Naibu waziri wa Tamisemi Bw.Kassim Majaliwa amewataka
maafisa elimu nchini kujiepusha na lugha chafu kwa walimu kwakuwa imebainika kuwa wamekuwa
wakiwakatisha tamaa baadhi ya walimu na kushindwa kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake mjini Tabora
Bw.Majaliwa alisema amekuwa akipokea malalamiko mengi ya walimu dhidi ya
maafisa elimu ambao wamekuwa na matamshi yasiyoridhisha na kuwafanya baadhi ya
walimu waione ngumu kazi ya ualimu hatua ambayo pia inapunguza rasilimali ya
uwajibikaji nchini.
Katika mkutano huo wa majumuisho ya ziara yake uliofanyika
Chuo cha Ualimu Tabora,Naibu waziri Majaliwa akawageuzia kibao pia watumishi wa
halmashauri waliokatika ofisi za Masijala kuacha tabia ya usumbufu kwa walimu
wenye shida mbalimbali na hasa wakati wa kufuatilia haki stahili zao jambo
ambalo alidai kuwa limeota mizizi kwa baadhi ya halmashauri.
Kwaupande mwingine sambamba na kubainisha kuwa Serikali ipo
katika mchakato wa kuboresha makazi ya walimu na maslahi yao kwa ujumla,Naibu
waziri Majaliwa alitumia fursa hiyo pia kuwataka madiwani waieleze jamii kuishi
vizuri na kuwapa ushirikiano walimu ambao watapangiwa kufanya kazi katika shule
zilizopo kwenye maeneo yao.
“Ndugu zangu madiwani tafadhari nawaombeni hebu jaribuni
mzungumze na jamii huko kwenye maeneo yenu kwani imezuka tabia ya kuwachezea
walimu kwa kuwalimisha usiku kucha,kuwalaza barabarani hadi asubuhi…..jamani
hii ni aibu”alisema Naibu waziri huyo akimaanisha vitendo vya kishirikina
wanavyodaiwa kufanyiwa baadhi ya walimu hasa walioko vijijini.
Naibu waziri Majaliwa ambaye alifanya ziara yake katika
wilaya zote za mkoa wa Tabora na kukagua baadhi ya shule,kuongea na walimu
pamoja na madiwani na wadau wengine wa elimu pia aliwataka kuwa na ushirikiano wa dhati katika harakati za kusimamia masuala ya elimu kwa shule za msingi na sekondari.
No comments:
Post a Comment