Pages

KAPIPI TV

Wednesday, June 13, 2012

CHAMA CHA KUTETEA HAKI ZA WANAUME CHAPIGA HODI BUNGENI"Sasa chataka kianze kutambuliwa rasmi na mhimili huo wa Bunge"





Kumb Na. CKHWT/HQ/VOL. 0001/2012                                   09/06/2012

OFISI YA SPIKA WA BUNGE LA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
S.L.P 941,
DODOMA.

Mh. Spika,

YAH: CKHWT KUOMBA KUWA WAGENI WAKO
KATIKA KIKAO KIJACHO CHA BUNGE LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA.

Rejea kichwa cha somo tajwa hapo juu,

Kwa heshima na taadhima Uongozi wa juu wa chama cha kutetea Haki za Wanaume Tanzania [ CKHWT ] umekaa na kutafakari kwa kina sana na kuona kuna umuhimu mkubwa wa kukuomba kuwa wageni wako katika kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Lengo kubwa la Chama hiki ni kuomba  kutambuliwa na mhimili huu muhimu katika nchi yetu kwa vile tumeona kuwa, pamoja na viongozi waasisi wa Taifa hili  kufanya mambo mengi mazuri, waasisi wa chama hiki wamegundua mapungufu makubwa kuhusu haki sawa kwa wote.

Hivyo chama hiki kinaomba kuwakumbusha viongozi wetu sasa kuwa baadhi ya mambo muhimu waliyoyaweka walisahau kukumbuka “siku ya mwanaume” nchini  ili Tanzania nayo sasa iweze kuonekana inamtendea haki mwanaume kwa kutomtenga katika mambo mazito ya kitaifa na kimataifa, ili  kuungana na nchi nyingine Duniani kuiadhimisha siku hiyo kama ilivyo kwa Siku ya Wanawake Duniani, Siku ya Mtoto Duniani n.k. siku ambazo huadhimishwa na walengwa ili kuweza kuwa na matamko mbalimbali na kauli mbiu zinazoimarisha na kujenga umoja wa Watanzania bila kuathiri haki za Binadamu upande wowote.

Mh.Spika, chombo hiki kitakuwa ni chombo huru ambacho moja ya malengo yake makubwa ni kutetea Haki sawa kwa wote tofauti na ilivyo sasa ambapo zipo taasisi zinazotetea upande mmoja, jambo linaloonyesha kubaguliwa kijinsia kwa Mwanamme wa Tanzania kwa vile hana sauti ndani na nje ya mipaka ya nchi. 

Mh. Spika, kupitia chombo hiki muhimu kwa Mwanamme wa Tanzania tunaliomba Bunge lako tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukitambua rasmi chama hiki na kwamba tunaomba sana kwa waheshimiwa wabunge wote, Serikali, waheshimiwa mabalozi wa nchi mbalimbali, taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, wafanya biashara mashuhuri akiwemo Mkurugenzi mtendaji wa makampuni ya IPP Dr Regnald Mengi na  wadau mbalimbali nchini mtuunge mkono kwa kutupa misaada mbalimbali ikiwemo majengo,fedha na vyombo mbalimbali vya usafiri ili kukiimarisha chama hiki kusaidia kuenea kwa kasi nchi nzima angalau chama hiki kiweze kuanza shughuli zake katika ngazi za Wilaya Mkoa na Taifa.

Pia tunaomba wasomi hususan vyuo vikuu nchini watusaidie kutoa michango ya maandishi itakayosaidia kuboresha katiba ya chama hiki ambayo itakuwa ni katiba Baba wa Mwanaume wa Tanzania.

Mh. Spika, sisi kama wadau na watetezi wa haki za binadamu ilikuwa inatupa wakati mgumu na mkanganyiko mkubwa  sana hasa wakati wa kutetea Haki za Binadamu kwa vile kuna baadhi ya taasisi ndani na nje ya nchi ambazo tayari zinatetea upande mmoja na kuuacha upande wa Baba ukiwa hauna mtetezi na msimamizi wa kuhakikisha kwamba  endapo mwanamme wa Tanzania hajatendewa Haki, mtetezi wa upande huo anasimamia haki ikiwemo kupewa msaada wa kisheria katika vyombo vya utoaji haki. 

Mh. Spika, kwa namna ya kipekee tunapenda kukipongeza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kwa Ripoti yake iliyotolewa kwa waandishi wa habari na wao kuitoa kwa umma ili kuona unyanyasaji anaofanyiwa Baba licha ya kutolewa kwa matukio mbalimbali na vyombo vinavyotetea upande mmoja huku vikiacha kutoa hali halisi bila upendeleo.

Baba wa Tanzania anatambulishwa kitaifa na kimataifa kuwa ni hodari kwa ukandamizaji akitumia mfumo dume huku kukiwa hakuna chombo kinachojibu tuhuma hizi kutimiza Demokrasia ya kweli kwa wote bila kuathiri Haki za Binadamu ndani na nje ya nchi.

Mh. Spika, tunaomba sasa tuishie hapa ili kulipa bunge hili nafasi ya kujadili na kutoa maelekezo kwa wadau mbali mbali ili chombo hiki kiweze kuwa huru kufanya shughuli zake kwa kuwa tayari tuko katika mchakato wa kukamilisha taratibu za usajiri na kuandaa sherehe za uzinduzi utakaofanyika Mkoani Mwanza kwa kumuomba Mh waziri Mkuu kuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo.

Asante kwa kukubali ombi letu.

Antony J.  Sollo

………………………………………
Katibu Mkuu wa CKHWT Taifa
Nakala:
Vyombo vyote vya Habari
                          

No comments: