Nape akizungumza na waandishi wa habari leo |
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinalaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wana siasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye
alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu
kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la
kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni
mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha
kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na
TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema
Nape na kuongeza;
"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake
wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama
vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa
kwa rushwa hii".
Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha
ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na
Chadema.
"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja,
na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo
ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge
waliotusaliti", alisena Nape.
Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na
viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna
hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi
kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati
na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu
wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo,
ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa
kwenye wizara hiyo.
"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara
hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi
mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa
kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia
serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua
kubwa ya maendeleo.
"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
No comments:
Post a Comment