Pages

KAPIPI TV

Tuesday, August 21, 2012

DR. KAFUMU WA IGUNGA AENGULIWA UBUNGE NA MAHAKAMA."Magufuli,Rage na Mkama wadaiwa kumponza"

Pichani ni aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Igunga Mh. Dk. Dalaly Peter Kafumu  akiwa na Kada wa CCM Dr.John Pombe Magufuli. (Picha na Maktaba)
Na Mwandishi wetu Nzega
MAHAKAMA KUU ya kanda ya Tabora imetengua nafasi ya Ubunge wa Mbunge  jimbo la Igunga Dkt,Dalali Peter Kafumu aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kufuatia shauri la kupinga matokeo yaliyo mpatia ushindi mbunge huyo kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi CCM  katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana jimboni humo.
Shauri Hilo lilifunguliwa na mlalamikaji Joseph Kashindye ambaye alikuwa mgombea wa chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA) dhidi ya Dkt,Peter Dalali kafumu,Mwanasheria Mkuu wa serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi jimboni humo Protace Magayane.
Akisoma hukumu hiyo jaji Mery Nsimbo Shangali kuwa mahakama ilipokea malalamiko 15 ambayo yalilidhiwa kwa pande zote mbili ambapo mahakama hiyo iliongeza madai nakufikia madai 17 ya msingi.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo jaji Mery Shangali alisema kuwa malalamiko yaliyothibitishwa na mahakama ni madai 10 huku hoja 7 zikithibitishwa na mahakama hiyo.
Akisoma hoja zilizothibitishwa na mahakama hiyo kuwa ni pamoja na Dr.John Pombe Magufuli Waziri wa ujenzi alitumia nafasi yake hiyo kutoa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu  ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa jimbo la Igunga ambao ndio wapiga kura.
Ilidaiwa pia Dr.John Magufuli akiwa katika uchaguzi mdogo huo wa Igunga  katika moja ya kampeni alitumia nafasi ya uwaziri kuwatisha wapiga kura wa jimbo hilo kama hawatamchagua mgombea wa CCM  watawekwa ndani.
Akiendelea kusoma hoja hizo Jaji Mery alisema kuwa Mbunge wa jimbo la Tabora mjini Adeni Rage kutangaza kuwa mgombea wa chama cha Demokrasia na maendeleo chadema kajitoa katika uchaguzi jimbo hilo mahakama ililidhika na ushahidi uliokuwa ukitolewa.
Katika hoja nyingine ni kwamba Imamu Swaleh Mohamed wa mskiti wa Ijumaa Igunga aliwatangazia waumini wa Dini ya Kiislam kuwa wasikichague chadema kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wamemdhalilisha mkuu wa wilaya ya Igunga Fatuma Kimario hata mahakama hiyo iliridhika na ushahidi  uliotolewa katika hoja hiyo.
 Hoja nyingine Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi Wilson Mkama alisema  kuwa chama cha chadema kimeleta makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga hata hivyo mahakama kwa kupitia mashahidi na vyombo vya habari iliridhika na ushahidi huo.
Katika Hoja kuu ya mahindi ambayo ilikuwa ni hoja kubwa na kutolewa ufafanuzi mkubwa zaidi ni kwamba,jaji Mery alihoji wananchi wa Igunga walikuwa na njaa sana?je kwanini uchaguzi usifanyike wakati wananchi wana njaa hivyo basi mahindi hayo yalitumika kama njia ya kujipatia umaarufu kwa baadhi ya wanasiasa hususani viongozi wa serikali.
Aliongeza kuwa suala la kutokupeleka malalamiko hayo kwa tume ya uchaguzi sio hoja ya msingi ambayo inaweza kumzuia mlalamikaji kupeleka malalamiko hayo katika mahakama kuu na hakuna kifungu chochote kinacho mzuia mlalamikaji kupeleka hoja hizo.
Akitoa hukumu hiyo Jaji Mery alisema kuanzia sasa jimbo la Igunga lipo wazi na kumuagiza msimamizi wa uchaguzi mkoa wa Tabora kufuata utaratibu unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kutumiwa nakala hizo za hukumu na milango iko wazi kwa kufuata utaratibu mwingine endapo mjibu madai huyo wa kwanza hajaridhika.
Hali ya usalama katika mahakama hiyo ilikuwa imeimarishwa huku wafuasi wa Chadema wakiwa wengi zaidi wakionekana kuwa na furaha hasa pale hukumu hiyo ilipotolewa.

No comments: