Na Anthony Mayunga-Mara
JESHI la polisi wilaya ya Butiama mkoani Mara limeweka ulinzi mkali
kwenye hospitali ya wilaya hiyo kufuatia tishio la jamii ya kabila la
Wazanaki kutaka kumuua mtoto aliyezaliwa hana miguu wala mikono kwa
imani kuwa ni mkosi kwa jamii hiyo.
Tukio hilo limetokea agosti 7 majira ya saa 7:00 mchana mara baada ya
Maria Joseph(18)mwanafunzi wa kidato cha pili Bumangi wilayani hapo
kujifungua mtoto huyo wa kiume mwenye afya nzuri lakini hana mikono na
miguu.
Kwa mjibu wa maelezo ya diwani wa kata ya Mliaza Denis kwa gazeti hili
kwa njia ya simu alisema kwa kushirikiana na mkuu wa kituo cha polisi
wilaya hiyo Inspekta Kadiwa waliamua kweka ulinzi hospitalini hapo
baada ya kuwepo mipango kutoka kwa jamii mtoto huyo auawe kwa madai
kuwa nimkosi(Kitimba).
"Baada ya kubaini hilo tumeamua kuweka ulinzi hospitalini hapo maana
haiwezekani kuruhusu watu waue mtoto kwa imani za kimila,lazima
alindwe maana ana afya nzuri na atalelewa hapo kituoni kwa muda huo
tukisubiri taratibu zingine"alisema diwani.
Alisema kwa sasa mama wa mtoto huyo anahitaji msaada zaidi kwa kuwa ni
mdogo na alitakiwa kuwa shuleni lakini akapewa ujauzito na mkazi mmoja
wa kijijini hapo aitwaye David Juma ambaye alitoroka baada ya kubaini
anatafutwa.
Hata hivyo alipotakiwa kutoa ufafanuzi ulinzi huo utakoma lini na
wakati atakapotoka hospitali wamejipangaje,alidai wanaendelea kuweka
mazingira mazuri ili asije akapata madhara kutoka kwa ndugu na baadhi
ya wazee ambao wanaamini kuwa kumwacha bila ulinzi anaweza kuuawa.
Tukio hilo anadai ni kwanza kwake kutokea eneo hilo,ingawa anadai kwa
wazee wa zamani wanadai yalikuwa yanatokea ndiyo maana wakaweka
utaratibu wa kuwaua watoto kama hao.
No comments:
Post a Comment