(Picha  na Nathaniel Limu).

Na.Nathaniel Limu.
Afisa wanyama pori katika halmashauri ya wilaya ya Singida Augustino Lawi Lorry aliyekuwa akikabiliwa na shitaka ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 4,000 (elfu nne tu), amenusurika kwenda jela miaka mitatu baada ya ndugu zake kumlipia faini ya shilingi laki tano (500,000).

Mshitakiwa Lorry baada ya kutiwa hatiani na mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida kwa kosa la kuomba rushwa ya shilingi elfu nne, alipewa adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki tano taslimu na akishindwa aende jela miaka mitatu.

Ndugu zake walipobaini kuwa mshitakiwa Lorry hana kiasi hicho cha fedha, mara moja walichangishana na kumlipia ndugu yao ili asiende kutumikia kifungo jela kwa hofu kwamba atapoteza ajira yake.

Awali mwendesha mashitaka, mwanasheria wa TAKUKURU mkoa wa Singida Boniface Kamwesigele, alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida Ruth Massamu, kuwa mnamo Septemba 8 mwaka juzi kati ya saa 1.00 na 1.30 asubuhi, jirani na hospitali ya mkoa, mshitakiwa bila halali, aliomba rushwa ya shilingi 4,000 kutoka kwa watu wanne waliokuwa wamepakia magunia manne ya mkaa kwenye baiskeli zao.

Alisema siku ya tukio, Abubakari Nkindwa, Juma Makuri, Adamu Seleman na Ally Salum kila mmoja alikuwa amepakia gunia moja la mkaa kwenye baiskeli na walikuwa wakisaka wanunuzi katika mitaa ya mjini Singida.

Boniface alisema wakati watu hao wakitafuta wateja wa kuwauzia mkaa, walikutana na mshitakiwa Lorry ambaye aliwaomba wamwonyeshe vibali/leseni zao za kufanya biashara ya mkaa.

Alisema baada ya watu hao kudai kuwa hawana kibali wala leseni, mshitakiwa alianza kuwaomba kila moja shilingi 1,000 ili asiwakamate na kuwapeleka kituo cha polisi.

“Watu hao waligoma kabisa kutoa rushwa hiyo na ndipo mvutano mkubwa ulizuka na kusababisha watu waliokuwa wakipita eneo la tukio, baadhi wakiwa ni maafisa kutoka ofisi ya TAKUKURU mkoa, kufika  kwa lengo la kuamua. Baada ya maafisa hao wa TAKUKURU kuwahoji watu hao, walidai kuwa walikuwa wanaombwa rushwa na Lorry”, alisema.

Mwanasheria huyo alisema kuwa baada ya maelezo hayo watu hao wanne pamoja na afisa wanyama pori Lorry, walichukuliwa hadi ofisi ya TAKUKURU ambapo faili lilifunguliwa kuhusu kitendo cha Lorry kuomba rushwa.