Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa
kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi
huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest
Act).
Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya
Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na
maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala ya kuwezesha
ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
Hivyokutokana na kujirudiarudia kwa mauaji
yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito kwa Rais Jakaya
Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi,
kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi
wa kina.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi
la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya
machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa
ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na wengine waliokuwa
wakiendelea na shughuli zao eneo la Msamvu, hivyo kusababisha kifo cha
raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.
CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji
hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na
CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya
msingi kwa raia wote.
CHADEMA hakikubaliani na hatua
zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na
maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012
ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa
maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji
husika.
CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na
Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na
mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na
Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa
na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la
tukio.
Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa
maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali
na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani
na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto
na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na
kudondoka.
Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza kwamba
bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo
pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya
risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia
mabomu ya machozi.
Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka
na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali
Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio
hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo
karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya
mashambulizi.
Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la
Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani
Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa
sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa maandamano
yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la
Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la
Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na
makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za
Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na
madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya
machozi.
Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA kilipanga
kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4
Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa
sheria.
Hata hivyo,
Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio
cha Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya
mikutano ya CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi
wowote.
Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA
ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja
na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na mkutano wa
CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26
Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi
la Polisi liliikubali.
Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa
barabara za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi,
hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi liliandika barua ya
kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake
kisheria) na pia limekataza maandamano.
CHADEMA kikaamua kwa mara nyingine tena
kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro,
tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya
watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012
mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.
Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi
la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu
taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi
ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu
za misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza
kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.
Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa
iwapo vyama vya siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka
ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria
ya Vyama vya Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya
kisheria ni kutumia mahakama.
Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa
sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa
ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo
likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa
kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.
Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa
wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa
wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa
sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa
jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka
sheria.
Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa
kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi yafanyike kwa msafara wa
vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya
machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika
eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo
yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano
ya magari na vyombo vingine vya usafiri.
Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu
kubwa kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa
muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla
kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani
kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona
wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la
mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka
mwanzo yasingetokea madhara yoyote.
Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya
maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio
husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi
huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act)
Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.
CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali
inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi
wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya
Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court)
katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.
CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia
kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli
husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya
dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi
bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye
utata.
Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali
Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa ianze
kutumika.
Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu
taratibu za maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu
ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili
ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi
kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya
majadiliano yanayoendelea na familia.
CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala
wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA
kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na
maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.
CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya
CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya
wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao
yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa
kisingizio hicho.
Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo
na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27
Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya
tarehe hiyo.
Tume hiyo inaendelea na mikutano yake ya
hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati
huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA
inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.
CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza
iwapo matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa
vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa
maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa
maslahi ya wengi.
CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua
baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem)
uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au
kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act)
kuwezesha uchunguzi huru.
Imetolewa tarehe 29 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment