TAARIFA KWA UMMA
Taasisi ya vyombo vya
habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania MISA-Tanzania) inasikitika kuarifu umma
wa watanzania kwamba inapinga vikali kitendo cha serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Magazeti Tanzania Bara
kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kuanzia
tarehe 30 Julai 2012.
Katika taarifa
iliyotolewa na serikali kupitia tangazo lake lililochapishwa kwenye magazeti
mbalimbali hapa nchini na kunukuu kutolewa kwa amri hiyo kupitia gazeti la
serikali (Government Notice) toleo namba
258 la tarehe 27 Julai 2012, serikali imeeleza kama ifuatavyo:
“Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana
gazeti la MwanaHalisi kwa mujibu wa sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu
namba 25 (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai 2012”
Aidha, tamko hilo la
serikali limeeleza pia kuwa sababu za msingi za kulifungia gazeti hilo ni
kufuatia machapisho mbalimbali ya gazeti hilo kwenye toleo Na. 302, Na. 303
pamoja na toleo Na. 304 yote yakiwa ya mwezi Julai 2012 pamoja na machapisho
mengine yaliyotangulia. Serikali imeeleza kuwa machapisho hayo yamekuwa “yakichapisha
habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii”
Hata hivyo, serikali
haikubainisha ni habari zipi katika machapisho hayo ambazo zinaeneza na kujenga
hofu kwa jamii. Kitendo hicho cha kutobainisha habari husika kinatufanya sisi
kama wanahabari na watetezi wa haki ya kupata taarifa pamoja na uhuru wa vyombo
vya habari nchini na katika kanda ya kusini mwa Afrika kutoridhia maamuzi ya
serikali kwani yamehusisha masuala ambayo hayakuwekwa bayana.
Ni kwa mashaka makubwa
ambayo yanatokana na tamko husika la serikali kwa kutumia maneno yafuatayo:
“Kuanzia sasa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo
vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo
zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu”
MISA–Tanzania
inasikitishwa na kauli hiyo kwani kauli hiyo ni kudhihirisha matumizi mabaya ya
sheria zilizopo katika kukandamiza uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo
vya habari kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 ibara ya 18 (b) na (d) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.
Haki ya kutafuta, kupata
na kutoa taarifa ni haki ya msingi ya kila binadamu na imetambuliwa hivyo na
Katiba ya Tanzania. Haki hii imetambuliwa pia na mikataba mbalimbali ya
Kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia bila masharti yoyote.
Kama kweli kuna taarifa
za uchochezi zilizochapishwa na gazeti la MwanaHalisi na kuhatarisha amani na
utulivu wa nchi, ni vyema serikali ingebainisha taarifa hizo kwenye chapisho
husika na siyo kuorodhesha machapisho mbalimbali kama sababu yake ya kulifungia
gazeti. Hata hivyo, mamlaka ya serikali kufungia gazeti kupitia msajili wa
magazeti ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na matumizi makubwa ya
madaraka.
Ni kwa sababu hizo kwamba
Ripoti ya Haki za Binadamu iliyowahi kuandaliwa na kutolewa na Tume maalumu
iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujulikana kama Tume
ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilibainisha sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kuwa ni
miongoni mwa sheria arobaini ambazo zinakandamiza haki za binadamu nchini.
Sheria hiyo haina budi kufutwa kwenye vitabu vya sheria za nchi hii.
Kitendo cha kulifungia
gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kinaweza kusababisha hofu kubwa kwa
watetezi wa haki za binadamu na wanahabari kwa ujumla. Kitendo hicho kinafuatia
kile cha kuwakamata na kuwaweka rumande (Oysterbay Polisi) wanaharakati zaidi
ya kumi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kuandamana kufuatia mgomo wa Madaktari
mnamo tarehe 9 mwezi Februari 2012.
MISA –Tanzania inalaani
vikali matumizi mabaya ya Dola katika kunyamazisha wanahabari wanapojaribu na
kuthubutu kufuatilia matukio mbalimbali na kuarifu umma kuhusu yale
waliyoyafanyia kazi kwa kina. Ni rai yetu kwa serikali kuwa ni vyema wabainishe
taarifa mahsusi zilizopelekea maamuzi ya kufungia gazeti la MwanaHalisi ili
kutuondolea hofu sisi tunaotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari. Kuendelea
kuficha taarifa husika ni kuendelea kuikanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977 (ibara ya 18) kupitia kivuli cha Sheria ya Magazeti ya mwaka
1976 ambayo kimsingi imepitwa na wakati na haiwezi kutumika kinyume na Katiba
ya nchi.
Ni rai yetu pia kwa
serikali ya Tanzania kwamba izingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika yale yenye kuhamasisha utoaji haki kuliko kujikita kwenye kifungu cha 30
cha Katiba hiyo ambacho kimsingi kinaweka mipaka maalumu ya ukiukwaji wa haki
za binadamu. Mipaka hiyo haionekani kuzingatiwa na serikali katika kulifungia
gazeti la MwanaHalisi.
Kwa
taarifa hii kwa umma, tunaiomba pia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kulifungulia gazeti la MwanaHalisi mapema iwezekanavyo na bila masharti ili
kuwawezesha watanzania kuendelea kunufaika na taarifa zinazochapishwa na gazeti
hilo ilmradi maadili ya uandishi wa habari yazingatiwe. Hii ni haki ya msingi
kwa kila mtu na ni vyema aione ikitekelezeka.
Taarifa
hii imetolewa na kusaini hapa Dar es salaam leo tarehe 31 Julai 2012.
Mohammed Tibanyendera
Mwenyekiti,
MISA-TAN
No comments:
Post a Comment