Askari wa jeshi la Polisi mkoani Tabora wamelazimika kutumia risasi za moto kuzima jaribio la kutaka kutoroka mahakamani watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui marehemu Mashaka Kalyuwa.
Tukio hilo ambalo lilidumu takribani kwa dakika kadhaa mitaa ya mahakama ya mkoa wa Tabora ambapo baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao kwa muda na kukimbilia kushuhudia milio ya risasi licha ya kuwa jambo hilo lilikuwa hatari kwa maisha yao.
Kwamujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha,watuhumiwa hao tisa wa kesi ya mauaji yaliyotokea tarehe 2 machi mwaka huu, waliletwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo inayowakabili.
Kamanda Rutha alisema wakati watuhumiwa hao wakipelekwa kwenye moja ya chumba cha kusikilizia kesi hatua chache kabla ya kuingia wanne kati yao walitimua mbio mbele ya ulinzi wa askari Polisi na kuanza kutokomea mitaani jambo ambalo askari Polisi waliokuwapo mahakamani hapo wakajaribu kuwakimbiza lakni ikashindikana.
Hata hivyo askari Polisi hao pamoja na kutoa amri halali iliyowataka watuhumiwa hao kusimama lakini waliendelea kukimbia jambo ambalo likawalazimu askari hao kuanza kufyatua risasi hewani mfululizo.
Wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya askari hao walifanikiwa kuwakamata wathumiwa watatu ambao ni Mihayo Mtima,Athuman Juma na Mashaka Shabani huku mtuhumiwa Masoud Said akatoweka kusikojulikana.
Kamanda Rutha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kumsaka mtuhumiwa huyo Masoud Said ambaye alidai kuwa ni hatari sana endapo kama ataendelea kukaa na jamii huko mitaani.
Kwaupande mwingine hakimu mkazi mfawidhi Bi.Cresencia Kisongo aliwahukumu kutumikia kifungo kwenda jela miaka miwili kila mmoja watuhumiwa hao watatu kufuatia mashtaka mawili yaliyofunguliwa dhidi yao kutokana na kufanya jaribio hilo la kutoroka mahakamani.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo hakimu mkazi mahakama ya mkoa wa Tabora Bw.Joctan Rushwela alilitaka jeshi la Polisi kuhakikisha kila mara wanapowaleta watuhumiwa hao wa kesi ya mauaji kuimarisha ulinzi na kuwafunga pingu wakati wote wawapo mahakamani.
No comments:
Post a Comment