Mwenyekiti
wa Jopo la Majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya
Huduma za Jamii na Uwezeshaji Prof. Samwel Wangwe (kushoto) akisalimiana
na Afisa Mahusiano wa Mgodi wa North Mara Bw. Zakayo Kalebo (kulia)
mara baada ya jopo hilo kuwasili kwenye mgodi huo.
Meneja
Mahusiano wa Mgodi wa North Mara Bi Fatuma Mssumi (mbele) akielezea
shughuli za mgodi wa North Mara mbele ya jopo la majaji waliotembelea
mgodi huo ili kuendelea na zoezi lake la kumtafuta mshindi wa Tuzo ya
Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji.
Afisa
Uhusiano wa Kijiji cha Matongo Bw. Magesa Wanjara akionesha jinsi ya
kutumia bomba la kisima cha maji kilichofadhiliwa na mgodi wa North Mara
mbele ya timu ya majaji, sekretarieti na wajumbe wengine.
Mwenyekiti
wa Umoja wa Kikundi cha Vijana cha Nyakegema Bw. Zacharia Mwita ( wa
pili kutoka kulia) akitoa maelezo mbele ya timu ya majaji na wajumbe
wengine kuhusu mchango wa mgodi wa North Mara kwa kikundi hicho kupitia
mradi wake wa mboga za majani. Kikundi hicho kina jumla ya vijana 578
kutoka katika vijiji saba vinavyouzunguka mgodi huo.
Mwenyekiti
wa Jopo la Majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya
Huduma za Jamii na Uwezeshaji Prof. Samwel Wangwe (kushoto) akisalimiana
na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ingwe Bw. Alfred Joseph mara
timu hiyo ilipofanya ziara kwenye shule hiyo iliyofadhiliwa na mgodi wa
North Mara.
……………………………………………
Na Greyson Mwase, Tarime
Imeelezwa kuwa mgodi wa North Mara
uliopo wilayani Tarime mkoani Mara umechangia jumla ya shilingi bilioni
7.5 katika kipindi cha mwaka 2013 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya
maendeleo katika vijiji saba vinavyouzunguka mgodi huo.
Akizungumza mbele ya timu ya
majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii
na Uwezeshaji chini ya mwenyekiti wake Prof. Samwel Wangwe Meneja
Mahusiano wa Mgodi huyo Bi Fatuma Mssumi alitaja vijiji hivyo kuwa ni
pamoja na Nyangoto, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Kewanja, Genkuru na
Matongo.
Bi Mssumi alisema kuwa kupitia
sekta ya elimu, mgodi ulichangia madawati 2700 yenye thamani ya shilingi
milioni 251.9 kwa ajili ya shule mbalimbali za msingi na sekondari na
kuongeza kuwa mgodi ulijenga shule ya sekondari ya Ingwe kwa shilingi
bilioni 1.1 miradi ambayo imekamilika.
Alisema kuwa mgodi ulifanya
ukarabati pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari ya Kemambo kwa gharama
ya shilingi milioni 905.5, na shule ya msingi ya Bong’eng’e kwa gharama
ya shiligi milioni 827.
Aliongeza kuwa mgodi huo katika
awamu yake ya kwanza ulichangia shilingi milioni 605. 8 kwa ajili ya
ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyamwaga mradi ambao bado unaendelea.
“ Pia mgodi uligharamia shilingi
milioni 12.7 kwa ajili ya wanafunzi waliofanya vizuri kusoma katika
shule na vyuo mbalimbali”, alisema Bi Mssumi
Aliongeza kuwa nia ya kuwekeza
katika elimu katika wilaya ya Tarime ni kuhakikisha wanajenga msingi
utakaopelekea kupatikana wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi katika
mgodi huo.
Akielezea mchango wa mgodi huo
katika sekta ya afya Bi Mssumi alitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na
ukarabati na ujenzi wa zahanati ya Genkuru uliogharimu shilingi milioni
61.2, upimaji wa macho kwa wanakijiji 3,000 kwa shilingi milioni 19
pamoja na upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa wanakijiji 1067 uliogharimu
shilingi milioni tano.
Aliendelea kusema kuwa mgodi huo
ulitoa msaada kwaajili ya upasuaji kwa wanakijiji 11 ambapo jumla ya
shilingi milioni 12.2 zilitumika
Akielezea sekta ya maji Bi. Mssumi
alisema kuwa mgodi ulichimba visima katika vijiji sita kwa thamani ya
shilingi milioni 888.3 pamoja na usambazaji wa maji katika vijiji vya
Nyangoto, Kewanja, Matongo na Kerende uliogharimu shilingi bilioni 1.2
Alisema kuwa mgodi pia ulifanya
ukarabati katika kituo cha afya cha Nyangoto kwa gharama ya shilingi
milioni 481.7 pamoja na usafi katika vijiji vya Nyangoto, Kerende,
Kewanja na Nyamwaga uliogharimu shilingi milioni 544.4
Alisisitiza kuwa ili kuhakikisha
kuwa wachimbaji wadogo wananufaika na sekta ya madini kupitia kujiajiri
mgodi huo ulichangia shilingi milioni 91.4 kwa kikundi cha wachimbaji
wadogo Tarime kwa ajili ya ununuzi wa mashine kwa ajili ya kusaga
kokoto.
Bi Mssumi aliongeza kuwa hatua
iliyofikiwa sasa ni mkandarasi kufanya kazi ya kutoa umeme kutoka mgodi
wa North Mara hadi mashine ilipo ili ianze kazi mara moja.
Alisema kuwa mgodi pia
ulifadhili miradi mbalimbali kwa gharama ya shilingi milioni 252.5
pamoja na vikundi vya kijamii/kidini kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8
Akizungumzia mchango wa mgodi huo
katika sekta ya miundombinu Bi Mssumi alisema kuwa mgodi huo ulikarabati
barabara yenye urefu wa kilomita 47.9 kwa gharama ya shilingi milioni
469 pamoja na uunganishaji wa umeme kwa kushirikiana na Shirika la Umeme
Nchini (Tanesco) katika vijiji vya Kerende na Matongo kwa gharama ya
shilingi milioni 472
Alitaja miradi mingine kuwa ni
pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi uliogharimu shilingi milioni 555.5
na ujenzi wa mahakama ya mwanzo Nyamongo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
nyumba za wafanyakazi wa mahakama hiyo kwa shilingi milioni 182.9 mradi
ambao haujakamilika bado.
Akizungumzia changamoto katika
utekelezaji wa miradi hiyo, Bi. Mssumi alisema kuwa kumekuwepo na tatizo
la wanavijiji kuhujumu miundombinu ya maji iliyowekwa hali inayopelekea
mgodi huo kuingia gharama kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo.
“Wapo wanakijiji wasio waaminifu
ambao huharibu miundombinu ya maji kwa makusudi ili kufanya biashara ya
maji jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya vijiji hivyo”
Alisisitiza Bi. Mssumi.