Pages

KAPIPI TV

Saturday, June 30, 2012

KUDUMAA KWA SOKA LA TABORA INATOKANA NA KUKOSA VIONGOZI WENYE NIA NJEMA

 Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ulinzi nchini Kitumbo Security Guard,Bw.Yusuph Kitumbo akiwa ofisini kwake wakati akiongea na mwandishi wetu kuhusu suala la michezo Tabora.

Na Mwandishi wetu Tabora.

Licha ya kuwa mkoa wa Tabora una historia kubwa katika tasnia hii ya michezo na kwa sehemu kubwa kwa miaka iliyopita umekuwa na sifa kemkem ya kuwepo kwa vipaji kwa wasanii mbalimbali ikilinganishwa na wakati huu tunaposhuhudia Kifo halali kabisa cha Michezo.

Ingawa kwasasa inawezekana kutumia neno moja tu ili iwe rahisi kueleweka kuwa Michezo mkoani Tabora imekufa kifo cha mende,yaani miguu juu mgongo chini.

Nikisema hivyo pia huenda nikaeleweka kwa wachache lakini nizidi kufafanua kuwa, kawaida Mende anakuwa na mgongo mpana kiasi kama akianguka chali ikiwa haujatokea msaada wa kitu kuwa karibu yake ashike ili aweze kujiinua basi ndio safari ya kuagana na uhai wake,kwa mantiki hiyo nitakuwa nimeeleweka kwa karibu asilimia zote kwa mtu mwenye uwezo wa kufikiri vizuri.

Hivi kila nikijaribu kujiuliza hii Tabora iliyokuwa na wachezaji wenye sifa kubwa hata kufikia hatua ya kuchezea vilabu vikubwa hapa nchini Simba na Yanga imekumbwa na nini mpaka kutoweka kabisa kwenye uwanda huu wa Michezo? au  imefikia kuwa Tabora tumejikita zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali na kusahau michezo kabisa ?na kama ni hivyo mbona hata maendeleo ya mtu mmojammoja nayo yamedumaa?sipati picha.

Maswali haya yalikuwa magumu upande wangu nikalazimika sasa kuwatafuta wadau lakini hasa niliamua kujikita kwenye soka kwani ndilo linalozidi kunitia machungu na hususani pale ninapo jiuliza Timu mahili ya mkoa wa Tabora Milambo ilikufaje au kulikuwa na mkono wa mtu? aah! hayo nayaacha yasinifikirishe sana.

Mmoja kati ya wadau wa Soka mkoani Tabora aliyefunua pazia la kutaka nijue hatma ya Tabora katika Soka ni Apollo Ndali,....huyu alinieleza mengi sana lakini nilichokichukua kwake ni pale aliponihakikishia kuwa Tabora bado kuna vipaji vingi kwa vijana lakini wametelekezwa.

Jambo hili liliniumiza sana nikakaza buti kutafuta wadau wengine baada ya kumuuliza ni nani aliyewatelekeza vijana ambapo jibu alilonipatia nilishika kichwa na kuelekea huko kwa wadau wengine ambapo wapo majibu yao hayakutofautiana sana na ya Apollo, hali iliyonifanya nianze kuamini juu ya hilo.

Lakini pamoja na kufuatilia kwa undani zaidi nikabaki na suala moja tu juu ya lawama kwa viongozi wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora ambao kwasasa kilikuwa  kinaongozwa na Ismail Aden Rage kama Mwenyekiti ambaye ni mbunge wa jimbo la Tabora mjini na Albert Sitta akiwa ni katibu wake,ambapo lawama hizo zimewakaba koo viongozi kwa madai ya kushindwa kukiendesha Chama hicho.

Hata mimi nilijikuta nataka kutokwa na machozi nilipoambiwa hicho chama cha soka mkoa wa Tabora hakina hata ofisi na kibaya zaidi Mwenyekiti Ismail Rage na Katibu wake Abert Sitta hata kuongea au kusalimiana hakuna,sasa nikajua na kuamini kuwa kweli kabisa Soka Tabora limekufa na kuzikwa lakini pia na matanga yamekwishafanyika.

Sikuchoka nikamtafuta mdau muhimu sana wa Soka Tabora ambaye ni mkurugenzi wa Kitumbo Security Guard,...huyu nilianza kwa kumuuliza kuwa kama ana habari juu ya kifo cha Soka Tabora,kwani nilitambua mchango wake mkubwa wa hali na mali  anaoendelea kuutoa hadi sasa kuhakikisha soka linakuwepo Tabora.

"Unajua kwakweli Viongozi wa Chama cha Soka Tabora bado wanatanguliza zaidi maslahi yao kwanza kuliko kurejesha heshima ya mkoa katika soka inayoonekana kupotea bila sababu"alisema Kitumbo kwa mara ya kwanza baada ya kunipa historia ndefu namna ya uendeshwaji wa Chama hicho cha Soka Tabora ambacho kwa sehemu kubwa sasa kinaonekana kuwa ni chama cha mfukoni.

Akaendelea kusema kuwa Rage si mtu wa kulaumiwa kwa sasa ingawa naye ni binadamu ana mapungufu yake  katika hili lakini zaidi anaonekana kutingwa na mambo mengi ya shughuli za kibunge na hivyo kukosa fursa ya kutoa mchango wake kwa Soka la Tabora.

Pamoja na kuuliza mambo mengi lakini hatimaye nikataka kujua ili Soka la Tabora lirudi kwenye nafasi yake nini kifanyike?...''Hakuna zaidi ya viongozi walioko madarakani kujiuzuru ili wapatikane wengine wenye uchungu na mkoa huu na sio wanaopiga blabla za majungu na kutanguliza maslahi yao binafsi"alijibu Kitumbo huku akizidi kusisitiza kwa wadau wa soka kuwa makini wakati wa uchaguzi utakapo wadia.

Swali langu la mwisho baada ya kuridhika kuwa kumbe uongozi ndio sababu kubwa ya kuuawa kwa michezo Tabora,nilitaka kujua kama Kitumbo atakuwa tayari kugombea uongozi tena ngazi ya Uenyekiti wa Chama cha Soka Tabora,..."Naam hilo bado ni mapema sana kulizungumzia,lakini kama nafasi hiyo itagombewa na watu wasio na uwezo kuongoza nitaangalia uwezekano"alijibu hivyo ingawa hakuniweka wazi juu ya hilo.

Kitumbo amekuwa akishawishiwa sana na wadau wa Soka kugombea nafasi ya Uenyekiti endapo uchaguzi ukiwadia hali ambayo inatokana na mchango wake wa hali na mali  katika kuinua Soka Tabora.

Mbali na wadau Kitumbo pia Serikali ya mkoa wa Tabora inamtambua juhudi mbalimbali anazozifanya  katika kuhakikisha soka la Tabora linarudisha heshima yake,ambapo ushahidi wa hivi karibuni ni pale alipozisaidia Timu mbili za mkoa wa Tabora zilizokuwa zikicheza ligi daraja la kwanza Rhino ya Jeshi la wananchi na Polisi ya Tabora.

Kwakuwa jibu ninalo sasa wacha nitulie kimya nisubiri uchaguzi huo wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora Tarefa huenda ikawa ni suluhisho baada ya kupatikana kwa viongozi waadilifu.         

    

 



No comments: