Pages

KAPIPI TV

Wednesday, June 13, 2012

POLISI DODOMA WAWASHIKILIA TISA KWA KUJIFANYA WAGANGA WA KIENYEJI

Baadhi ya watuhumiwa wa utapeli wa kufanya waganga wa kienyeji wa  Kundi la Lamba Lamba  wakiwa wameshika dhana za kazi wakiwaonyesha waandishi wa habari pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen hawapo pichani. Kutoka kushoto waliovaa kawaida ni Mkude S/O Mwenda 32 yrs, Mkulima, na Joseph S/O John miaka 27, Mkulima, wote wakazi wa Mkoka – Kongwa na  SALEHE S/O OMARI, mwenye umri wa miaka26, mkulima wa Songe Kilindi Mkoani Tanga aliyevaa lubega nyekundu kwa nyeusi na ndani ana fulana mistari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen akiwaonyesha waandishi wa habari hawapo pichani vyeti feki vya watuhumiwa wa  kundi la Matapeli la LAMBA LAMBA   vyeti hivyo ni vya (UMAWATI )– cha mtuhumiwa  DK. Shabani R Kisoma amacho kirefu chake ni UMOJA WA WAGANGA WATAFITI WA MAGONJWA  SUGU UKIMWI NA TIBA ASILIA TANZANIA, na  (CHAUMUTA) – Cha mtuhumiwa anayejiita DK. Hussein Shomari Mabogo, ambaye amekamatwa , kirefu chake ni CHAMA CHA UTAFITI WA MAGONJWA SUGU NA UKIMWI KWA TIBA ASILIA. 

Na. Luppy Kung'alo, Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watuhumiwa tisa wa utapeli wanaojifanya Waganga wa Jadi na Tiba Asilia kwa kuwalaghai wananchi katika vijiji mbalimbali kisha  kuwatapeli na  kusababisha hofu, na uvunjifu wa Amani miongoni mwa wanakijiji mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw. Zelothe Stephen alisema watuhumiwa hao wanajiita LAMBA LAMBA walikamatwa juzi  katika Wilaya ya Kongwa, katika kijiji cha Mkoka  baada ya Polisi kupata taarifa kuwa, wanakijiji hicho kuwavamia katika nyumba waliyofikia na kutaka kuwauwa.
”Matapeli hawa wametokea Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Marogoro, na kuvamia mkoa wetu, kisha kufanya utapeli wao na kuzusha hali ya hofu na isiyo ya kawaida kwa wanakijiji wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma”. Alisisitiza Kamanda Zelothe Stephen.
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema, Kundi hilo la LAMBA LAMBA limekuwa  likichochea Chuki na Uadui  miongoni mwa wanajamii kwa kufanya vitendo vya kupandikiza vitu nyakati za usiku, halafu baadae  mchana wanakwenda kuvifukua na kudai wanabaini wachawi na kutoa uchawi katika kila nyumba kwa madai ya kualikwa na wazee wa Kimila.
Kamanda Zelothe Stephen alisema Matapeli hao, wamedai kualikwa na wazee wa kimila  chini ya Mwenyekiti na Katibu waitwao SAMANDARO S/O?  Na CHIPENDWA S/O? Na kupewa makazi katika nyumba mbili za ukoo wa MAPUGA S/O? Ambazo zinasimamiwa na Bw. SOSPETER S/O MAPUGA.
Akizungumza moja ya tukio lilozua hofu na kusababisha uvunjifu wa amani alisema katika shuguli zao walipita kila nyumba katika kijiji walichodai kualikwa na wazee hao  lakini walipofika  katika nyumba ya MESHACK s/o MAPUGA aliwakatilia kuingia kwake hivyo waliondoka kwenda katika vijiji vingine.
Alisema Baada ya kuondoka  hapo Mtoto wa Mzee MESHACK S/O MAPUGA aitwaye MARTHA S/O AINEA MAPUGA MIAKA (34) mgogo mkazi wa kijiji cha Mlanje alianza kuumwa tumbo kisha kupelekwa zahanati ya Mkoka na hatimaye Hospitali ya wilaya Kongwa ambapo madaktari walithibitisha kifo cha binti huyo kutohusiana na imani za kishirikina lakini kwa bahati mbaya alifarikia dunia usiku wa tarehe 10/06/2012 akiwa Hospitalini hapa.
”Kifo hicho kilileta sintofahamu katika familia hiyo, iliyopelekea kufikiri kwamba kikundi cha LAMBA LAMBA walihusika na kwamba  ndio tatizo kwa sababu za imani kishirikina.”aliongeza Bw, Zelothe Stephen.

Mkuu huyo wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma alisema kutokana na hali hiyo  wanakijiji waliungana na familia ya wafiwa na kwenda kuwavamia kundi la LAMBA LAMBA   wakiwa na silaha za jadi, ambazo ni mikuki, mapanga na marungu kwa lengo la kutaka kuwaua lakini walifanikiwa kuvunja mlango na madirisha na kukuta wametoroka.
 
Baadhi ya wanakijiji walitoa   taarifa  za tukio hilo kwa Jeshi la Polisi na  Operesheni ya kuwatafuta watu hao ilianza  ambapo jumla ya watuhumiwa saba kati ya tisa wa kundi hilo  walikamatwa usiku huo na wengine wawili walikamatwa siku iliyofuta wakiwa wanawafuatilia wenzao, alisema Kamanda Zelothe.
 
 Bw. Zelothe Stepen alisistiza kwamba  pindi upelelezi  utakapo kamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
 
Hata hivyo Kamanda Zelothe alisema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeunda Kikosi kazi Maalumu katika wilaya zake zote kwa lengo la  kufanya Operesheni Maalum  ili kudhibiti  na kutokomeza kundi hilo na washirika  wake na kuahidi kuwasiliana na Makamanda wenzake wa mikoa ili kudhibiti vitendo hivyo.
 
”Napenda kutoa wito kwa wananchi wote, viongozi wa Serikali katika ngazi za Vijiji, Kata, Tarafa na  Wilaya kusimamia Sheria, Kanuni na taratibu za nchi zinavyotaka, ili kuweza kudhibiti uhalifu huu na  kuondoa hali ya sintofahami miongoni mwa jamii inayoweza  kusababisha uvunjifu wa Amani ndani na nje ya mkoa wa Dodoma inatokomezwa.” Alisistiza kamanda Zelothe Steven

No comments: