatua
nyingine zitakazochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni pamoja na
kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo na mawasiliano. Aidha,
sekta binafsi itahamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki na
Maendeleo ya Afrika kupitia Dirisha la kuendeleza sekta binafsi.
Kadhalika, Serikali itaajiri watumishi 71,756 katika sekta za Elimu,
Afya, Kilimo na kada nyingine.
IV. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:
93. Mheshimiwa Spika,
katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imefanya maboresho katika
mfumo wa kodi kwa nia ya kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya
ndani. Maboresho yaliyofanywa ni pamoja na marekebisho ya sheria za
kodi, kanuni na taratibu za usimamiaji wa kodi. Aidha hatua hizi
zimechangia katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya
kodi. Hata hivyo kuna changamoto katika kuhuisha mapato ya ndani ili
kupunguza utegemezi wa bajeti hatua kwa hatua. Kwa
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
94. Mheshimiwa Spika,
ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mfumo wa kodi,
napendekeza kufanya maboresho katika sheria mbalimbali za kodi kama
ifuatavyo:-
a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b) Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d) Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
e) Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
f) Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
g) Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
h) Misamaha ya Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs);
i) Marekebisho mengine katika baadhi ya sheria za kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha; na
j) Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
k) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
A. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
95. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo: -
(i) Kuanzisha
kiwango kipya (VAT Rate) cha asilimia 10 cha Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwa baadhi ya watu, taasisi na mashirika yanayopata unafuu wa
kodi hiyo
(special
relief). Kwa mantiki hiyo, wale waliokuwa hawalipi kodi hiyo kuanzia
sasa watalipa asilimia 10. Hatua hii itazihusu Kampuni binafsi, watu
binafsi na Kampuni zitakazopewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji Tanzania
isipokuwa zile zenye vyeti hivyo kwa sasa. Aidha, itahusu pia Mashirika
yasiyo ya Kiserikali isipokuwa yale yaliyopewa msamaha wa kodi pale
yanapotoa huduma ya chakula, dawa baridi na vifaa kama vile sabuni
ambavyo vinatolewa msaada kwenye vituo mahsusi vya kulelea watoto yatima
na shule;
(ii) Kurekebisha
kifungu cha 19 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani ili kuongeza Mashine za Elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi
(Electronic Fiscal Devices - “EFDs”) katika orodha ya vifaa vinavyopata
msamaha wa kodi hiyo. Lengo ni kuwawezesha walipa kodi kupata vifaa
hivi kwa gharama nafuu na kuhamasisha matumizi yake kwa kuwa ni muhimu
katika kutoa stakabadhi za mauzo ya bidhaa na huduma;
(iii) Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya
gesi iliyoshindiliwa na gesi ya mabomba (Compressed Natural Gas and
Piped Natural Gas). Msamaha wa kodi unatolewa ili kuhamasisha matumizi
ya gesi katika magari, kupikia, nyumbani, taasisi na viwandani. Aidha,
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) litawajibika kuhakiki vifaa
hivyo ili kuhakikisha kwamba vitatumika kujenga miundo mbinu ya gesi.
96. Mheshimiwa Spika, Mitambo na vifaa vya kujenga miundombinu ya gesi asili vinavyoombewa msamaha wa kodi ni kama ifuatavyo:-
- CNG vehicles conversion kits – vifaa vinavyoongezewa kwenye magari yaweze kutembea kwa kutumia nishati ya gesi asili;
- High pressure vessels (CNG and LPG cylinders) – mitungi maalumu ya kutunzia gesi asili iliyoshindiliwa na gesi ya LPG;
- Natural Gas Compression plants equipments – vifaa kwa ajili ya mitambo ya kushindilia gesi asili;
- Natural gas pipes (Transportation and Distribution pipes) – mabomba maalum ya kusafirishia na kusambazia gesi asili;
- CNG storage cascades – mitungi maalum ya pamoja ya kusafirishia na kuhifadhia gesi asili iliyoshindiliwa;
- CNG transportation trailers - magari na matela ya kusafirishia gesi asili iliyoshindiliwa;
- Natural gas metering equipments – mita za kupimia kiasi cha gesi asili;
- Pipeline fittings and valves – vifaa vya kuunganishia mabomba na kuruhusu/kuzuia gesi kupita;
- CNG Refueling/filling equipment – vifaa vya kujazia gesi asili kwenye magari;
- PNG/CNG accessories – vifaa vidogo vidogo vinavyotumika katika ujenzi wa mabomba ya gesi asili na katika mitambo ya kushindilia gesi asili;
- Gas Receiving Unit – vifaa vya kupokelea gesi ya mabomba;
- Condensate Stabilizer – vifaa vya mifumo ya kuimarisha uhifadhi wa condensate;
- Flare Gas System – vifaa kwa ajili ya mifumo ya kuunguza gesi kwa ajili ya usalama;
- Air & Nitrogen System – vifaa vya mifumo ya hewa na ya Nitrogen;
- Condensate Tanks and Loading Facility – matanki ya kuhifadhia condensate na vifaa vya kupakilia;
- System piping on piperack – mifumo ya kubeba mabomba ya gesi asili;
- Instrumentation – vifaa vya umeme na udhibiti kwenye mifumo ya gesi asili.
- Majiko yaliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya gesi pekee.
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 22,565.1
B. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
97. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
- Kuweka kiwango cha chini cha mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo cha shilingi 3,000,000 kisichotozwa kodi na kurekebisha matabaka (bands) ya walipa kodi. Lengo la hatua hii ni kulinda mapato halisi ya Serikali na kuhakikisha kwamba wenye mapato ya chini ya kiwango cha kutozwa kodi cha shilingi 3,000,000 hawatozwi kodi chini ya mfumo wa kukadiria kodi Walipa kodi wadogo “Presumptive Scheme” kama ilivyo kwenye mapato yatokanayo na ajira. Hivi sasa Wafanyabiashara wenye kipato hicho wanatozwa Sh. 35,000.
Viwango vya sasa na vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
Viwango vya sasa
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
| ||
(i)
|
Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
|
Shs. 35,000/=
|
1.1% ya mauzo
| |
(ii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/= na yasiyozidi Shs. 7,000,000/=
|
Shs. 95,000/=
|
Shs. 33,000/= + 1.3% ya mauzo yanayozidi Shs. 3,000,000/=
| |
(iii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 7,000,000/= na yasiyozidi Shs. 14,000,000/=
|
Shs. 291,000/=
|
Shs. 85,000/= + 2.5% ya mauzo yanayozidi 7,000,000/=
| |
(iv)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/= na yasiyozidi Shs. 20,000,000/=
|
Shs. 520,000/=
|
Shs. 260,000/= + 3.3% ya mauzo yanayozidi Shs. 14,000,000/=
| |
Viwango vinavyopendekezwa
| ||||
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
| ||
(i)
|
Kwa mauzo yasiyozidi Shs. 3,000,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
Asilimia sifuri (0%)
| |
(ii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs 3,000,000/= na yasiyozidi Shs 7,500,000/=
|
Shs. 100,000/=
|
2% ya mauzo yanayozidi
Shs 3,000,000/=
| |
(iii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/= na yasiyozidi Shs 11,500,000/=
|
Shs. 212,000/=
|
Shs. 90,000/= plus 2.5% ya mauzo yanayozidi Shs 7,500,000/=
| |
(iv)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/= na yasiyozidi Shs 16,000,000/=
|
Shs. 364,000/=
|
Shs. 190,000/= + 3.0% ya mauzo yanayozidi Shs 11,500,000/=
| |
(v)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/= na yasiyozidi Shs 20,000,000/=
|
Shs. 575,000/=
|
Shs. 325,000/= + 3.5% ya mauzo yanayozidi Shs 16,000,000/=
| |
- Kutoza Kodi ya Zuio ya asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na riba inayotolewa na mabenki kwa wafanyabiashara ambao si wakaazi (non-residents). Lengo ni kuweka usawa kwa walipa kodi wote.
- Kufanya marekebisho ya kifungu cha 54 (2) cha sheria ya kodi ya mapato ili kufuta msamaha wa kodi ya mapato kwa makampuni yenye hisa zipatazo asilimia 25 au zaidi. Lengo la marekebisho haya ni kuleta usawa kwa walipa kodi wanapopata gawio.
- Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa raslimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa hisa za kampuni za ndani unaofanywa na Kampuni mama ya nje ya nchi.
- Kuongeza kima cha chini cha kutozwa kodi (threshold) kwenye mapato ya ajira kutoka shilingi 135,000 hadi 170,000. Hatua hii itaongeza kipato kwa mfanyakazi.
- Kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwa soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es salaam Stock Exchange). Lengo ni kulifanya soko hilo kukua.
- Kusamehe Kodi ya Mapato (kwa wenye leseni) yatokanayo na michezo ya kubahatisha iliyokwishalipiwa kodi chini ya sheria ya kodi ya michezo ya kubahatisha, SURA 41. Lengo la hatua hii ni kuepusha wenye leseni za biashara ya michezo ya kubahatisha kulipa kodi mara mbili.
- Kusamehe Kodi ya Zuio kwenye riba ya mikopo inayotozwa na mabenki ya nje kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye sekta na shughuli muhimu katika mkakati wa kukuza uchumi (Strategic Investors). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wawekezaji hao wanapopata mikopo kutoka kwenye mabenki ya nje ya nchi na hivyo kuhamasisha uwekezaji hapa nchini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 105,672.3
C. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
98. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
- Kufuta Ushuru wa bidhaa uliokuwa unatozwa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo. Hivi sasa mafuta hayo yanatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 40 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji katika viwanda hapa nchini. Aidha, hatua hii itaongeza uzalishaji na kuleta ushindani sawa kwa wenye viwanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa nchi nyingine hivi sasa hazitozi ushuru kwenye bidhaa hiyo.
- Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini. Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato.
Kwa
kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurekebisha
sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii utaanza rasmi
tarehe 1 Januari, 2013.
- Kufuta msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo isipokuwa kwa miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya dini, Balozi, Ofisi za Balozi, Wanabalozi na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha haitahusu Kampuni za Madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.
- Ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyotengeneza maji ya matunda (juisi) dhidi ya ushindani usio haki wa bidhaa hiyo kutoka nje, maji ya matunda kutoka nje yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 83 kwa lita ambapo yanayozalishwa hapa nchini yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 8 tu kwa lita.;
- Kurejea msamaha wa ushuru wa mafuta ya petroli (fuel levy) uliotolewa mwaka 2011/12 kwenye mafuta yanayotumika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili usomeke kama Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwenye mafuta ya Petroli.
- Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe, vinywaji baridi, sigara, na mvinyo kama ifuatavyo: -
a. Vinywaji baridi kutoka shilingi 69 kwa lita hadi shilingi 83 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya shilingi 14;
b. Mvinyo
uliotengenezwa kwa Zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango
kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 145
kwa lita, ikiwa ni punguzo la shilingi 275;
c. Mvinyo
uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango
kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,345 kwa lita hadi shilingi
1,614 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 269;
d. Vinywaji vikali, kutoka shilingi 1,993 kwa lita hadi shilingi 2,392 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 399.
e. Bia
inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa,
kutoka shilingi 248 kwa lita hadi shilingi 310 kwa lita, ikiwa ni
nyongeza ya shilingi 62;
f. Bia
nyingine zote, kutoka shilingi 420 kwa lita hadi shilingi 525 kwa
lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 105 sawa na shilingi 52.5 kwa chupa
yenye ujazo wa nusu lita;
Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo: -
a) Sigara
zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka
shilingi 6,820 hadi shilingi 8,210 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na
nyongeza ya shilingi 1,390 kwa sigara elfu moja au shilingi 1.4 kwa
sigara moja;
b) Sigara
zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa
hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 16,114
hadi shilingi 19,410 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 3,296 au shilingi 3.3 kwa sigara moja;
c) Sigara
nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 29,264 hadi
shilingi 35,117 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya shilingi
5,853 sawa na shilingi 5.8 kwa sigara moja;
d) Tumbaku
ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka shilingi
14,780 hadi shilingi 17,736 kwa kilo, ikiwa ni nyongeza ya shilingi
2,956 kwa kilo; na,
e) Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.
- Kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye Gesi asilia inayotumika viwandani kwa kiwango cha Shilingi 0.35 kwa kila futi ya ujazo (Shs 0.35 per cubic feet);
- Kuongeza Ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 12. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa huduma hii katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ambapo tupo kwenye soko la pamoja.
Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 144,054.9
D. Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, Sura 196;
99. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kuongeza kiwango cha Ushuru wa mauzo nje (export levy)
kwenye bidhaa za ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka
asilimia 40 za sasa au Shilingi 400 kwa kilo moja hadi asilimia 90 au
Shilingi 900 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Lengo la
hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hapa nchini na kuongeza
thamani ya bidhaa za ngozi. Aidha hatua hii itachangia katika kukuza
ajira viwandani na kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 26,431.8
E. Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
100. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA 41; kama ifuatavyo:-
i. Kuongeza
tozo la Gaming Tax kwa casino kutoka asilimia 13 ya mapato ghafi ya
mchezo wa kubahatisha (Gross Gaming Revenue) hadi asilimia 15;
ii. Kutoza tozo kwenye michezo ya Utabiri wa matokeo ya michezo (Sports Betting) kwa asilimia 6 ya “total stakes”;
iii. Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 43 kwenye michezo ya “SMS Lotteries”;
iv. Kutoza tozo la Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 15 kwa michezo ya Internet Casino.
v. Kuweka kipengele katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya kubahatisha kinachotamka kwamba “gaming tax shall be conclusive tax”.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 6,360.
F. Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
101. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari,
SURA, 124 kwa kuanzisha utaratibu wa kumiliki usajili wa namba za
magari zenye utambulisho wa taarifa za mtu binafsi kwenye gari lake kwa
ada ya shilingi 5,000,000 kwa miaka mitatu.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 50
G. Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
102. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya
Ndege, SURA, 365 kwa kuongeza tozo ya huduma za viwanja vya ndege
(Airport Service Charges) kutoka kiwango cha sasa cha Dola za Kimarekani
30 hadi Dola 40 kwa safari za nje na kutoka Shilingi za Tanzania 5,000
hadi Shilingi 10,000 kwa safari za ndani.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,597.7
H. Misamaha ya kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)
103. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kufanya marekebisho kwenye sheria husika za kodi na
matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi kwenye magari kwa
walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka nane (8) kwa
magari hayo badala ya miaka 10. Aidha, magari yenye umri wa zaidi ya
miaka nane (8) yatatozwa Ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la
hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na kulinda
mazingira.
I. Marekebisho mengine katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha
104. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera
katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya
kurahisisha utekelezaji wake.
105. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, SURA 231 ili kwanza,
kuweka kinga dhidi ya mali zinazomilikiwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika Mashariki ikiwemo nyumba, akiba, fedha na akaunti za benki dhidi
ya mashauri ya kisheria, maamuzi ya kimahakama na utaifishaji. Pili,
kuipa hadhi ya mdai benki hii kama ilivyo kwa Taasisi ya Fedha ya
Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili
kuiwezesha kupewa upendeleo endapo yatatokea matatizo yoyote katika soko
la fedha. Tatu, kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutekeleza
maamuzi ya Baraza la uongozi (Governing Board) la EADB kwa kurekebisha
Jedwali la Sheria hii kupitia Tangazo la Serikali na baadaye
kuwasilisha taarifa Bungeni. Nne, kutoa tafsiri ya mali za
benki ili kutoa ufafanuzi kwamba mali za benki ni pamoja na nyumba za
benki, akiba za fedha zilizokasimiwa kwa EADB kwa ajili ya utendaji
wake.
J. Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
106. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali
zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha
kulingana na hali halisi ya ukuaji wa uchumi.
K. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
107. Mheshimiwa Spika,
Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao cha
maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for
Finance) mnamo tarehe 18 Mei 2012 jijini Kampala, Uganda. Kikao hicho
kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha
(EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha
wa 2012/13. Mapendekezo hayo yanalenga katika kuboresha Sekta za
Viwanda, Usafirishaji, Afya, Nishati, Mifugo, Mawasiliano na Habari.
108. Mheshimiwa Spika, maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni: -
i. Kutoza
ushuru wa asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 35 kwenye ngano
inayotambuliwa katika HS Code 1001.90.20 na HS Code 1001.90.90 kwa
kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za
uingizaji wa bidhaa hii nchini kwa vile uzalishaji wa ndani bado ni wa
chini kuweza kutosheleza mahitaji.
ii. Kuongeza
Ushuru wa Forodha kwenye galvanized wire kutoka asilimia sifuri (0%)
hadi asilimia 10 inayotambuliwa katika HS Code 7217.20.00. Hatua hii
inalenga katika kuwianisha viwango vya utozaji wa Ushuru wa Forodha kwa
vile bidhaa hii inatengenezwa kutokana na hot rolled steel wire rods
zinazotambuliwa katika HS Code 7213.20.00 ambayo inatozwa ushuru wa
asilimia 10.
iii. Kutenganishwa
kwa bidhaa zinazotambulika katika HS Code 2106.90.91 ili kutenganisha
virutubisho vya chakula na madini (food supplements and mineral premix)
vinavyotumika katika kutengeneza chakula cha watoto wachanga na
kuzitoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga
katika kuwezesha watoto wachanga na wagonjwa kuweza kupata vyakula
vyenye virutubisho kwa bei nafuu na kuimarisha afya zao.
iv. Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwenye
ving’amuzi (set top boxes) vinavyotambuliwa katika HS Code 8528.71.00
ili kuwezesha mabadiliko ya kutoka katika teknolojia ya analogi na
kwenda katika teknolojia ya digitali. Hatua hii inatekeleza makubaliano
ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba ifikapo Desemba
2015 ziwe zimetoka kwenye mfumo wa utangazaji wa analogi kwenda
digitali.
v. Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye umeme (HS Code 2716.00.00) kutoka asilimia 10
hadi asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama
ya umeme unaonunuliwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
hivyo kupunguza gharama za uzalishaji katika nchi hizo.
vi. Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye glasi za ndani (inner glass) za chupa za chai
(thermos) zinozotambuliwa katika HS Code 7020.00.90 kutoka asilimia 25
hadi asilimia sifuri ili kutoa unafuu na kuchochea ukuaji wa viwanda
vya kuunganisha chupa za chai katika nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa kuwa bidhaa hiyo haipatikani katika Jumuiya.
vii. Kutenganisha
programu (software) inayotambulika katika HS Code 8523.80.00 ili
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia sifuri (0%). Lengo ni kuhamasisha
ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano na hivyo kuongeza mchango wake katika
Pato la Taifa.
viii. Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwenye malighafi ya
kutengeneza sabuni (Palm Sterini, RBD) inayotambuliwa katika HS Code
1511.90.40 kwa kipindi cha mwaka moja. Hatua hii inalenga katika kuvipa
unafuu viwanda vidogo vya kutengeneza sabuni hapa nchini na kuviwezesha
kumudu ushindani katika bidhaa hiyo inapoingizwa kutoka nje.
ix. Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa malighafi ya
kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika HS
Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi
cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na
kukuza viwanda vidogo vya sabuni nchini.
x. Kupunguza
Ushuru wa Forodha kwenye bidhaa inayojulikana kama cathodes
inayotambuliwa katika HS Code 7403.11.00 kutoka asilimia 10 hadi sifuri
(0%). Hivi sasa bidhaa hii inatozwa ushuru wa asilimia 10 ambapo shaba
iliyotengenezwa kwa ukamilifu (refined alloys/refined copper) hutozwa
ushuru wa asilimia (0%), ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria ya
ushuru wa forodha ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004. Lengo la
hatua hii ni kuwianisha ushuru wa malighafi inayotumika kuzalisha
bidhaa hii ili iendane na kanuni/taratibu za kutoza ushuru
zinazozingatia viwango vya usindikaji.
xi. Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 35 kwenye
saruji inayotambuliwa katika HS Code 2523.90.00 kwa kipindi cha mwaka
mmoja.
xii. Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji
wanaotumia mafuta ya kutengeneza vilainishi (castor oil and its
fraction) inayotambuliwa katika HS Code 1515.30.00 Hatua hii imezingatia
kwamba bidhaa hii ni mali ghafi inayotumika katika kutengeneza
vilainishi;
xiii. Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za
barabara vijulikanavyo kama road guard rails kwa kutenganisha HS Code
7308.90.90. Lengo ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya
barabara. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bidhaa hii haizalishwi kwa
kiwango cha kukidhi mahitaji ya soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
109. Mheshimiwa Spika,
Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
i. Kufanya
marekebisho katika Kifungu 30(b) cha Sehemu B ya Jedwali la Tano la
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kutoa msamaha wa
Ushuru wa Forodha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake
vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini. Msamaha huu hautahusisha
vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na
uchimbaji wa madini.
ii. Kufanya
marekebisho katika aya ya 22 (a) ya Jedwali la Tano la Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza “refrigerated
trailers” katika bidhaa zinazopata msamaha wa Ushuru wa Forodha. Hatua
hii inalenga katika kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya
trela yenye majokofu ili kuimarisha biashara ya usambazaji bidhaa kama
vile nyama, maziwa n.k.
iii. Kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi zinazotumika katika
kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical diagnostic
kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri (0%) vinapoagizwa
kutoka nje. Aidha, lengo pia ni kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo
katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
iv. Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano, B kwenye aya ya 15 ili kuongeza
vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali na kuvipa msamaha wa
ushuru wa forodha vinapoagizwa nje na wafugaji wa nyuki. Lengo ni
kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki.
v. Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
vi. Kufanya
marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya
mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa
wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto
wenye utapia mlo na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hatua hii
inalenga katika kuwawezesha kupata vyakula hivyo kwa gharama nafuu na
kuboresha afya zao.
110. Mheshimiwa Spika, Marekebisho mengine ninayotarajia kufanya kwenye Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
i. Kufuta
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye ujazo wa cc 3000. Hatua
hii haitahusu miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye
msamaha wa kodi kwenye mikataba, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya
kimataifa (Diplomats and Diplomatic missions).
ii. Kupunguza
msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye bidhaa zinazotambulika kama
“deemed capital goods” kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90. Kwa
mantiki hiyo, mwekezaji atatakiwa kulipa asilimia 10 ya kodi zote
zinazotozwa kwenye bidhaa husika.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 12,805
Mheshimiwa Spika, hatua
zote za mapato kwa ujumla zimezingatia azma ya Serikali ya kukuza
uchumi na kuongeza mapato ili hatimaye kupunguza utegemezi wa bajeti
kutoka kwa wahisani. Aidha, ili kutekeleza azma hiyo, hatua za mapato
zinalenga katika kupunguza misamaha ya kodi hatua kwa hatua ili kufikia
kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa kama ilivyo katika nchi
nyingine Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
L. Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
111. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2012, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2012/13
112. Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, Serikali
inatarajia kukusanya shilingi bilioni 15,119.6. Kati ya mapato hayo,
Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya
shilingi bilioni 8,714.8 sawa na asilimia 18 ya Pato la Taifa. Aidha,
mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 362.2
sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
113. Mheshimiwa Spika, Washirika
wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutusaidia mwakani kwa kutupatia
misaada na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,156.7. Kati ya fedha
hizo, shilingi bilioni 842.5 ni misaada na mikopo ya kibajeti na
shilingi bilioni 2,314.2 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya
maendeleo, ikijumuisha Basket Funds na fedha za Millenium Challenge
Account (MCA - T).
114. Mheshimiwa Spika, Serikali
inategemea kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,886.1 kutoka vyanzo vya
ndani na nje kuziba pengo la mapato. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za
Serikali za muda mfupi zinazoiva, shilingi bilioni 483.9 ambayo ni
asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,254.1 ni mikopo
yenye masharti ya kibiashara.
115. Mheshimiwa Spika, Kwa
upande wa matumizi, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi
bilioni 15,119.6 katika mwaka 2012/13 kwa ajili ya matumizi ya kawaida
na ya maendeleo. Jumla ya shilingi bilioni 10,591.8 zimetengwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha shilingi bilioni 3,781.1 kwa
ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Taasisi na Wakala za
Serikali na shilingi bilioni 2,745.1 kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa
Serikali. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 4,527.8 zimetengwa kwa ajili
ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,213.6
kitagharamiwa kwa fedha za ndani na shilingi bilioni 2,314.2
kitagharamiwa kwa fedha za nje (misaada na mikopo ya miradi ya
maendeleo ikijumuisha miradi ya MCA (T) na basket fund).
116. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2012/13 inakuwa kama ifuatavyo:-
Mapato
|
Shilingi Milioni
| |||
A.
|
Mapato ya Ndani
|
8,714,671
| ||
(i) Mapato ya Kodi (TRA)
|
8,070,088
| |||
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi
|
644,583
| |||
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
362,206
| ||
C.
|
Mikopo na Misaada ya Kibajeti
|
842,487
| ||
D.
|
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha MCA (T)
|
2,314,231
| ||
E.
|
Mikopo ya Ndani
|
1,631,957
| ||
F.
|
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara
|
1,254,092
| ||
JUMLA YA MAPATO YOTE
|
15,119,644
| |||
Matumizi
| ||||
G.
|
Matumizi ya Kawaida
|
10,591,805
| ||
(i) Deni la Taifa
|
2,745,056
| |||
(ii) Mishahara
|
3,781,100
| |||
(iii) Matumizi Mengineyo
|
4,065,649
| |||
Wizara 3,311,399
| ||||
Mikoa 49,701
| ||||
Halmashauri 704,549
| ||||
H.
|
Matumizi ya Maendeleo
|
4,527,839
| ||
(i) Fedha za Ndani
|
2,213,608
| |||
(ii) Fedha za Nje
|
2,314,231
| |||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
|
15,119,644
| |||
117. Mheshimiwa Spika, mambo yaliyozingatiwa wakati wa mgao wa fedha kwa bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na yafuatayo:-
i. Kuweka
mafungu yote katika kiwango cha mgao wa fedha kinacholingana na
matarajio ya matumizi ya mafungu husika kwa mwaka 2011/12;
ii. Kuyatengea fedha matumizi yasiyoepukika kama vile posho za kisheria, “ration allowance”, nk.
iii. Maeneo mapya ya utawala;
iv. Fedha zinazotolewa kwa wizara zenye utaratibu wa kubakiza (retention);
v. Maeneo ya vipaumbele (strategic na non-strategic).
118. Mheshimiwa Spika,
bajeti ninayoiwasilisha ina uwiano wa asilimia 70 kwa matumizi ya
kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo. Viwango hivyo vya
uwiano vimezingatia ukweli kwamba makisio ya matumizi ya maendeleo kwa
fedha za ndani ya Shilingi 1,871.5 bilioni na makisio ya matumizi ya
maendeleo kwa fedha za nje ya Shilingi 3,054.1 bilioni yenye jumla ya
Shilingi 4,925.6 kwa mwaka 2011/12 hayatafikiwa. Hivyo, inatarajiwa
kwamba hali halisi ya matumizi ya maendeleo itakuwa Shilingi 2,983
bilioni ambayo ni karibu ya asilimia 22. Kwa kipindi kilichoishia
Aprili, 2012 matumizi ya maendeleo kwa fedha za ndani yalifikia 1,201.6
bilioni na matumizi ya maendeleo kwa fedha za nje ni shilingi 1,450.4
bilioni. Sababu za kutofikiwa kwa malengo hayo ya matumizi nimezieleza
hapo awali ikiwa ni pamoja na kutopatikana kwa fedha za mikopo ya
kibiashara na kuchelewa kwa fedha za misaada na mikopo ya miradi ya
maendeleo kutoka kwa wahisani. Aidha, uwiano huo umezingatia maeneo
niliyoyataja hapo juu ambayo ni matumizi muhimu.
VI. HITIMISHO
119. Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia bajeti hii imejipanga kutekeleza Mpango wa Maendeleo
wa mwaka 2012/13 ambao unaelekeza uwekezaji wa rasilimali za Taifa
kwenye maeneo machache ya kipaumbele kwa lengo la kuongeza kasi ya
kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini. Serikali itaendelea kuhamasisha
sekta binafsi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Aidha,
kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika kutumia fursa
zinazojitokeza kwa kutoa huduma na kuzalisha mali ili kujiongezea
kipato.
120. Mheshimiwa Spika,
kufanikiwa kwa Bajeti ya Mwaka 2012/13 kunahitaji nidhamu ya hali ya
juu kwa kila Wizara, Idara, Mikoa, Taasisi na Mamlaka za Serikali za
Mitaa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma. Matumizi
yasiyokuwa na tija na ambayo si muhimu ni vyema yakaepukwa. Sekta
binafsi ina uwezo mkubwa wa kuchangia katika uchumi. Hivyo, ni muhimu
kila Wizara, Idara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa fursa
kwa sekta binafsi ili waweze kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi
wa Taifa letu.
121. Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka
huu unafanyika miezi michache kabla ya zoezi muhimu la Sensa ya Watu na
Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti 2012. Kauli mbiu ya sensa ya
mwaka huu ni ‘‘Sensa kwa Maendeleo Jiandae Kuhesabiwa’’. Napenda
kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine katika ngazi
zote kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hili ambalo matokeo
yake yatawezesha kupata takwimu muhimu zitakazowezesha Serikali kupanga
mipango kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwa usahihi.
122. Mheshimiwa Spika, napenda
kutumia nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wote wa Jimbo la
Kalenga kwa kunichagua kuwa Mbunge wao na kwa ushirikiano wanaonipatia.
Napenda kuwaahidi kuwa nitaendelea kushirikiana nanyi kuliletea
maendeleo Jimbo letu la Kalenga. Mwisho namshukuru mke wangu mpendwa
pamoja na familia kwa kuwa msaada kwangu katika kutekeleza majukumu haya
mapya.
123. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment